Saturday, October 31, 2009

Ronaldo amuita Rooney Real Madrid

(Wayne Rooney)
(Cristiano Ronaldo)
London, England
CRISTIANO Ronaldo amemshauri Wayne Rooney kumfuata Real Madrid. Mshambuliaji huyo wa bei mbaya, anasema Real inaweza kutisha zaidi iwapo itakuwa na nyota huyo wa Manchester United.
Ronaldo aliambia SunSport: "Wayne atafanya vizuri hapa. Nadhani anaweza kuwa msaada mkubwa kwetu.
"Itakuwa vizuri zaidi kama atakuja. Hii ni sehemu nzuri kwa wachezaji wa viwango vya juu duniani."Wayne ana ila kitu kinachoweza kumfanya kuwepo hapa.
"Ameweza kuonyesha waziwazi ni kwa kiasi gani amekuwa tishio England kwa miaka ya hivi karibuni.
"Na hakuna shaka kwamba hata akija hapa ataendelea kuwa juu. Itakuwa furaha kumuona siku moja hapa Real Madrid.
"Najua inaweza kuwa ngumu kwake kuja England."Anaipenda sana England, anaipenda Manchester, na isitoshe yeye ni kijana wa Liverpool Na United ni klabu nzuri kwake.
Lakini huwezi kujua nini kitatokea baadaye.
Ndoto ya Ronaldo kucheza Real imekumbana na matatizo baada ya kuumia kifundo cha mguu, huku timu yake ikipoteza mechi tatu kati ya tano ilizocheza.
Moja ya kipigo kibaya ni kile cha wiki hii cha mabao 4-0 dhidi ya timu ya daraja la tatu Alcorcon, ambapo kimemuweka pabaya kocha Manuel Pellegrini.

Kizungu champiga chenga Teves

London, England

CARLOS Tevez ameshauriwa kujifunza lugha ya kiingereza.
Mara nyingi Tevez, amekuwa akihitaji mkalimani kwa ajili ya kumsaidia kupokea maelezo pamoja na kuwepo England kwa miaka mitatu.
Lakini mwenzake kutoka Argentina, Pablo Zabaleta anaongea kiingereza kizuri katika kipindi cha miezi 12 tu England.
Na amemuambia Tevez wakati umefika wa kujifunza kiingereza.
Zabaleta, 24, alisema: "Ni muhimu. Najifunza kiingereza mara moja kwa wiki, na 'kizungu' kinaonyesha mafanikio sasa. najaribu, na kujaribu.
"Sikuwa naongea kiingereza kabla ya kuja, lakini kupitia masomo sasa naweza kuongea.
"Nimemwambia Carlos anaweza kuja kwangu ili nimfundishe."Wakati fulani anajaribu kuongea, lakini ni lazima kujifunza kwa sababu tunahitaji kuongea na wachezaji wenzetu na makocha.
"Na hasa ukizingatia kwa sasa tunaishi England."
'Kizungu' cha Zabaleta kinatia moyo hasa kwa mtu ambaye hakuweza hata kuongea neno alipojiunga na Man City akitoka Espanyol Agosti 2008.
Tevez, hajawahi hata siku moja kufanya mahojiano kwa kiingereza.Watu wengi wakiwemo waandishi wa habari walishangaa kuona mchezaji huyo akizungumza Kihispania wakati akitangaza kujiunga na City kutoka Man United pamoja na kukaa misimu miwili England.

Puyol aongeza mkataba Barca


MADRID, Hispania
NAHODHA wa Barcelona, Carles Puyol ameongeza mkataba mwingine tena wa miaka mitatu na mabingwa hao wa Barani Ulaya ambao unatarajia kumalizika Juni, 2013, klabu hiyo ilisema jana.
Dili hilo la beki huyo wa Hispania mwenye miaka 31, limegharimu dola milioni 14.8 za kimarekani, ambapo mkataba huo pia unatakiwa kumuwezesha kucheza asilimia 60 za mechi zote za klabu hiyo kwa msimu, Barcelona ilisema kupitia tovuti yake ya mawasiliano.
"Nina furaha na ninajiamini na klabu, benchi la ufundi na wachezaji wenzangu kwa kile walichonionyesha," Puyol aliiambia TV ya Barca

Friday, October 30, 2009

Nondo....mambo ya kulinda mtaji


Nyasi za Taifa kuwaka moto kesho

(kocha wa Simba-Patrick Phiri)
(Kocha wa Yanga-Kostadin Papic)

