Friday, July 31, 2009

KONDIC NAYE YUMO!!!!



Razak Khalfan mdogo wake Nizar Khalifan

Beki wa Yanga, Wisdom Ndlove
Vicent Barnabas

Kigi Makasi
Kipa wa Yanga, Nelson Kimathi ambaye amebeba mikoba ya Juma Kaseja
John Njoroge

Mohammed Bakari wa Yanga
Idd Mbaga wa Yanga
Kocha mkuu wa Yanga, Dusan Kondic (kushoto) akiwa anawaelekeza kitu baadhi ya wachezaji wa timu hiyo waliohudhuria mazoezi kwenye ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam (Picha na Seleman Mpochi)

Mazoezi Yanga yadoda

Na Jacqueline Massano, Coco Beach
HATIMAYE imekuwa! Zile tetesi za wachezaji wa Yanga huenda wakasusia mazoezi kutokana na kutolipwa mishahara yao ya miezi miwili, zimejidhihirisha leo baada ya wachezaji 10 tu kati ya 30 wa klabu hiyo kujitokeza kufanya mazoezi katika ufukweni wa bahari wa Coco.
Hali hiyo imeonekana mapema asubuhi wakati Alasiri ilipofika katika ufukweni huo kushuhudia mazoezi ya wachezaji hao ambao yanaendeshwa na kocha mkuu wa klabu hiyo, Dusan Kondic na wasaidizi wake.Alasiri iliwashuhudia wachezaji hao tisa wakijifua ufukweni huku watatu kati yao wakiwa wa kigeni na waliobaki ni wazawa.
Wachezaji waliojitokeza ni kipa Obren Curkovic, Nelson Kimati, Idd Mbaga, Shadrack Nsajigwa, John Njoroge, Wisdom Ndlove, Vicent Barnabas, Razack Khalfan, Bakari Mohammed na Kigi Makasi.
Hata hivyo, mwandishi wa gazeti hakuweza kuzungumza na kocha Kondic ila alifanikiwa kuzungumza na mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga, Emmanuel Mpangala ambaye alisema baadhi ya wachezaji wao ni wagonjwa.
Mpangala alisema mazoezi wanaofanya wachezaji hao ni magumu na ndiyo maana baadhi yao wakitoka mazoezini siku inayofuata wanashindwa kurudi tena mazoezini.
"Kwa kweli haya ni mazoezi magumu, ndiyo maana wengine wanashindwa kurudi kwani wakiamka kesho yake wanadai kuumwa," alisema Mpangala.
Aidha, Mpangala licha ya hao wanaosingizia kuumwa, lakini wengine ni wagonjwa wa kikweli kweli akiwemo Hamis Yusuph aliyepigwa na majambazi, Ally Msigwa (shingo), Boniface Ambani (nyonga), Athuman Idd (malaria), Shamte Ally (mguu) na Fred Mbuna (kifundo cha mguu).
Alipoulizwa kuhusiana na wachezaji wengine ambao hawajahudhiria mazoezi, bosi huyo amesema wataonekana kwenye mazoezi ya jioni yanayofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Alasiri ilipomuuliza kama ni kweli wachezaji hao wamegoma kuja uwanjani kwa sababu hawajalipwa mishahara yao, alisema: "Si kweli mbona hata jana walikuwepo."
Hivi karibuni baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo, walikaririwa wakidai kugomea mazoezi hadi hapo uongozi wao utakapowalipa mishahara yao ya miezi miwili.

Thursday, July 30, 2009

Man City yamnasa Kolo

London, England

Manchester City imerejea tena nyumbani kwa Arsenal na kumsajili beki mahiri wa Ivory Coast, Kolo Toure.
Kabla ya Toure, 28, Man City pia ilimsajilia mshambuliaji wa 'The Gunners', Emmanuel Adebayor mwanzoni mwa mwezi huu.
Beki huyo amesaini mkataba wa miaka minne, taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa na kocha Mark Hughes na kutumwa kwenye tovuti ya klabu hiyo ilisema jana.
Hakuna maelezo juu ya ada ya uhamisho iliyowekwa wazi mpaka sasa, lakini udadisi wa vyombo vya habari vya England, unaonyesha kuwa City imetumia paundi milioni 16 kukamilisha usajili.
City sasa iko kwenye mipango ya kujenga safu ya ulinzi baada ya kukamilisha safu ya ushambuliaji msimu huu."Sio siri kwamba kwa kipindi hiki tunajaribu kujenga safu ya ulinzi, na tunadhani kuja kwa Kolo ni kufanikiwa kwa zoezi letu la kujenga timu," alisema Mark Hughes.
Waliwahi kutaka kumsajili beki wa Everton, Joleon Lescott na Chelsea-John Terry, lakini ofa zao zilipigwa chini. Man City ambayo inaonekana pesa si tatizo kwa upande wao, tayari wameshamsajili Roque Santa Cruz wa Paraguay kutoka Blackburn Rovers, Carlos Tevez wa Argentina na Adebayor wa Togo.
Pia kiungo wa England, Gareth Barry naye amejiunga na City akitoka Aston Villa, na kufanya gharama yote ya kuwaleta wanasoka hao kufikia paundi milioni 90.
Kabla ya kujiunga na City, Toure alijiunga na Arsenal akitoka klabu ya Ivory Coast ya Asec Mimosas Februari 2002, na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa FA mwishoni mwa msimu wake wa kwanza mwaka 2003.
Beki huyo alikuwa tegemeo kubwa kwa Arsenal kiasi cha kuonekana chaguo namba moja la kocha Wenger sambamba na Sol Campbell msimu wa 2004, ambapo Arsenal ilicheza mechi nyingi bila kupoteza.

