Tuesday, December 29, 2009

Simba kuteta mwishoni mwa wiki

#Ni kujadili mabao mawili ya Yanga
Na Badru Kimwaga
VIONGOZI wa klabu ya Simba wanatarajia kuwekana 'kitimoto' na kujadili kipigo cha Yanga katika kikao chao cha Kamati ya Utendaji kitakachofanyika mwishoni mwa wiki.
Viongozi na wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji wameshajulishwa kikao hicho muhimu, ambacho pia kitatoa nafasi ya kujadili mambo mengine muhimu ya maendeleo ya klabu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu ya Simba, ni kwamba kikao hicho ambacho ni muendelezo ya kikao kilichofanyika awali Novemba 30 kitafanyika kwenye hoteli ya Regency.
Kubwa litakaloongelewa kwenye kikao hicho ni kipigo toka Yanga, uchaguzi mkuu na hoja ya mapato na matumizi ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu sasa.
Kamati hiyo inaundwa na Ayoub Semvua, Omar Gumbo, Mohammed Mjenga na Hassan Othman 'Hassanoo', iliyopewa kazi ya kukutana na TFF kwa lengo la kufanyia marekebisho ya katiba yao kabla ya kuitishwa kwa uchaguzi mkuu.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji, Said 'Seydou' Rubeya, alithibitisha kupata barua ya mualiko wa kikao hicho na kusisitiza anaenda kwenye kikao hicho kutaka majibu ya ombi lake juu ya mapato na matumizi ya klabu yao.

Kipigo kingine chaisubiri Simba

*Yanga yatamba
Na Jacqueline Massano

KATIKA mwendelezo wa kunogewa na furaha ya ushindi dhidi ya watani wao wa jadi Simba, mabingwa wa soka nchini, Yanga imesema ingetamani kupata nafasi nyingine ya 'kuionea' Simba wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajia kuanza baadaye mwezi ujao Visiwani, Zanzibar.
Yanga ilimaliza uchovu wa kutoondoka na furaha kila inapokutana na Simba baada ya kuwanyuka Wekundu hao wa Msimbazi mabao 2-1 katika mechi ya dakika 120--nusu fainali ya michuano ya Kombe la Tusker iliyomalizika kwa Yanga kutwaa ubingwa.
Simba, mabingwa wa soka nchini, Yanga na Mtibwa zitashiriki kutoka Bara, wakati wenyeji timu za Kisiwani Zenji ni pamoja na Malindi, Miembeni, Jamhuri, Zanzibar Ocean View na Mafunzo.
Afisa Uhusiano wa Yanga, Louis Sendeu amesema kuwa kikosi chako kwa sasa kiko imara kukabiliana na timu yoyote, na italeta furaha kama watakutana tena na Simba kwenye michuano hiyo.
Katika michuano ya Tusker, Simba ilimaliza kwa kushika nafasi ya tatu, kufuatia ushindi wa jasho jingi lililokauka baada ya dakika 120 na kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tusker ya Kenya katika mechi ya nusu fainali, huku Tusker ikikosa nafasi hiyo kiduchu baada ya kuwa mbele bao 1-0 mpaka dakika za majeruhi kabla ya Simba kusawazisha na kupelekea nyongeza ya dakika.
Alisema kuwa ushindi mafanikio mazuri waliyopatra kwenye michuano ya Tusker imefungua njia zaidi ya ushindani hasa katika michuano ya Ligi Kuu.
"Kama tutapangwa kundi moja na Simba, au ikatokea kukutana katika hatua yoyote, basi hii ndiyo furaha yetu. Kwa sasa tunaweza kuifunga Simba tunavyotaka. Ilikuwa makosa kudhani kwamba Simba haifungiki," alisema.
Wakati Yanga wakikosa mapumziko baada ya michuano ya Tusker, wapinzani wao Simba wako mapumzikoni mpaka Januari 2. Kwa mujibu wa Sendeu, timu yao inaanza mazoezi leo kwenye uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika, IST.
Hata hivyo taarifa za hofu kwamba Simba huenda isishiriki michuano hiyo, zimezimwa leo baada ya kuthibitisha ushiriki wao kupitia mtoa habari Clifford Ndimbo.
Ndimbo amesema kuwa, klabu yao itashiriki michuano hiyo kama ilivyopangwa, na kwamba wanatarajia kuanza mazoezi muda mfupi baada ya kurejea kocha Patrick Phiri aliyerudi zambia kwa mapumziko mafupi.