Na Badru Kimwaga, Jijini
VIGOGO vya soka nchini Simba na Yanga Jumamosi wanatarajiwa kuwa 'vitani' katika pambano la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2009-2010.
Hilo litakuwa pambano la 127 kati yao tangu mwaka 1953, likijumuisha ile ya ligi na mingineyo iwe ya vikombe au ya kirafiki.Katika mechi zao za awali 126, Yanga ndio wanaoongoza kwa kushinda mechi nyingi ukilinganisha na watani zao, wakiibuka kidedea mara 47 dhidi 42 za watani zao na kupata sare mechi 37.
Tangu 1965 kwa michezo ya ligi bila kujali kama ni ya Tanzania Bara au Muungano, Yanga imeshinda mechi 30 dhidi ya 25 za watani zao na sare mbalimbali ni mechi 27, huku Yanga ikifunga mabao 95 na kufungwa 82 na kujikusanyia jumla ya pointi 122 dhidi ya 101 za Simba.
Pamoja na Yanga kuongoza karibu kila mlolongo wa mechi za watani, bado imeshindwa kuvunja rekodi ya idadi kubwa ya magoli iliyowekwa na Simba Julai 19, 1977 walipolala mabao 6-0.Kipigo hicho kilichokuwa kisasi cha Simba dhidi ya Yanga iliyowalaza mabao 5-0 mnamo Juni Mosi, 1968, mpaka leo kimekuwa 'mzimu' unaoisumbua Yanga kwa miaka 32 sasa.
Katika mechi hiyo ya kihistoria mshambuliaji, Abdalla Kibaden 'King Mputa' alifunga mabao matatu peke yake, kitu kilichoshindwa kufanywa na mwingine katika historia za timu hizo katika ligi tangu 1965.
Hata hivyo wapo waliofunga mabao mawili katika mechi moja za watani hao ambapo kwa upande wa Yanga ni marehemu Maulid Dilunga, Saleh Zimbwe na Said Mwamba. Wengine ni Omar Husseni 'Keegan' na Idd Moshi.Kwa Simba wapo Jumanne Hassani 'Masimenti', Dua Said, Emmanuel Gabriel, Nico Nyagawa na Steven Mapunda 'Garincha'.
Beki Seleman Sanga wa Yanga ndiye wa kwanza kujifunga katika mechi za watani alipofanya hivyo mwaka 1977 katika kipigo cha mabao 6-0, Lilla Shomari wa Simba aliyejifunga 1983, Simba ikilala mabao 2-0 na Mustafa Hozza wa Simba alifanya hivyo 1996 Yanga na Simba zilipotoka sare ya 4-4 Omar Husseni 'Keegan' wa Yanga, nduye anayeongoza kwa kufunga magoli mengi katika mechi baina ya vigogo hivyo akiwa na goli sita akifuatiwa na marehemu Edward Chumila wa Simba mwenye mabao mabao matano.
Wachezaji Abeid Mziba 'Tekelo', Makumbi Juma 'Homa ya Jiji', Sekilojo Chambua na Idd Moshi wa Yanga na Dua Said wa Simba wanafuatia katika orodha hiyo kwa kufunga mabao manne kila mmoja.
Wapo waliofunga magoli matatu ambao ni Kibadeni, Kitwana Manara 'Popat' na Said Mwamba 'Kizota', huku kukiwa na orodha ndefu ya waliofunga mabao mawili na moja moja.
Zipo mechi zingine za vikombe kadhaa kama vile vya Tusker ama mechi za kirafiki timu hizo zimeweza kutambiana kwa zamu, lakini Simba ikiongoza kwa kushinda mechi nyingi.
Kwa mujibu wa kumbukumbu tulizonazo ni kwamba tangu mwaka 2001, Simba na Yanga zimekutana mara 17 katika ligi na Simba wakishinda mara nane huku watani wakitamba mara moja na wote wakapata sare mara nane.
Mara ya mwisho Yanga kula kichapo kwa Simba ilikuwa Oktoba 24, 2007 ilipolala bao 1-0, Morogoro kwa bao la Ulimboka Mwakingwe na kuzinduka mwaka jana walipoilaza Simba kwa bao la Mkenya Ben Mwalala.
Kwa kuangalia hali ilivyo Yanga katika mechi ijayo itakuwa na kazi kubwa ya kulinda ushindi wao wa mwaka jana na pia kuvunja rekodi ya miaka 32 ya Simba ya kipiugo cha mwaka 1977.Pia itataka kuzuia rekodi ya Simba ya kushinda mechi mfululizo bila kufungwa au kuambulia sare katika ligi ya msimu huu.
Yanga inayotetea taji la ligi hiyo, ina nyota kadhaa wa ndani na nje ya nchi ambao hata hivyo hawajaonyesha makeke kama wenzao wa Simba waliosajili 'mapro' watatu tu ambao tayari wameshaonyesha umahiri wao.
Wageni hao wa Simba ni pamoja na Joseph Owino, Hilary Ichessa na Emmanuel Okwi, ambao kila mmoja ameshafumainia nyavu, huku Yanga mgeni aliyefunga ni Mike Baraza, huku wengine wakivurunda.
Timu zote kama msimu uliopita zipo chini ya makocha wa kigeni, Simba ikiwa na Mzambia, Patric Phiri, Yanga ikinolewa na Mserbia Kostadin Papic aliyemrithi Dusan Kondic ambao wanambiana kuwa lazima timu zao zishinde.
Bila shaka pambano hilo la Jumamosi litakuwa lenye upinzani na litakaloweza kutoa picha ya nani atakayecheka msimu huu wakijiandaa kwenda mapumziko kwa ajili ya duru la pili la ligi hiyo.