Wachezaji Yanga walia njaa

Na Mwandishi Wetu, Jijini
WAKATI Ligi Kuu ya Bara ikikaribia kuanza, baadhi ya wachezaji wa klabu ya Yanga, wamesema mpaka sasa hakieleweki kimaisha kutokana na uongozi kutowalipa mshahara yao ya miezi miwili ikiwa ni pamoja na wengine kutomaliziwa fedha zao za usajili.
Akizungumza na Alasiri kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wachezaji wa klabu hiyo (jina tunalo), amesema uongozi kwa sasa unawachukulia 'poa' na kuwaona kama watoto ndiyo maana wanashindwa kuwalipa mishahara yao.
"Siyo mishahara tu, wengine hawajamaliziwa fedha zao za usajili na hadi sasa hatujapewa mgawo wetu wa ubingwa. Lakini sisi ndiyo tunaolalamika ila wenzetu kutoka nchi jirani wako kimya kwa kuwa maisha yao yapo juu," alisema.
Mchezaji huyo amesema wachezaji wanapodai fedha zao uongozi unakuja juu na kuwatishia kuwasimamisha au kuwafukuza kwenye kambi.
"Hivi mtu unawezaje kufanyakazi bila kulipwa mshahara, wenyewe wanafurahia ushindi na wala si kingine. Timu ikivurunda wanakuja juu, lakini sisi tukidai chetu wanakuwa wakali, hivi tutaishi hivi hadi lini," alisema.
Amesema ingekuwa ni wachezaji wa kimataifa ndiyo wanadai fedha zao uongozi ungekwenda kukopa popote pale ili uweze kuwalipa lakini kwa kuwa ni wao wanawapuuza.
Akiongea zaidi kwa niaba ya wenzake, amesema kutokana na hali hiyo ya ukata, mazoezi ya timu hiyo yamedorora kufuatia baadhi ya wachezaji kususia.
"Wengine hawahudhurii hata kwenye mazoezi. Mazoezi bila pesa mkononi? nadhani haiwezekani."
Lakini wakati wachezaji hao wakilalamikia hayo, katibu mkuu wa Yanga, Lucas Kisasa, amegeuka Mbogo alipoulizwa madai hayo ya wachezaji.
Alisema kwa kufoka: "Mtaje mchezaji anayedai pesa Yanga.""Hivi nyie huko ofisini kwenu mmeshalipwa mishahara? Au, mkicheleweshewa mshahara mnajiandika kwenye magazeti? Alihoji na kuongeza: "Mnataka kuleta mgogoro klabuni wakati tumetulia kwa sasa...andikeni habari za jengo letu kukamilika, achana na stori kama hizo za mambo ya mishahara."

Tuesday, July 28, 2009

Mwalala ajuta kuitosa Yanga


Na Badru Kimwaga, Jijini

MSHAMBULIAJI nyota toka Kenya, Ben Mwalala ambaye amerejea Jijini Dar baada ya kushindwa majaribio ya kucheza soka la kulipwa huko China, anajuuta kuikosa klabu yake ya zamani Yanga katika michuano ya Ligi Kuu msimu huu.
Yanga iliamua kumtema Mwalala katika usajili wake msimu huu kwa madai anakwenda kusaka maisha klabu ya Zheijing Green Town FC, huku akiwa amemaliza mkataba wake, hivyo kukosa kucheza ligi nusu ya kwanza ya msimu, hivyo kwa sasa kuangalia ustaarabu mwingine wa kutafuta mahali pa kujihifadhi.
Akizungumza na Alasiri jana usiku, Mwalala alisema kwa sasa yupo Dar baada ya kurejea kwenye majaribio yake, bila kusema lolote kama atarejea nchini kwao Kenya kusaka timu ya kuichezea au ataenda wapi 'kutesti' zali.
"Aah nimesharudi bwana, mambo hayakuwa mazuri na kwa sasa napumzika kwanza, ila tutazungumza vema baadae," Mwalala alisema kwa ufupi alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi.
Hata hivyo kukwama kwa Mwalala kupata timu nje ya nchi imekuwa kama bahati mbaya kwake kwani klabu aliyokuwa akiichezea Yanga ilishamfungia milango katika usajili mpya kwa kumtema kufuatia kumaliza nae mkataba.
Kocha Mkuu wa Yanga, Dusan Kondic alinukuliwa kuwa, Mkenya huyo aisahau Yanga kwa sasa hadi utakapofika wakati wa usajili mdogo kuona kama wamsajili au la kulingana na kiwango atakachokuwa nacho.
Mwalala, ameachwa na Yanga akiwa na shujaa aliyeisaidia timu hiyo kufuta uteja wa miaka nane mfululizo kwa Simba kwa bao lake lililoipa ushindi wa bao 1-0 na pia kufunga bao jingine lililoipa Yanga sare ya mabao 2-2 kwa watani zao hao katika mechi ya pili ya ligi kuu msimu uliopita.

Monday, July 27, 2009

TAFCA kuchaguana Agosti

Na Jacqueline Massano, Jijini

CHAMA cha makocha wa mpira wa miguu Wilaya ya Kinondoni, TAFCA, kinatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu Agosti 9 mwaka huu.
Mwakilishi wa Chama hicho Kinondoni katika Mkutano mkuu wa TAFCA Taifa, Boniface Wambura amesema fomu za kuwania uongozi wa chama hicho zimeanza kutolewa jana.
Amesema fomu hizo zitakuwa zikipatikana katika ofisi za Chama cha Mpira wa Miguu Kinondoni, KIFA, na mwisho wa kuchukua na kurudisha umepangwa kuwa Agosti 3 mwaka huu.
Amezitaja nafasi zinazowaniwa kwenye uchaguzi huo kuwa ni ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu mkuu, katibu msaidizi, mhazini, mhazini msaidizi, mjumbe wa mkutano mkuu wa TAFCA na wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji.
Amesema wanaowania nafasi za juu za mwenyekiti hadi mweka hazina msaidizi watatakiwa kuchukua fomu kwa sh.10,000 huku nafasi ya ujumbe watachukua kwa sh. 5,000.
Wambura amesema usajili kwa wagombea unatarajia kufanyika Agosti 5 mwaka huu na wanachama ambao hawajaripa ada zao wanatakiwa kufanya hivyo.

Mambo si hayo


Ona walivyopendeza


Sunday, July 26, 2009

Maids wa Jimmy Charles

Kushoto ni Karama Kenyunko, Romana Mallya na wa mwisho ni Jacqueline Massano (Picha kwa hisani ya Omary Fungo)

Jack naye alikuwepo

Wasimamizi wa harusi ya Mr&Mrs Jimmy Charles ilifungiwa kwenye kanisa la Katoliki la Boko

Kikapu Afrika kutimua vumbi leo

Na Jacqueline Massano, Jijini
MASHINDANO ya mpira wa Kikapu ya Afrika Kanda ya tano yanatarajia kuanza kutimua vumbi leo hadi Agosti 2 mwaka huu nchini Uganda.