Monday, December 28, 2009

SOFAPAKA yawanyatia wawili wa Mtibwa


KLABU ya soka ya SOFAPAKA kutoka Kenya, imewazimia wachezaji wawili wa timu ya Mtibwa Sugar.
Fununu zilizoifikia blog hii ni kwamba uongozi wa klabu hiyo umeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na mabeki hao wa Mtibwa.
Wachezaji hao ambao wanaweza kulamba bingo hilo iwapo yatafikiwa makubaliano kati ya uongozi wa Mtibwa na Sofapaka ni Idrisa Rajabu na Abdulhim Amour.
Habari zilizopatikana ni kwamba endapo uongozi huo utafanikiwa kuwasajili wachezaji hao itawatumia kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

Yanga yaitisha Simba

UONGOZI wa klabu ya Simba umekiri mahasimu wao Yanga walistahili kutwaa ubingwa wa michuano ya kombe la Tusker kutokana na kujiandaa vizuri kuliko wao.
Aidha, uongozi huo umewataka wanachama wao kuacha kumsaka mchawi kwa matokeo yaliyowatokea katika michuano hiyo iliyomalizika jana, na badala yake kutakiwa kushikamana kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu nchini.
Katibu Msaidizi wa klabu hiyo, Mohammed Mjenga, alisema watani wao walionekana kubadilika kisoka kwa kucheza mpira wa pasi na kwa kiwango hicho walistahili kuwa mabingwa wa Tusker.
Mjenga alisema ni dhahiri Yanga walijiandaa vyema kwa michuano hiyo tofauti na Simba na ndio maana waliweza kuibuka washindi katika mechi yao na hawana la kusingizia zaidi ya kuridhika na matokeo.
Alisema hata hivyo pamoja na kuwapa heko watani zao, bado binafsi anawatupia lawama waamuzi kwa kuonyesha udhaifu katika michuano hiyo."Tatizo la waamuzi ni sugu na hatujui litaisha lini, ni kama hawajui wajibu wao wawapo uwanjani," alisema Mjenga.
Pia aliwataka wanachama wa Simba kuacha kumsaka mchawi kutokana na matokeo ya mechi yao na Yanga na badala yake kushikamana pamoja kwa ajili ya kujiandaa na duru la pili la ligi kuu pamoja na Kombe la Shirikisho.
Mjenga alisema, lawama kwa sasa wakati muafaka, ila umoja na mshikamano pamoja na kumsapoti kocha na wachezaji kwa michuano iliyopo mbele yao ndio kitu cha muhimu zaidi.

Simba wamgeuzia kibao Phiri

BAADA ya kuchapwa mabao 2-1na mahasimu wao Yanga katika mechi ya nusu fainali ya kombe la Tusker, Simba sasa wameamua kumgeuzia kibao kocha wao mkuu, Mzambia Patrick Phiri.
Baadhi ya mashabiki, wapenzi na manazi wa timu hiyo wamesema kocha huyo ndiyo sababu kubwa ya kufungwa na Yanga, na kisha wachezaji kucheza chini ya kiwango katika michuano hiyo iliyomalizika kwa klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani kutwaa taji.
Wakizungumza baada ya pambano lao la Alhamisi kumalizika, wapenzi hao wa Simba wakasema kitendo cha Phiri kuondoka na kwenda mapumzikoni nyumbani kwao Zambia na kuwapa mapumziko ya muda mrefu wachezaji, ndiyo sababu iliyosababisha wachezaji hao kuporomoka viwango.
"Kama kocha angekuwepo kambini na timu huko Zanzibar na kutoa mazoezi kama yale anayowapa katika Ligi Kuu Bara, basi wana imani wasingefungwa na kunyanyaswa na Yanga uwanjani na pia kuchukua ubingwa," alisema Muhidin Parojo mnazi wa Simba.
Simba timu inayochukuliwa kama ni kioo cha michuano hiyo, imecheza katika kiwango duni na kuwashangaza mashabiki waliozoea kuiona ikicheza Ligi Kuu mechi 11 bila kufungwa wala kutoka sare."
Katika mechi ua kusaka mshindi wa tatu, Simba waliishinda Tusker kwa mabao 2-1 na kushika nafasi ya tatu.Mashabiki wengi wamemtaka kocha Phiri kutowapa mapumziko tena wachezaji wake na badala yake awafanyishe mazoezi makali mara baada ya mwaka mpya kuanza.

Hali ilivyokuwa fainali Kombe la Tusker

Athuman Idd 'Chuji' akimzuia mchezaji wa Sofapaka wakati wa fainali za Kombe la Tusker zilizofanyika jana. Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kuchukua kombe hilo.
Kipa wa timu ya Sofapaka, Wilson Obungu akiwapigia kelele wachezaji wenzake wakati wa mechi ya fainali hizo.