Eeh! msikie huyu naye!


Jamani hata viazi nabeba!

(My first lady wa Barrack Obama, mama Michelle Obama akiwa na watoto wakisukuma kitoroli chenye viazi. Picha kwa Hisani ya Reuters)

Thursday, October 29, 2009

Rais amtetea kocha wa Real Madrid

(Manuel Pellegrini-Kocha wa Real Madrid)
(Florentino Perez-Rais wa Real Madrid)
MADRID, Hispania
KOCHA wa Real Madrid Manuel Pellegrini anahitaji "muda na utulivu" ili kukamilisha kibarua cha kukisuka kikosi chake ghali kuwa timu kamili, kwa mujibu wa rais wa klabu hiyo Florentino Perez.
Real Madrid bado inawewesekana kutokana na kipigo cha bao 4-0 ilichokipata Jumanne timu ya daraja la tatu ya Alcorcon katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Mfalme, na kuzua wasiwasi kkwa vyombo vya habari kuhusu hatma ya kocha huyo kabla ya mchezo wao wa Jumamosi wa La Liga dhidi ya Getafe.
"Napenda kupeleka ujumbe wa kuwatuliza wapenzi, "alisema Perez, aliyetumia euro milioni 250 (sawa na dola za Marekani milioni 369) kwa kununulia wachezaji kama akina Cristiano Ronaldo na Kaka katika kipindi kilichopita cha usajili.
"Inatakiwa kukumbuka kuwa wachezaji wengine wageni waliwasili kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi na hii inahitaji kipindi fulani cha kuzoea mazingira."
"Msimu huu ndio kwanza una miezi miwili na bado tunajaribu kuunda timu."
Tiny Alcorcon, aliyecheza katika ligi hiyo akiwa katika kikosi cha vijana cha Real Madrid na bajeti ya timu hiyo ilikuwa ndogo zaidi ya mara 400 zaidi ya vigogo hao wa Hispania, aliweza kukisambaratisha kikosi cha kocha Pellegrini licha ya kuwepo kwa mabeki wa Hispania Raul Albiol na Alvaro Arbeloa, na wachezaji wengine wa kimataifa.
Kipigo hicho kilifuatia suluhu ya wiki iliyopita huko Sporting Gijon katika La liga na kuruhusu mabingwa Barcelona kuongoza ligi hiyo kwa pointi tatu zaidi kileleni na kipigo cha 3-2 nyumbani dhidi ya Milan katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Akudo yatema wanenguaji wengine

Na Sabato Kasika, Jijini

BENDI ya Akudo 'Vijana wa Masauti, imeendelea na zoezi la kuwatema wanenguaji wake ambapo sasa wale waliorudishwa nyumbani kwao Kongo wamefikia watano.
Awali waliorudishwa kwa mara ya kwanza kutokana na kiwango chao cha kazi kushuka walikuwa watatu na sasa wameongezeka wengine wawili na kufanya idadi yao kuwa watano.
Meneja wa bendi hiyo Fadhil Mfate aliwataja waliotemwa awali kuwa ni Judith, Cerren na Shushuu ambapo wameongezeka wengine wawili aliowataja kwa majina ya Joseline na Fanny Bosawa.
"Nafasi hawa wawili zimeshachulikuwa na Bekham na Sandra ambao tayari wameshaanza kuonyesha makali yao ndani ya bendi ya Akudo Impact," amesema Mfate.
Amefafanua kuwa nafasi za wale watatu wa awali zitazibwa siku chache zijazo kwa madai kwamba kuna mtu ambaye uongozi wa bendi umemtuma Kongo kuleta wanenguaji wapya.
Amesema kabla ya kumtuma mtu kuwaleta, kulikuwa na mpango ambao walikubaliana na Werason kwamba angekuja kufanya onyesho nchini na kisha kuiachia Akudo wanenguaji watatu.
Amedai kuwa kwa vile bendi hiyo iko matawi ya juu, inataka wanenguaji wenye viwango ambao watasaidia kuifanya iendelee kubaki kwenye nafasi hiyo ambayo inang'ang'aniwa na bendi nyingi.
Wakati ikiendelea na maandalizi ya albamu ya pili, Akudo inatamba na nyimbo za albamu ya kwanza ya Impact ambazo baadhi yake ni 'Safari Sio Kifo', 'Walimwengu sio Binadamu', 'Yako Wapi Mapenzi'.