Katika mashindano hayo, Tanzania inatarajiwa kuwakilishwa na timu ya wanaume ya ABC na ya wanawake ya JKT.
Akizungumza na Alasiri, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini,TBF, Lawrence Cheyo amesema timu hizo mbili zimepata tiketi za kushiriki kwenye mashindano hayo baada ya kushika nafasi za juu kwenye ligi ya taifa ya Tanzania.
Amesema mbali ya Tanzania, nchi nyingine zinazotarajia kushiriki kwenye mashindano hayo ni Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Ethiopia, Eritrea, Somalia na Sudan.
Cheyo amesema anaimani kuwa timu hizo zimefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kwenda kushindana na kurudi na ushindi Tanzania.

Sunday, July 19, 2009

SIYO KUIMBA TU, HATA KUNENGUA ANAWEZA

Waimbaji wa bendi ya Twanga Pepeta wakionyesha vitu vyao jukwaani. (Picha kwa hisani ya Sabato Kasika).

HATA MIMI NAWEZA!!!

Muimbaji wa muziki wa dansi, Khadija Kimobiteli (Picha kwa hisani ya Sabato Kasika)

50 Cent afuta tattoo


HOLLYWOOD, Marekani

CURTIS "50 Cent" Jackson ameamua kuondoa baadhi ya michoro maarufu ya mwilini mwake, ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kufanikiwa katika fani yake mpya ya uchezaji wa filamu Hollywood.
"Nimefuta baadhi ya tattoo kwasababu wakati wa kurekodi filamu, kama tunatakiwa kufika pale saa 12.00, mimi nalazimika kufika saa 2.00 usiku wa jana yake," 50 Cent alisema.
"Nalazimika kuwa na masaa manne kwa ajili ya kufanyiwa marembo ya kuficha michoro ya mwilini mwangu.
Hivyo nimeamua kufuta michoro ya mkononi. Mkono wangu wa kulia.
"Muasisi huyo wa lebo ya G-Unit hata hivyo hajamaliza michoro mingi aliyo nayo mwilini. Bado ana michoro mikubwa miwili mgongoni, iliyoandikwa "50 Cent" na tattoo inayosomeka "Southside".
Hatua hiyo ya 50 Cent inakuja kufuatia nyota huyo kucheza kama nyota wa filamu ijayo ya 'Streets Of Blood'.
Filamu hiyo ya drama, ambayo inawahusisha pia Sharon Stone, Val Kilmer na Michael Biehn, inazungumzia magangwe wa mitaani na rushwa kwa mamlaka za polisi baada ya janga la Kimbunga cha Katrina mjini New Orleans.
Nje ya Hollywood, single mpya ya 50 Cent ya "Ok, You're Right" kutoka katika albam yake mpya inayosubiriwa sana ya 'Before I Self Destruct', imeendelea kuchezwa kwa kasi na vitu vya radio.
Rapa huyo pia ameachia "mixtape" zake mpya za "War Angel" na "Forever King', aliyoitunuku kwa Mfalme wa Pop, Michael Jackson.

Jada atamba 'kuduu' na Will Smith


NEW YORK, Marekani
KWA msanii yeyote, hakuna tuzo kubwa kama ya Oscar. Uwe katika orodha ya wanaowania tuzo, mshereheshaji au hata kuwepo pale ukumbini tu, kwasababu si rahisi kuona watu wakilikosa tukio hilo la kupita kwenye zulia jekundu.Na wakati hisia kwamba habari habari inayokuja ni ya ukumbini kwenye zulia jekundu, hilo waachie Will na Jada Pinkett-Smith wachague kilicho bora zaidi kwao. Kwa mujibu wa Jada, anachojali zaidi ni kutazamwa tu na Big Will kwa macho ya mvuto ili kuamsha 'mizuka' yake.“Ndani ya gari (limousine), tukiwa njiani kuelekea kwenye tuzo za Oscar mwaka huu, Will akaanza kuniangalia kwa jicho lile linalonifanya niwe chizi,” muigizaji huyo alisema kuliambia jarida la Shape. “Tukaanza kubusiana kimahaba, na kilichofuata...., unajua, wacha niseme tu kwamba tulikosa kuhudhuria kwenye zulia jekundu kwasababu vipodozi vyote nilivyojipamba vilikwisha.”Lakini kwa kuwa mambo hayo aliyafanya na mumewe Will, haizui mshangao. Hasa kama masimulizi hayo yametoka kwa mtu ambaye anayataja "mapenzi mengi" na mumewe kwenye magari, kwenye nyumba za rafiki zao, kwenye maduka ya mavazi na sehemu nyinginezo kama sehemu ya kudumisha ndoa yao na kuwafanya wasichokane.


Dikta afichua siri ya Michael Jackson

LOS ANGELES, Marekani

DAKTARI aliyempa Michael Jackson dawa zilizobadili rangi ya ngozi yake kuwa nyeupe Dk. Arnie Klein, amesema Mfalme wa Pop huyo kamwe hakupenda kuwa mzungu bali ni dawa zilizoidhuru ngozi yake.
"Michael alikuwa mweusi," alisema Dk Klein kuiambia CNN. "Alijivunia asili yake".
Dk Klein alisema kilichompa cha nyota huyo wa pop kuwa mweupe ni 'cream' alizompa kwa ajili ya kutibu ugonjwa wake wa ngozi uitwao Vitiligo, ambao hudhoofisha ngozi na kumtoa mtu madoa-doa.
Mtabibu huyo amesema ugonjwa huo ulimuanza Michael Jackson mkononi na kusambaa kote mwilini isipokuwa usoni.Mwanamama rafiki wa Michael, muigizaji Cicely Tyson, amesema soksi ya mkononi aliyoivaa Michael kwa mara ya kwanza kwenye video ya wimbo wake wa 'Billie Jean' ambayo ikaja kuwa kama alama yake ya kumtambulisha, aliibuni kwa ajili ya kuficha ugonjwa huo wa ngozi mkononi mwake.
"Mimi na Michael tulishea mbunifu wa mitindo kwenye miaka '80, na nilikuwepo pale pamoja nao wakati wakiibuni soksi ile ya mkononi," alisema Cicely kumwambia mtangazaji wa CNN Don Lemon.
"Nililazimika kubebwa mwamvuli," alisema Lee Thomas, ambaye aliandika kitabu cha maisha yake alichokiita 'Kugeuka Mweupe' ambacho kinasimulia mateso ya kimwili na kiakili anayoyapata Mmarekani Mweusi aliyebadilika rangi ya ngozi yake na kuwa mweupe baada ya kupatwa na ugonjwa wa ngozi wa Vitiligo.
Lee, mwandishi wa habari wa televisheni na mshindi wa tuzo ya Emmy wa Detroit, Michigan, aliiambia CNN alikumbwa na hali kama ya Michael Jackson."Nilitokwa na madoa meupe kwenye mkono wangu mmoja, nikalazimika kuvaa soksi ya mkono ili kushika mic wakati nikitangaza," alisema Lee.
Utetezi huu, huenda ukapunguza makali ya habari zilizokuwa zikiandikwa kumuelezea Michael ikiwemo iliyomtaja kama "mvulana 'hendisamu' mweusi aliyegeuka mwanamke mzee aliyechoka wa Kizungu".
Makala za sasa zimemtetea Michael kama mtu ambaye dunia imekuwa "ikimuonea" kwa kumshutumu kwa miaka mingi bila ya kuzingatia historia yake ya maisha ambapo "alinyimwa" nafasi ya kuwa mtoto.
Akiwa na umri wa miaka 10 tu tayari alikuwa ana majukumu ya ki-utuzima ya kutumbuiza katika ratiba ndefu na kuwaliwaza mashabiki, kazi alizozifanya chini ya uangalizi wa karibu wa baba yake Joe Jackson aliyekuwa akimuita "pua kubwa" na hata kumchapa anapokosea katika mazoezi ya bendi.
Ndio maana akaimba katika wimbo wake aliouita 'Childhood' uliokuwemo kwenye albam yake ya 'History': "Mmewahi kuniona nikiwa mtoto? Naitafuta dunia niliyotokea... hakuna mtu anayenielewa. Wanaona kama nafanya vitu vya ajabu.
Kwasababu nafanya utani wakati wote, kama mtoto, lakini hebu niacheni... Watu wanasema siko sawa eti kwasababu napenda mambo ya kitoto.
Ni wakati wangu kufidia maisha ya utoto ambayo sikupitia."Kutokana na kutamani maisha ya utoto, ndio sababu Michael hakutaka hata watoto wake waende shule akiona ndio njia sahihi ya kuwapa muda wa kutosha wa kufurahia kuwa watoto kitu ambacho yeye hakukipata. Lakini upendo wake wa kutaka kucheza na watoto ulimzulia kesi ya kudhalilisha mtoto kimapenzi, ambayo hata hivyo aliishinda.

MAPOZI HAYOOO!

Rapa Lil' Kim (kushoto) na mwimbaji Cyndi Lauper (kulia) wakiwa kwenye pozi.

Kaseba, Cheka uso kwa uso Oktoba

Na Jacqueline Massano, DDC Mwenge

BONDIA wa kick Boxing, Japhet Kaseba amesema yupo kwenye mazoezi makali kwa ajili yakujiandaa na pambano dhidi ya Francis Cheka wa Morogoro inayotarajia kufanyika Oktoba 3 mwaka huu. Kwa mujibu wa Kasebe, pambano hilo linatarajia kufanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.Cheka kwa sasa anashikilia mkanda wa Tanzania wakati Kaseba ni bingwa wa Kick Boxing.Kaseba amesema baada ya kuona kuwa Cheka amekosa mpinzani amaeamua kuingia kambini kwa ajili ya kujifua ili aweze kupambana naye."Nimepumzika kwanza Kick Boxing, na sasa najifua ngumi ili niweze kupanda uliongoni na Cheka ambaye hadi sasa hana mpinzani," alisemaBondia huyo amewataka wapenzi na mashabiki wa ngumi kujitokeza kwa wingi siku hiyo uwanjani kwa ajili ya kushuhudia pambano hilo ambalo anadai litabeba hisia za watu wengi."Kila mmoja naimani ana hamu ya kumuona Cheka anapigwa baada ya kushinda pambano lake mara mbili dhidi ya Rashid Matumla, lakini kwa sasa naawambia kuwa hatoki," alitamba bondia huyo.

Friday, July 17, 2009

Mr Tabasamu anayetaka kutoka na kila mtu


Mr Tabasamu anayetaka kutoka na kila mtu
Na Amour Hassan
RAPA wa Bongofleva Mr Blue anafahamu kuwa ni yeye 'mkubwa sana' katika gemu hii ya kizazi kipya.
Anafahamu kuwa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati jina lake linazungumzika vizuri.
Lakini pia anafahamu kuwa hajafika anakoelekea."Unaweza ukajiamini kuwa ni 'mkubwa' katika gemu hapa nyumbani halafu ukasahau kuwa wewe ni mtoto mchanga kabisa barani Afrika na kiwango cha dunia ni sawa na hujazaliwa kabisa," alisema rapa huyo alipozungumza na blogu ya jirushe-jiachie.
Blue alisema anafahamu kuwa kwa ukanda huu wa Afrika Masharariki na Kati ameshakubalika vyema lakini ana changamoto kubwa ya kufungua mipaka zaidi.
"Haina maana kufanya muziki halafu ukaishia kutamba nyumbani kwako tu. Ni sawa na kuimba bafuni wakati wa kuoga, wnaokusikia ni watu wa ndani kwenu tu na ni rahisi kukusifu hata kwa uongo. Changamoto ya kweli ni kufanya kitu kizuri kitakachoweza kukubalika nje. Watu wa nje wakikwambia kuwa unaweza hapo ndipo unapoweza kuamini kuwa unaweza," alisema.
Baada ya kuumaliza mwaka 2008 kwa kishindo kupitia wimbo wake wa 'Tabasamu' unaobamba kila kona kuanzia katika vituo vya radio, televisheni na klabu za burudani, Mr Blue amesema anataka kuendelea na kasi hiyo mwaka huu.