Jahazi kumtoa Daktari wa Mapenzi leo

Na Mwandishi Wetu

KUNDI la Jahazi Modern Taarab `Wana Nakshi Nakshi' leo litazindua albamu yake ya Daktari wa Mapenzi, katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa kundi hilo, Mfalme Mzee Yussuf alisema onyesho hilo litakuwa na aina yake na litapambwa na burudani kibao.
Pia, inaelezzwa kuwa uzinduzi huo utakwenda sambamba na sherehe za kundi hilo za kutimiza miaka mitatu tangu kundi hilo liliposajiliwa rasmi na kuanza kutoa burudani katika kumbi mbalimbali.
"Uzinduzi wetu wa Oktoba 30 (leo) utakwenda sambamba na birthday yetu ya kutimiza miaka mitatu tangu kundi liliposajiliwa rasmi, litakuwa onyesho kubwa sana na la aina yake, ambapo pia kutakuwa na wasanii wengine watakaopamba.
Mbali na Daktari ya Mapenzi inayobeba jina la albamu, vibao vingine vilivyomo katika albamu hiyo ni 'Chokochoko', 'Domo Kaya', 'Fungu la Mungu Sikosi' na 'Roho Mbaya Haijengi'.
Tayari nyimbo za albamu hiyo mpya zimesharekodiwa na zimeanza usikika katika vituo mbalimbali vya radio hapa nchini na zimeonyesha kupendwa sana.Tayari kundi hilo linatamba na albamu zake nne ambazo ni Two In One, Kazi ya Mungu, Tupendane na VIP, ambayo inaendelea kutesa hadi sasa kwa makali yake.
Kibao cha Daktari wa Mapenzi kilipigwa kwa mara ya kwanza Idd Mosi katika ukumbi wa Travertine na kuwachengua vilivyo wapenzi hasa kibwagizo chake kisemacho "Baridi, baridi imenishika..." na kuwafanya wapenzi kuwehuka.

Banana kushiriki Wahapahapa

Na Jimmy Charles

MWANAMUZIKI wa muziki wa kizazi kipya Banana Zoro anatarajia kushiriki kwenye tamasha kubwa la uzinduzi wa albamu ya 'Wahapahap'a inayotoa elimu juu ya kuwaepusha vijana na ngono zembe litakalofanyika Novemba 6, jijini Mbeya.
Afisa kutoka wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya Habari na Ukimwi, Benard Fimbo alisema lengo la tamasha hilo ni kutoa elimu kwa vijana juu ya kujiepusha na ngono ambazo zinaweza kuwasababishia kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Fimbo alisema katika miaka ya karibuni kwa kiasi kikubwa wasanii, wanahabari na mashirika binafsi yanayojihusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi wamesaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo tofauti na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Kwa upande wake mkurugenzi wa waandaaji wa tamasha hilo Deo Mwanansabi alisema mbali ya Banana kutoa burudani kwenye tamasha hilo pia kutakuwa na wanamuziki wengine wa hapa nchini.
Aliwataja wanamuziki hao kuwa ni Enika, bendi kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park na bendi ya Wahapahapa.
Mwanansabi alieleza kuwa mara baada ya tamasha la jijini Mbeya kumalizika wasanii hao watafunga safari hadi mkoani Iringa kwa ajili ya kufanya tamasha jingine lenye malengo ya kuwaelimisha vijana juu ya gonjwa hilo, ambapo hakutakuwa na kiingilio katika matamasha yote hayo.

Makomandoo Simba, Yanga kukipatapata

Na Jimmy Charles
SHIRIKISHO la soka nchini (TFF), limewachimba mkwara makomandoo wa timu za Yanga na Simba kuachana na mawazo ya kutaka kuingia bure kwenye mchezo wa watani hao uliopangwa kuchezwa kesho kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini jana, Afisa Habari wa TFF, Frolian Kaijage alisema kuwa TFF kwa kushirikiana na jeshi la Polisi wamejiandaa kuhakikisha hakuna mtu anayeingia bure.
Kaijage alieleza kuwa endapo mtu yeyote atakuwa na malengo hayo atakuwa amechelewa kwani hakutakuwa na nafasi ya bure kwa watu wasiokuwa na kazi maalum ndani ya uwanja huo.
"TFF imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila shabiki mwenye nia ya kutaka kushuhudia mchezo huo analipa kiingilio na kama yupo komandoo mwenye nia hiyo ni vema akafuta mawazo yake hayo,"alisema Kaijage.
Aliongeza kuwa mbali ya kutoa tahadhari kwa watu wenye kutaka kuingia bure lakini pia amewatahadharisha watu wenye nia ya kughushi tiketi ama kununua kwa wingi na kuziuza tena kuachana na mpango huo.
Kaijage alieleza kuwa TFF, kamati inayosimamia uwanja huo pamoja na jeshi la Polisi
wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanawadhibiti watu watakaokuwa na nia ya kutaka kujiingizia kipato kwa njia ya magendo.
Alitoa wito kwa mashabiki wa kweli wa timu hizo kujinunulia tiketi zao kweney maeneo yaliyopangwa ili kuepuka usumbufu.