KUTOKA NA KILA MTU
Mistari ya hatari, kiitikio cha ukweli na 'biti' la kushiba vimetoa bonge la songi linalotosha kumfanya aliyenuna atabasamu.Na bila ya shaka, video ya kupania iliyofanywa na studio ya Kallaghe Pictures, imechangia umaarufu wa wimbo huo na, infact, imeitoa vyema kampuni hiyo ya video na kuifanya izungumziwe katika matawi ya kampuni inayotawala kwa muda mrefu ya Visual Lab.
Muunganiko wa vitu vikubwa katika maandalizi ya wimbo huo, umetosha kumrejesha vyema Blue ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu, ukiacha nyimbo mbili-tatu za kushirikishwa na wasanii wenzake.
Lakini katika marejeo yake ya 2009, Blue anataka kuufuta ukimya ambao ameukiri katika mashairi ya 'Tabasamu' pale aliporap: "Mr Blue vipi, mbona sikusikii tena, mbona sikusikii ukinena, mbona sikusikii ukisema."
Rapa huyo amesema amedhamiria kufanya mambo makubwa mwaka huu baada ya kuuanza vyema kwa wimbo wake huo aliofungia mwaka.
Baada ya mashabiki wa kizazi kipya kusikia kiitikio cha ukweli kutoka kwa msanii Steve aliyemtambulisha kwenye gemu kupitia wimbo huo wa 'Tabasamu', ambao chipukizi huyo amenata na 'biti' kama 'supastaa' mzoefu, Mr Blue anasema mwaka huu anataka kutoka na kila mtu.
"Natamani kila mtu atoke. Natamani kila mtu afanikiwe katika kile anachokifanya. Natamani kila mtu awe na maisha bora, natamani kila amtu awe na raha ya maisha," alisema. "Mmemshamsikia Steve, na sasa mwaka huu kuna wakali wengine wapya kibao wanakuja. Sitaki kukutajia kwa sasa kwa sababu kuongea sio staili yetu ya maisha, sisi ni vitendo tu, tunatoa 'pini' mashabiki wenyewe wanatuletea taarifa za mitaani huko watu wanavyopagawa."
Alisema kupitia mdhamini wake mpya Tippo wa Zizzou Fashion, ambaye pia anamdhamini rapa wa East Zoo Ngwair, amesema anatarajia kuachia single nyingine mwezi Machi.
"Nazipa muda nyimbo zangu kama ambavyo nimekuwa nikitoa miaka yote. Najua kwa kipindi hiki chote hadi Machi mashabiki watakuwa wanaendelea 'kutabasamu' tu," alisema.
Alisema hataji jina na wimbo kwa sababu maalum lakini umefanywa na aliyekuwa prodyuza wake wa muda mrefu marehemu Roy Bukuku wa G2 Records kabla hajafariki.
"Ni kwa ajili ya kumbukumbu ya prodyuza wangu," alisema rapa huyo ambaye jina lake la kuzaliwa ni Herry Samir.
Nyota huyo ambaye nyimbo zake zimekuwa zikifananishwa na maisha yake, alijikuta akiitwa Mr Blue kufuatia wimbo wake wa kwanza katika gemu ulioitwa 'Mr Blue'.
Wimbo wake mwingine wa 'Mapozi' ulimfanya pia ajulikane kama 'Bwana Mapozi'.
Lakini uwezo wake mkubwa katika gemu pia ulishuhudia rapa huyo akifunika hata katika nyimbo alizoshirikishwa kama 'Mbona' wa PNC, 'Joanita' wa Pingu na Deso, 'Nilikataa' wa Top Band akiwa na TID na Q-Chillah na 'Nipe Mkono' alioshirikishwa na Mrembo wa Milenia Miss Tanzania 2000 Jacqueline Ntuyabaliwe a.k.a K-Lynn.

Tuesday, July 14, 2009


Man City yamtega Adebayor

London, England
MANCHESTER City imesema imeamua kuzama mfukoni kupanga kutoa kiasi cha paundi milioni 25 kumsajili mshambuliaji Emmanuel Adebayor kutoka Arsenal.Kama 'dili' hilo litakamilika, basi nyota huyo kutoka taifa dogo Afrika--Togo, ataingia mkataba wa miaka mitano, na kumwezesha kulamba mshahara wa paundi za Kiingereza 130, 000 kwa wiki (zaidi ya shilingi milioni 260).Uamuzi wa kumnyemelea nyota huyo anayedaiwa 'kuchuja' kiwango Arsenal, umefikiwa baada ya kushindwa kumchomoa Samuel Eto'o kutoka Barcelona.Kocha Mark Hughes anatambua kwanini ni muhimu Adebayor kuziba nafasi ya Eto'o, hivyo anafanya juu chini kuhakikisha anamtwaa.Adebayor alikuwa akitarajia kwenda kujiunga na AC Milan ya Italia, ingawa tayari ana mkataba mrefu wa kucheza Emirates kwa mshahara wa paundi 80,000 kwa wiki.Bosi wa Washika Bunduki wa London, Arsene Wenger huenda akatumia pesa za mauzo ya Adebayor kumleta mshambuliaji wa Morocco Marouane Chamakh anayecheza Bordeaux.Kuondoka kwa Adebayor kunaweza kuwa furaha kwa baadhi ya mashabiki wa Arsenal ambao walikuwa wakimtazama kwa jicho la 'kutofaa' kubaki.Lakini City wanadhani kuwa nyota huyo anaweza kurejesha makali yake kama ilivyokuwa msimu wa mwaka 2007-08, alipoibuka kinara kwa kupachika wavuni mabao 30 akiwa na Gunners.
By Alasiri

Mauzo albamu za Jackson balaa

LONDON, England
ALBAMU za nyimbo za aliyekuwa bingwa wa midundo ya Pop Marekani, Michael Jackson zinazidi kushika chati za mauzo jijini London, nchini England, ambako mwanamuziki huyo alikuwa afanye onyesho lake la mwaka kabla ya kifo kumkuta.Albamu sita ziko kwenye chati za 10-bora, habari toka kwenye kampuni inayosimamia chati hizo za muziki ilisema jana.Albamu ya "The Essential", ndiyo inayoshika namba moja kwenye chati hizo.Bingwa huyo wa miondoko ya Pop, alifariki mwezi uliopita kutokana na kuugua ghafla ugonjwa wa moyo, ingawa bado kuna utata wa kifo chake.Nafasi ya tatu kwenye chati hizo, inashikiliwa na albamu yake ya "Off the Wall", ambayo wiki iliyopita ilikuwa katika nafasi ya 10, huku "Thriller", ikipanda mpaka nafasi ya sita.Albamu yake nyingine iliyomo kwenye 10-bora ni pamoja na "The Motown Years", iliyopigwa na Michael Jackson na kundi la Jackson Five, "Number Ones" na "Thriller 25". Wiki iliyopita, kampuni hiyo ilitangaza mauzo ya nakala 600,000 na hivyo kufanya nakala zilizouzwa tangu kufarika kwa Jackson kufikia milioni 1.5.

By Alasiri

Kabula kutoka na ushindi


Na Jacqueline Massano
Muimbaji wa muziki wa Injili nchini Kabula J. George anaratajia kuizindua albamu yake mpya aliyoipa jina la Ushindi yenye nyimbo nane ikiwa katima mfumo wa Tape, CD, VCD na DVD.Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa uzinduzi huo George Kayala alisema kuwa, uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Julai 5 mwaka huu katika ukumbi wa Matanta Msimbazi Center na maandali kwa ajili ya shughuli hiyo yanaendelea.Kayala alisema kuwa katika uzinduzi huo, kutakuwa na waimbaji wengi wakali wa muziki huo ambao kwa pamoja watakuwa na kazi ya kulihubiri Neno la Mungu kwa njia ya uimbaji.“Maandalizi yote kwa ajili ya uzinduzi wa Kabula yanaendelea, na siku hiyo kutakuwa na waimbaji mbalimbali ambao kwa pamoja watajumuika kulihubiri Neno la Mungu kwa njia ya uimbaji katika ukumbi huo,” alisema Kayala.Mratibu huyo alisema kuwa, nyimbo zote zilizomo katika albamu hiyo zinaupako wa ajabu kutokana na kuwagusa watu wengi ambapo wamekuwa wakizisikiliza na miongoni mwao wamekuwa wakipona magonjwa yao kwa njia ya kusikiliza vibao hivyo.

By Alasiri

Monday, July 13, 2009

Mshambuliaji wa pembeni wa Yanga, Mrisho Ngassa akionyesha machachari yake.

Yanga kuita wake kesho


Na Daniel Mkate

WAKATI klabu ya soka ya Simba inaanza rasmi mazoezi leo kwa ajili ya Ligi Kuu Bara msimu huu, uongozi wa mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga, umewaita wachezaji wake wote iliowasajili kuripori klabuni ifikapo kesho.Akizungumza na Alasiri mapema leo, mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya klabu hiyo, Emmanuel Mpangala, alisema wachezaji hao wameitwa kuripoti klabuni kwa ajili ya maandalizi ya ligi kuu."Tumeshawataarifu wachezaji wetu wote kuripoti klabuni ifikapo kesho, lakini muda wa kuingia kambini bado," alisema Mpangala.Mpangala alisema wachezaji hao wameitwa kwa ajili ya maandalizi ya ligi kuu inayotarajiwa kuanza Agosti 23 mwaka huu na kushirikisha timu 12.Hata hivyo, Yanga huenda ikatumia uwanja wake wa Kaunda kufanyia mazoezi pamoja na kuweka kambi kutokana na kukamilika kwa ukarabati wake wa mwaka mmoja na nusu.Mwenyekiti wa klabu hiyo, Iman Madega, awali alinukuliwa akisema timu yao itaweka kambi kwenye uwanja wake wa Kaunda baada ya kukamilika kwa asilimia kubwa ya ukarabati wake.Timu zitakazoshiriki ligi kuu pamoja na Yanga ni Simba, Manyema, Azam na African Lyon za Dar, JKT Ruvu ya Pwani, Mtibwa Sugar, Moro United za Morogoro, Prisons ya Mbeya, Majimaji ya Songea, Toto Afrika ya Mwanza na Kagera Sugar ya Kagera.

Ambani

Mshambuliaji wa Yanga Boniface Ambani akiwa uwanjani.

Simba mazoezini bila wageni

Simba
BAADA ya kukamilisha usajili wake, Simba imeanza mazoezi leo asubuhi ufukweni bila ya kuwa na wachezaji wake wa kigeni iliowasajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Bara, na wala kocha wao Patrick Phir ambaye bado yuko mapumziko Zambia.
Akizungumza na Alasiri mapema asubuhi, kocha msaidizi wa Simba, Amri Saidi amesema timu hiyo imeanza mazoezi kwenye ufukwe wa Coco kwa ajili ya maandalizi ya ligi hiyo.
Wachezaji hao wa kigeni ambao hawajafika mazoezini ni Emmanuel Okwi wa Uganda, Owino Joseph, Hilary Echesa (Kenya) na Danny Mrwanda.
Amesema wachezaji wote waliosajiliwa na klabu hiyo wamehudhuria kwenye mazoezi hayo isipokuwa wale wa kigeni.
Amewataja baadhi ya wachezaji waliohudhuria mazoezini kuwa ni Juma Kaseja, Uhuru Suleiman, Amri Kiemba, Ramadhan Haruna, Salum Gilla, Ulimboka Mwakingwe, Deo Bonivanture 'Dida'.
Wengine ni Salum Kanoni, Mohammed Kijuso, Mussa Hassan 'Mgosi', Haruna Moshi, Mustapha Ally 'Bartez', Salum Kanoni, Naftari David, Juma Nyoso, Nico Nyagawa na Kelvin Yondan.
"Wa kigeni bado hajaripoti kwani wanaendelea kukamilisha taratibu fulani ila kuanzia kesho nahisi tunaweza kwa nao," alisema
Amesema programu hiyo ya ufukweni itakuwa ya wiki moja ambapo baadaye watahamia kwenye kambi ya Bamba Beach iliyopo Kigamboni.
"Hii ni kwa ajili ya kuwapa stamina wachezaji wetu, na itawasaidia sana," alisema
Amri amesema mazoezi hayo yatakuwa ya kwenda na kurudi kabla ya kuiweka timu kambini tayari kwa kuingia msituni.

uchawi kwenye soka

Mchezaji wa kigeni afichua ushirikina ulivyogubika soka la Tanzania


Na Jacqueline Massano
MASUALA ya ushirikina katika soka ya nchi yetu ingawa yamekuwa yakizungumziwa kichinichini lakini kwa kweli kwa miaka mingi sasa yameonekana kushamiri katika soka ya nchi yetu.

Uchawi katika soka kwa kiasi kikubwa umekuwa hauzungumziwi waziwazi kutokana na sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa imani ikiwa suala hilo litazumgumzwa basi mtoa siri anaweza kudhurika.

Hata hivyo, kuna watu wachache waliokuwa na ubavu na kujitokeza waziwazi kuelezea jinsi, ambayo suala hilo lilivyo baya na linavyodumaza akili za wanasoka wetu.

Kutokana na ukweli kuwa basi kama kweli uchawi ungekuwa unafanya kazi basi timu ya soka ya taifa, Taifa Stars ingekuwa mabingwa wa dunia, Afrika lakini ushahidi wa suala hilo uko kwenye rekodi za michuano ya kimataifa.

Kama kweli suala hilo lingekuwa kuna nguvu katika soka basi kwa nini Simba, Yanga na timu nyingine zinaboronga kwenye mechi za kimataifa?

Imani za ushirikina, hata hivyo, limekuwa likiwekewa kipaumbele kuanzia soka ya ngazi za chini hadi kwenye ngazi ya taifa.