Cheka na katuni....Kabwela anavituko


Simba yaipa Yanga maneno makali

Na Jacqueline Massano

WAKATI jobo la Yanga likitua Zanzibar jana na kutangaza kutembelea mazoezi ya watani zao wa Jadi, Simba, uongozi wa wekundu hao wa Msimbazi umeng'aka na kuwataka wana-yanga hao kutothubutu kufanya hivyo.
Baadhi ya wanachama hao wa Yanga wakiandamana na mwenyekiti wao, waliwasili Zanzibar jana kwa lengo la kwenda kufuata baraka kutoka kwa wazee na wanachama wengine waliopo huko.
Akizungumza mapema leo, meneja wa Simba, Innocent Njovu amesema kama Yanga wameenda Zanzibar kwa mambo yao na hawatajihusisha kwa namna yoyote na ziara yao.
Kauli hiyo, imekuja baada ya Yanga kudai kuwa leo inatarajia kutembelea mazoezi ya Simba yanayofanyika Mbweni, Zanzibar.
"Kama Yanga inakuja kwa ajili ya mambo yao, hatuna shida nao lakini kama safari yao inalenga kuvuruga kambi yetu, naomba niseme wazi kuha hatutakuwa tayari," alisema.
"Viongozi na wanachama wengine wa Yanga watakaokuja kwenye kambi yetu, wajiandae kujuta. Hatujahusika kwa namna yoyote na maandalizi yao, lakini wao wanaona kwetu ndio sehemu ya kufanya mchezo," alisema zaidi.
"Tunajua hata Yanga huku Zanzibar ina mashabiki wengi lakini inatakiwa kuzungumza na mashabiki wao, na wala si kutuingilia sisi," aliongeza.
Homa ya pambano hilo, limezidi kupata kila dakika kutokana na timu hizo mbili kuanza kuhisi kuhujimiwa.

Makinda wa Arsenal waizima Liverpool

LONDON, England

CHIPUKIZI wa Arsenal jana waliifanyia kweli Liverpool baada ya kuichapa mabao 2-1 katika mechi Kombe la Ligi, matokeo ambayo yanaivusha timu hiyo hatua ya robo fainali.
Katika mechi nyingine, Manchester City waliwachapa mabingwa wa daraja la pili, Scunthorpe United mabao 5-1, na kuingia hatua ya nane bora, huku Chelsea 'wakiiadabisha' Bolton Wanderers na kipigo cha mabao 4-0 kwenye uwanja wa Stamford Bridge.
washindi hao wanaungana na mabingwa watetezi Manchester United, washindi wa pili wa mwaka jana Tottenham Hotspur, Blackburn Rovers, Portsmouth na Aston Villa katika mechi za robo fainali ambazo zitazikutanisha timu zinazocheza Ligi Kuu ya England Jumamosi wiki hii.
Kocha wa Arsenal Arsene Wenger, akiiongoza timu yake kucheza mechi ya 750, aliweka imani kubwa kwa vijana wake na walifanya vizuri kwenye mechi.
Fran Merida, 19, kiungo wa kimataifa kutoka Hispania alikuwa wa kwanza kufunga bao kwa Arsenal baada ya dakika 19 tangu kuanza kwa mchezo, kabla ya Liverpool kusawazisha kwa bao safi la Emiliano Insua, likiwa la kwanza kwake katika mechi sita.
Liverpool, nayo ilijaza vijana kwenye mechi hiyo na kuonyesha kandanda safi lakini walishindwa kupata ushindi dhidi ya Arsenal katika kipindi cha miaka tisa.
Bao lililoitosa Liverpool lilifungwa na kwa shuti kali la mguu wa kushoto katika dakika ya 50 na mchezaji Niklas Bendtner.
"Kulikuwa na tofauti ndogo sana kati ya timu hizi," alisema kocha wa Arsenal Arsene Wenger wakati akiongea na Sky Sports.
"Kikosi chetu kilikuwa hatari, na chao pia kilikuwa hivyo, lakini nadhani kuna wachezaji wazuri na wenye uwezo kushinda taji msimu huu."
Kocha wa Liverpool Rafa Benitez, aliyefanya mabadiliko tisa kutoka kwenye kikosi kilichoifunga Manchester United Jumapili iliyopita aliipongeza timu yake na kusema kipigo hicho hakiusiana na ushindi wa Jumapili dhidi ya United.
"Ndio, hatuna raha kupoteza mchezo lakini kufungwa kwetu si hakuhusiani na ushindi wa United. Timu ilikuwa nyingine kabisa kwa sababu mashindano ni ya aina nyingine pia."
Manchester City, ambao hawajawahi kushinda kombe kubwa tangu mwaka 1976, ilikuwa ya kwanza kufunga bao kupitia kwa Stephen Ireland baada ya dakika tatu tangu kuanza kwa mchezo, kabla ya Jonathan Forte kusawazisha katika dakika ya 26.
City walirejea tena mbele kwa bao la pili kupitia kwa Roque Santa Cruz, likiwa bao lake la kwanza tangu ajiunge kutoka Blackburn Rovers.Mabao mengine yalifungwa Joleon Lescott, Carlos Tevez na Michael Johnson.
Chelsea nayo iliipeleka puta Bolton kwenye uwanja wa Stamford Bridge, huku Salomon Kalou, Florent Malouda, Deco na Didier Drogba wakiwa mashujaa baada ya kila mmoja kufunga bao.