Mashabiki wa soka nchini kwa miaka mingi wamekuwa wakishuhudia vitendo mbalimbali vinavyoashiria soka yetu kugubikwa na imani za uchawi.

Hali hiyo ya imani za ushirikina imekuwa ikitawala kwa muda mrefu, ambao zaidi na hushuhudiwa kabla ya mechi za soka kuanza.

Kwa mfano kuna timu huamua kuruka ukuta wa uwanja kabla ya mechi kwa kuhofia pengine kutakuwa uchawi wa kuwadhuru kwenye geti la kuingilia uwanjani.

Kuna nyakati nyingine wachezaji huingia uwanjani bila ya kufunga kamba za viatu na kufungia uwanjani.

Hata hivyo, katika miaka ya 1980, kulikuwa kuna matumizi ya ndege aina ya njiwa kama ilivyotokea katika mechi ya Simba na Yanga mwaka 1981, ambapo mashabiki wa Simba walirusha njiwa aliyefungwa hirizi na baadae alishindwa kuruka kutoka uwanjani.

Pia bila ya kusahau vitendo vya kuvunja mayai uwanjani, ambavyo vimekuwa vikifanyika mara nyingi katika soka.

Kwa mfano mwaka 1974 wakati mshambuliaji wa Simba, Saad Ally alipoanguka katika mchezo dhidi ya Yanga, ambao Simba ililala 2-1 kwenye uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza kumekuwa kuna imani kwa hadi leo hii kuwa pale alipoangukia Saad hakuna jani lililoota hadi.

Mchezaji mmoja kigeni, ambaye anachezea timu mojawapo kubwa ya jijini Dar es Salaam na aliomba kuhifadhiwa jina lake kwa kuhofia kuzodolewa, alieleza ushirikina imekuwa sehemu ya maisha ya klabu hiyo anayochezea.

Alisema anaamini sababu kubwa inayofanya klabu za soka nchini kuliporomosha soka la Tanzania ni pamoja na wachezaji wake kujikita katika imani za uchawi.

Alisema imefikia wakati sasa uchawi umeingia katika damu za viongozi na wachezaji wa klabu kiasi cha kushindwa kuwaamini wachezaji wake na kuamua kuwapeleka kwa mganga ili waweze kuibuka na ushindi viwanjani.

Klabu hizo zinaamini haziwezi kufanya vizuri bila ya kujihusisha na masuala ya ushirikiana ikiwa ni pamoja na kwenda kwa mganga ili ziweze kupewa dawa ya ushindi.

Mchezaji huyo sio wa kwanza kulalamikia suala hilo, hata kocha wa zamani wa Yanga, marehemu Tambwe Leya aliwahi kulalamikia suala hilo wakati alipokuwa anainoa Yanga katika vipindi tofauti.

Tambwe mara ya kwanza alipokuja kufundisha Yanga katika miaka ya 1970, moja ya masuala, ambayo aliyapiga vita kwa kiasi kikubwa yalikuwa masuala ya uchawi katika soka.

Kocha, ambaye alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na muumini mkubwa wa kanisa la Katoliki, alifikia hatua kukorofishana na uongozi wa Yanga kutokana na masuala hayo.

Aliingia katika ugomvi mkubwa mwaka 1975, wakati wa maandalizi ya mechi ya robo fainali ya Klabu Bingwa ya Afrika dhidi ya Enugu Rangers ya Nigeria.

Yanga ilitolewa kwa sheria ya ugenini baada ya kufungana 1-1 jijini, Dar es Salaam lakini timu hizo zilikuwa zimeshindwa kufungana katika mchezo wa kwanza jijini Enugu.

Tambwe, hata hivyo, alilalamikia kuwa kitendo cha viongozi wa Yanga kuwafanyisha kwa muda mrefu masuala ya ushirikina na kuwafanya kushindwa kuzingatia mafunzo yake.

Pia mwaka 1995, aliporejea kuinoa Yanga kwa mara ya pili ilijikuta ikitolewa na Blackpool ya Zimbabwe kwenye robo fainali ya Kombe la Washindi baada ya kufungwa mechi zote mbili, Tambwe alilalamikia kitendo cha wachezaji kuamshwa usiku wa manane.

Mwaka 1996, Yanga kulifumuka mgogoro mkubwa wa matumizi mabaya ya fedha za Kombe la Hedex baada ya kudaiwa kuwa viongozi walitumia kiasi cha sh. milioni 3.3 kwa masuala ya ushirikina.

Pia Simba kumekuwa na kawaida ya kuchagua viongozi walio na uwezo wa kuifunga Yanga na hasa kwenye masuala ya ushirikina na sio katika masuala ya uongozi wa soka.

Ndio maana hata viongozi wa zamani wa Simba wamekuwa wakizungumziwa kwa sifa zaidi ya kuifunga Yanga na sio masuala ya kuendeleza klabu.

Kwa mfano kumekuwa kuna msemo kuwa Pan African imekuwa ikipanda na kushuka kutoka kwenye ligi kutokana na `kumzika fedha' mganga wao aliyewasaidia kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na ule wa Muungano mwaka 1982.


Vitendo hivyo vya kishirikina si kwa Tanzania pekee hata kwa nchi za Afrika ambazo zinaamini kuwa ushirikina ni moja ya silaha ya mafanikio katika soka na si vinginevyo.

Hata hivyo, ushirikina huo haupo tu kwa klabu kwani hata wachezaji nao wanaamini kuwa hawawezi kucheza soka uwanjani bila ya kufanya mambo ya kichawi kama vile kwenda kwa mganga kwa ajili ya kupewa kinga.

Mchezaji huyo alifichua hata baadhi ya wachezaji majina yao (tunayahifadhi) wanatuhumiwa kujihusisha na masuala ya kishirikina ikiwa ni pamoja na kusaka njia za kuwafanya wenzao wasicheze soka.

Wachezaji hao wanaamini hakuna kitu cha ziada ambacho kinaweza kutumika bila kukubali kujishughulisha na suala hilo la ubebaji wa 'matunguli' na ndiyo njia pekee ya kupata namba.

Pia alilalamia kuwa wachezaji wengi wa Tanzania hawaamini kucheza mpira bila ya kujihusisha na masuala ya ushirikina. Imani hiyo inawafanya baadhi yao kudiriki hata kuwaumiza wenzao kwa kuwaendea kwa waganga.

Kuna msemo wachezaji wengi huwa wanapenda kuutumua kuwa fulani amempigilia 'misuli' mwenzake ili achukue namba yake. Huu msemo unatumika sana kwenye soka hasa kwa baadhi ya wachezaji wenye tabia hizo za kishirikina.

Akizungumzia kuhusiana na suala hilo la ushirikina mmoja wa wachezaji wa klabu kubwa hapa nchini, anasema suala hilo la ushirikina lipo na amelishuhudia kwa macho yake kutoka kwa wachezaji na viongozi wa klabu hizo akifichua wakati hirizi ziliposhonwa katika jezi zao.

Alieleza baada ya kuona kitu hicho aligoma kuvaa jezi hiyo na baadae aligomea kitendo cha kupelekwa katika kambi ya maficho kwa ajili ya kufanya ushirikina wa kujihami kufungwa.

Mchezaji huyo anasema yeye binafsi haamini kama ushirikina ni moja ya njia mbadala ya kumfanya aweze kuwika katika medani ya soka. "Mimi binafsi siamini uchawi kwani nimekulia katika dini, inakuwa ni vigumu kuamini vitu kama hivyo.

"Kwa kweli tukiendelea hivi sidhani kama tutafika mbali, kwani wachezaji wengi wa kitanzania wanapenda sana ushirikina. Na hii inatokana na baadhi yao kutojiamini kama wanaweza," anasema mshambuliaji huyo wa kimataifa.

Anasema tangu amejiunga na timu hiyo mkubwa hapa nchini, amekutana na mambo mengi ya kutisha ambayo yanahusishwa na uchawi na hakuamini kama yanaweza kufanywa na klabu kubwa kama hiyo. "Siyo tu wachezaji, hata viongozi wanaamini kuwa hawawezi kupeleka timu uwanjani hadi waende kwa waganga," alisema.

Anafafanua kuwa wachezaji wakiona hawapangwi katika mechi huwa wanakimbilia kwa waganga kwa ajili ya kuelezea shida zao, kitu ambacho anadai si suluhisho katika soka.

"Kupangwa au kutopangwa kwenye mechi ni suala la kocha, na wala si kwenda kwa mganga kuomba msaada. Pia wanatakiwa wakumbuke kuwa juhudi ndiyo zinakufanya kocha akuone na kukupanga na wala si mganga." anasema kwa masikitiko.

Anaongeza kuwa wachezaji wengi wa Tanzania ni wavivu wa mazoezi na wala hawajitumi uwanjani na ndiyo maana wanapoona hawapangwi katika mechi wanaanza kuhisi kuwa fulani kamroga na yeye anaamua kwenda kwa mganga.

Kutokana na hali hiyo, mshambuliaji huyo anasema wachezaji wa aina hiyo mara nyingi huwa wanazeekea kwenye timu zao kwa sababu hawawezi kwenda kucheza soka popote pale kufuatia na imani zao za kishirikina.

Alisema kwa kiasi kikubwa hali hiyo imechangia wanasoka wengi kushindwa kupata nafasi ya kucheza Ulaya kutokana na kutokuwa fiti.

"Ulaya hakuna uchawi kwenye soka, kule ni vipaji tu. Na ndiyo maana hakuna mchezaji hata mmoja ambaye anaweza kupata timu nje, yote ni kwa sababu ya uchawi tu," anaongeza

Akitolea mfano wa timu za nje, anasema wachezaji wengi wa nje wanajituma kwenye mazoezi na wanashika kile wanachofundishwa na ndiyo maana wanawika na wala si masuala ya ushirikina.

"Ushirikiano ndiyo kitu pekee kwa wachezaji, siyo mwingine anawaza ushirikina mwingine anategea uwanjani kitu ambacho hakipo kabisa kwenye soka," alieleza.

Anasema ameshuhudia mara kadhaa viongozi wakizipeleka timu kwa waganga ili ziweze kufanya vizuri lakini haikusaidia kitu na matokeo yake timu inachapwa mabao mengi. "Haya sasa yule anayekwenda kwa mganga na asiyekwenda kwa mganga yupi bora?" alihoji mchezaji huyo.

"Hapa kinachotakiwa ni mbinu tu na wala si kupeleka wachezaji kwa waganga, huko hakuna mafanikio hata kidogo," anamalizia kwa kusema

Licha ya kauli hizo kutoka kwa mchezaji, klabu za Simba na Yanga mara kwa mara zimehusishwa katika matukio mbalimbali ya ushirikina hasa timu hizo mbili zinapokuwa zinakutana.

Pia baadhi ya wazee wa klabu hizo mbili wanaamini kuwa kwa kufanya hivyo, timu inaweza kufanya vizuri na kuibuka kwa ushindi na ndio maana huomba hata bajeti kubwa kwa sababu ya masuala hayo ambayo wameyabatiza kuwa ya `utendaji'.

====

Yanga yamsajili Bengo

WAKATI Simba ikiwa ina lengo la kumchukua kiungo wa klabu ya Villa ya Uganda, Stevin Bengo, watani zao wa Jadi, Yanga wamewazidi kete kwa kumchukua mchezaji huyo na kumfanyia majaribio.Yanga jana ilikuwa inawafanyia majaribio wachezaji wake wa kigeni kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.Habari zilizoifikia Alasiri jana uwanjani hapo, Simba ilikuwa na mpango wa kutaka kumsajili mchezaji huyo lakini ilishindikana baada ya kuzidiwa ujanja na Yanga ambayo iliizunguka.Inasemakana wakati kamati ya usajili ikiendelea kujipanga na kuhakikisha kuwa inamsajili mchezaji huyo, inakuja kutaamaki mchezaji huyo ameshaingia kwenye himaya ya Yanga.Hata hivyo, Alasiri ilipojaribu kuzungumza na mchezaji huyo alidai kwamba yeye alichofuata Tanzania ni kumalizana na uongozi wa Yanga na wala si vinginevyo."Mimi sijaja kwenye majaribio, nipo kwa ajili ya kujadiliana kitu na uongozi wa Yanga halafu naondoka narudi kwetu," alisemaMbali ya Bengo wachezaji wengine wenye nafasi kubwa ya kusajiliwa na Yanga, ni Mrwanda, Kamanzi Abdulkarim ambaye anachezea timu ya Alexander ya Ugiriki, na Kobongo Homole wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Mazoezi hayo yalionekana kuwa na msisimko baada ya mashabiki lukuki kujitokeza uwanjani hapo kwa ajili ya kuangalia vifaa hivyo vipya.Baadhi ya mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo walisikika wakiwafagilia zaidi wachezaji kutoka Uganda, Rwanda na wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
======