Wednesday, October 28, 2009

Benitez amnyemelea Mata

London, England
RAFA Benitez yuko tayari kumsajili wingi wa kimataifa wa Valencia Juan Mata wakati wa usajili mdogo Januari mwakani..Mata, 21, amekuwa na wakati mgumu msimu huu, na Valencia wanaonekana kuwa tayari kumuuza kutokana na kukabiliwa na ukata.Huenda wakampiga bei kwa paundi za kiingereza milioni 16.Benitez ana uhakika kumnasa mchezaji huyo ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2012 kwa mshahara wa paundi 10,000 kwa mwenzi.Baba mzazi wa Mata, Juan Snr, ambaye pia ni agenti alisema: "Tunataka Valencia watambue kipaji cha kweli cha mtoto, na sio suala la pesa tu."Juan aliongeza: "Suala hili litamalizwa na klabu na wakala. Benitez ni kocha mkubwa, nataka kuweka mkazo kwenye soka bila usumbufu."

Eeh! manjonjo mengine bwana, haya sasa na nyinyi muige

Ronaldinho wa AC Milan, akimiliki mpira wakati wa mechi ya ligi kuu ya Italia 'Serie A' dhidi ya Napoli iliyochezwa uwanja wa San Paolo mjini Naples, jana. Picha: REUTERS

Raha si raha!

MCHEZAJI wa Arsenal, Fran Merida akishangilia baada ya kufunga goli dhidi ya Liverpool wakati wamechi ya Kombe la ligi iliyochezwa mjini London, jana. Arsenal ilishinda mabao 2-1. Picha: REUTERS

Du, poleni wapenzi wa Liverpool

Mikael Silvestre wa Arsenal,(juu) akimdhibiti vikali mchezaji wa Liverpool, David Ngog wakati wa mechi ya Kombe la Ligi iliyochezwa uwanja wa Emirates mjini London, jana. Picha REUTERS

Kaduguda amkimbia Mwalusako

Na Jimmy Charles
KATIBU Mkuu wa Simba Mwina Kaduguda jana alimkimbia Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga Lawrence Mwalusako katika mahojiano maalum juu ya mchezo wao wa keshokutwa yaliyoandaliwa na Radio One katika kipindi chake cha kumepambazuka michezo.
Kaduguda, Mwalusako na Afisa Habari wa Shirikisho la soka nchini (TFF),Frolian Kaijage walialikwa kwa pamoja kwenye kipindi hicho kwa ajili ya kuujadili mchezo huo wa Jumamosi, utakaochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo ni Mwalusako na Kaijage pekee ndio waliofika kwenye kipindi hicho kilichokuwa kikiongozwa na Maulidi Kitenge, ambapo Kaduguda alishindwa kuungana na wenzake.
Akizungumzia kitendo cha Katibu huyo wa Simba kuingia mitini Kitenge alieleza kuwa Kaduguda alipewa taarifa za kufika kwenye kipindi hiocho mapema lakini hawakujua nini kilimsibu hadi kushindwa kufika.
"Kaduguda ameshindwa kutokea ingawa alipewa taarifa za kushiriki kwenye kipindi hicho mapema,"alisema Kitenge.

Vodacom yamwaga tiketi kwa mashabiki

Na Jimmy Charles

KAMPUNI ya simu za mikononi ya Vodacom imetoa tiketi 20 za viti maalum kwa mashabiki 10 wa timu za Simba na Yanga kwa ajili ya kushuhudia mchezo utakaowakutanisha watani hao wa jadi keshokutwa.
Washindi hao kila mmoja atapatiwa tiketi mbili pamoja na kulipiwa gharama za usafiri kutoka maeneo wanayoishi pamoja na kulipiwa gharama za malazi na chakula kwa muda wa siku mbili.
Akiwatangaza washindi hao meneja matukio na promosheni wa Vodacom, Rukia Mtinwa alisema kuwa washindi hao kila mmoja anatakiwa kuja na jamaa yake mmoja, ambapo wote watalipiwa gharama zote muhimu.
Mtingwa aliwataja washindi hao kuwa ni Mary Kaduguda, Thabit Kaizer, Adam Chonya, Jingu Mseya na Rajabu Mhamila wote wakiwa ni mashabiki wa Simba.
Mashabiki wa Yanga walioshinda tiketi hizo pamoja na jezi za timu yao hiyo ni Muhidi Sufian, Issa K, Fulgence Ramadhani, Idrisa Mohamed na Maimbo Mkeia.
Wakati huo huo benki ya Stanbic imemchagua mshindi wa mwezi wa droo yake ya kwenda nchini Angola kushuhudia fainali za mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini humo, ambapo Meriso Suzan mkazi wa Arusha ameibuka kidedea.

Umeona mihela hiyoooo! Haya sasa kazi kwenu wadau


Hi!

I hope you are well.
Please advise me if I have drafted my resignation letter vizuri:


Dear Manager, I'm resigning with immediate effect - The reason for my resignation is what i found in my garage this morning before coming to work.


See for yourself...

Simba TMK kuikalia Yanga

Na Badru Kimwaga, Temeke

KATIKA kuhakikisha timu yao inaendelea na wimbi la ushindi kwa asilimia 100, wanachama wa klabu ya Simba wilaya ya Temeke, wanakutana jioni hii kupanga namna ya 'kuiua' Yanga wanayotarajia kukutana nayo katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Jumamosi wiki hii.
Wanakutana kuanzia saa 10 jioni pale kwenye makao yao makuu, Temeke Mwisho jijini Dar es Salaam siku mbili kwenye uwanja mkuu wa Taifa.
Akizungumza na Alasiri jana, Katibu wa matawi ya Simba-Temeke, Husseni Simba, alisema wamelazimika kukutana leo, ili kupanga mikakati na kusoma dua ya maangamizi ya kuiua Yanga siku ya Jumamosi.
Simba, alisema pamoja na kukiamini kikosi chao, lakini wameona ni bora kukutana kuisaidia kwa namna moja au nyingine timu yao kwa vile wanajua mechi za Simba na Yanga huwa zina mambo yake.
"Tunakutana kesho (leo) saa 10 jioni kwa ajili ya kupanga mikakati maalum na 'kuangusha' dua kuiombea mema timu yetu," alisema Simba.
Katibu huyo alisema kikao hicho kitawahusisha viongozi na wanachama wa klabu hiyo matawi ya Temeke na kuwahimiza wenzake kujitokeza mapema kabla ya saa 10 kitakapoanza kikosi hicho ambacho alisema kitajadili mambo mengine kadhaa yanayohusiana na klabu yao na matawi hayo ya Temeke.
Upande wa Yanga wamekuwa wapole katika majigambo tofauti na misimu miwili iliyopita ambapo timu hizo zilipokutana zilitoka sare mara mbili na mechi mbili kila upande ulishinda mechi moja moja.

Tuesday, October 27, 2009

Hatoki mtu hapa!

Serena Williams wa Marekani akirudisha mpira kwa Svetlana Kuznetsova wa Russia (hayupo pichani) wakati wa mashindano ya tenisi ya Ubingwa wa WTA Tour mjini Doha, jana. Picha :REUTERS

Yanga Chini ya Ulinzi

Na Jacqueline Massano, Jijini

ZIKIWA zimebaki siku mbili na masaa kadhaa, jiji la Dar es Salaam kutekwa na shamrashamra za mechi ya miamba ya soka nchini, uongozi wa klabu ya Yanga umewaweka wachezaji wake kwenye ulinzi mkali.
Yanga ambayo inajiandaa na mechi dhidi ya Simba itakayofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, imeweka kambi Jangwani makao makuu ya klabu yao iliopo mtaa wa Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Habari zilizoifikia Alasiri mapema leo na kuthibitishwa na mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, ni kwamba wachezaji hao hawaruhusiwi kukutana na mtu wa aina yeyote anayekwenda kambini hapo kwa lengo la kuwasalimia.
Mchezaji huyo amesema kutokana na mechi hiyo kwa sasa wachezaji hawaruhusiwi kutoka nje ya jengo hilo kutokana na ulinzi ambao umewekwa na wanachama wa klabu hiyo.
Amesema kutoka kwao nje ni kwenda kufanya mazoezi ambapo wanafanyia kwenye uwanja wao na kuingia ndani kwa ajili ya kupumzika.
"Ukionekana tu na hao wanachama unatoka nje au mtu akija hapa kambini ni balaa, yaani unazua balaa, si unajua wanachama wa Yanga walivyo? Hapa walipo wamelizunguka jengo letu."
"Si unajua tena maandalizi ndiyo yameanza, na sisi hatuendi kuweka kambi popote ni hapa hapa Jangwani, na ndiyo maana wanachama wamejaa, wengine wanalala hapa hapa nje. Hivyo sisi huwa tunakaa juu ghorofani tunawaangalia tu," alisema mchezaji huyo
Alipoulizwa kuhusu simu zao za mkononi alisema hajui kama wataendelea kuwa nazo au watanyang'anywa kama wanavyofanyiwa kwenye mechi za miaka mingine wanapokutana na watani zao hao wa Jadi.
"Kwa kweli simu sijui, maana hawa hawatabiriki, wanaweza kutunyang'anya au kutuachia," alisema

Maximo atangaza kikosi cha Stars

Na Mwandishi Wetu, Jijini

KOCHA Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo amewajumuisha kwa mara ya kwanza kwenye kikosi chake kinachotarajia kumenyana na timu ya taifa ya Misri Novemba 5 wachezaji watatu, ambapo mmoja kati yao anacheza soka la kulipwa nchini Msumbiji.
Mbali ya kuwaongeza wachezaji hao lakini pia Maximo amewarejesha kundini wachezaji sita ambao hawakuwepo kwenye kikosi chake kilichomenyana na timu ya taifa ya Rwanda mapema mwaka huu.
Maximo pia ameendelea kuwaita wachezaji wake wa kimataifa wanaocheza soka la kulipwa nchini Ulaya Henry Joseph, Nizar Khalfan na Nadir Haroub kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake.
Wachezaji wapya walioitwa na Maximo ni kipa Mohamed Mwalami anayecheza soka la kulipwa nchini Msumbiji kwenye klabu ya Ferroviaro,Agrey Morris wa Azam Fc na Said Ahmed wa Moro United.
Wachezaji waliorejeshwa kwenye kikosi hicho ni Ally Mustapha, David Naftari, Stephen Mwasika, Ibrahim Mwaipopo, Shabani Nditi na Abdullahim Amour.
Akitangaza kikosi hicho kwa niaba ya Maximo kocha mkuu wa timu za taifa za vijana, Rodrigo Stocler alisema kuwa uteuzi wa wachezaji hao umezingatia nidhamu, uwezo, umri na ushirikiano wao kwa wenzao.
Stocler alisema kikosi cha Stars kitakuwa na jumla ya wachezaji 36, ambapo kati yao wachezaji watano watatoka kweney timu za taifa za vijana.
Kikosi kamili cha Stars kinaundwa na makipa, Ally Mustapha,Shaban Dihile, Shabani Kado na Mohamed Mwalami,walinzi ni Agrey Morris, Shadrack Nsajigwa, Erasto Nyoni, Davis Naftari, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Salum Swedi, Juma Jabu na Stephen Mwasika.
Viungo ni Nurdin Bakari, Ibrahim Mwaipopo, Juma Nyoso, Shaban Nditi, Abdulahim Amour, Henry Joseph, Rashid Gumbo, Mwinyi Kazimoto,Kigi Makasi, Nizar Khalfan na Said Ahmed,washambuliaji ni Mrisho Ngassa, Mwana Sammata, Musa Mgosi, Danny Mrwanda,John Boko, Jerry Tegete na Zahoro Pazi.
Wachezaji kutoka timu za vijana ni Amani Kiata,Yusuph Soka, Himid Mao, Thomas Emmanuel wote kutoka timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 na Thabit kutoka timu ya vijana wenye umri wa miaka 17.

Mambo ya katuni hayooooo!


Dah! Sijui itakuwaje?

KOCHA WA TIMU YA TAIFA 'TAIFA STARS' MARCIO MAXIMO KUTAJA WATAKAOIVAA IVORY COAST

Micho aitabiria ushindi Yanga

Na Renatha Msungu

ALIYEKUWA kocha mkuu wa klabu ya Yanga, Milutin Sredejovic 'Micho' ameitabiria timu yake hiyo ya zamani kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani zao wa Jadi, Simba.
Yanga na Simba inatarajia kumenyana Jumamosi ya wiki hii jijini Dar es Salaam, kwenye mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Akitoa maoni yake kwa njia ya mtandao jana, kocha huyo ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya St. George ya Ethiopia, alisema Yanga ina asilimia kubwa ya kushinda mechi hiyo kwa sababu itakuwa imejiandaa kiakili tofauti na Simba.
Micho alisema mechi hiyo ambayo Simba imejiwekea matumaini ya kushinda itakuwa ni ngumu kwa sababu hata Yanga nayo imepania kuibuka na ushindi huo ili iliweze kutetea taji lake.
"Simba imeshajiwekea kushinda mechi hiyo kwa kuwa imeanza vizuri katika ligi hiyo na ndiyo maana hata mechi yake dhidi ya Yanga inaiona ni nyepesi tu," alisema Micho
Alifafanua zaidi kuwa Simba inaweza kupoteza mchezo huo kwa sababu itaingia uwanjani kwa kujiamini na pia tayari imeishaidharau Yanga kuwa haiwezi kushinda mechi hiyo.
Aidha, kocha huyo alisema aliwahi kushuhudia timu ikiingia uwanjani kwa kujiamini lakini hatimaye ilifungwa na timu ambayo haikuwa dalili ya kufanya vizuri kwenye mechi hiyo. "Simba inajiamini sana, lakini mimi nikiwa kama kocha mwenye uzoefu ikifanya mchezo inaweza kufungwa na Yanga tena bao 1-0 na wala si zaidi ya hapo, na ikijitahidi sana inaweza kutoka sare ya bao 1-1," alisema kocha huyo