Mshambuliaji wa pembeni wa Yanga, Mrisho Ngassa akiwatoka wachezaji wa Sofapaka.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga, wakiwa wamembeba kocha wao, Kostadin Papic mara baada ya kuchukua ubingwa jana.
Mshambuliaji wa Yanga, Jerry Tegete akionyesha kikombe juu baada ya kuzawadia alipoibuka kuwa mfungaji bora kwenye michuano hiyo. Pia mchezaji huyo alipewa dola 2,000.

Katibu mkuu wa Simba, Mwina Kaduguda akipokea mfano hundi ya sh. milioni 10 baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa tatu wa michuano hiyo.

Baadhi ya wachezaji wa Yanga, wakiwa na mwenyekiti wao Iman Madega wakishangilia baada ya kupewa kombe la Tusker.

Nahodha wa Yanga, Abdi Kassim 'Babi' na kocha mkuu wa timu hiyo, Papic akionyesha juu mfano wa hundi ya sh. milioni 40 baada ya kuibuka mabingwa wa michuano hiyo.

Wednesday, December 23, 2009

Simba yatamba kuitafuna Yanga

BAADA ya kuanza vizuri kwenye michuano ya Tusker, Simbari, imesema imejiwekea malengo ya kushinda mchezo wa kesho dhidi ya Yanga wa nusu fainali ya Kombe la Tusker ili kudumisha rekodi yake iliyoianza katika Ligi Kuu Bara.
Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na uhakika na imesema dhamira ya kushinda mchezo wa kesho inatokana na ubora wa wachezaji wake akiwemo mkongwe Mike Barasa katika safu ya ushambuliaji.
Kocha msaidizi wa Simba, Amri Said 'Jaap Stam' ameiambia Alasiri jana kuwa vijana wake wapo katika hali nzuri kwa silimia 99 na kwamba kuifunga Yanga pekee haitoshi bali inataka kuvikwa taji.
"Pamoja na kwamba Simba inaongoza kwa kulitwaa kombe hilo, lakini kitendo cha kukutana na Yanga katika hatua yoyote ni changamoto ya kipekee inayoisukuma Simba kushinda," alisema.
Alisema kuifunga Yanga katika mchezo wa leo kuna maana kubwa mbili, kwanza kutaiwezesha Simba kutinga fainali na pili kutaifanya imalize mwaka vizuri.
Amri alisema katika soka la Tanzania na nchi nyingine zenye mvuto wa mchezo huo, timu pinzani zinapokutana ni lazima ratiba za wapenzi zinavurugika kila mmoja akitaka kuiona.
"Sisi tunatambua hilo na ndiyo maana tumejiwekea malengo ya kushinda na baadaye kulitwaa kombe lenyewe," alisema.

Yanga kuingia mafichoni

KIKOSI cha wachezaji 26 wa mabingwa wa soka nchini, Yanga kinatarajia kuingia mafichoni jioni ya leo kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kesho dhidi ya watani wao wa Jadi, Simba.
Mechi hiyo ya nusu fainali ya pili ya michuano ya Kombe la Tusker inatarajia kufanyika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, inasemekana kuwa huenda Yanga ikamkosa mchezaji wake mmoja Stevin Bengo wa Uganda, ambaye yuko kwao kutokana na kuumwa.

Wednesday, December 9, 2009

Messi aongoza wanaowania tuzo

LONDON, England

NYOTA wa Barcelona Lionel Messi ana nafasi ya kuongeza tuzo ya mcheaji bora wa mwaka wa dunia wa FIFA katika zawadi yake ya mchezaji bora wa mwaka wa Ulaya ya Ballon d'Or.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye atakuwa mchezaji wa kwanza wa Argentina kushinda tuzo hiyo, yumo katika orodha hiyo pamoja na mchezaji mwenzake wa Barcelona Xavi na Andres Iniesta.
Anayeshikilia tuzo hiyo Cristiano Ronaldo na nyota mwenzake wa Real Madrid Kaka ndio wanaokamilisha orodha ya wachezaji wanaowania tuzo hiyo.
Mshambuliaji wa England Kelly Smith yumo katika orodha ya wachezaji wanmaowania tuzo kama hiyo kwa upande wa wanawake.
Messi, Xavi na Iniesta wanatengeneza muhimili wa timu ya Barcelona, na kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Primera Liga na Kombe la Ligi msimu uliopita.
Messi alipiga mpira wa kchwa uliopmpita kipa wa Manchester United Edwin van der Sar na kuiwezesha Barca kuibuka na ushindi wa bao 2-0 katika fainali iliyofanyika Rome nchini Italia.
Wiki iliyopita, Muargentina huyo alimbwaga Ronaldo kwa kura nyingi katika kinyang'anyiro cha kuwania tuzo ya mwanasoka bora wa Ulaya baada ya kupata pointi 473 dhidi ya 233.
Sasa mchezaji huyo anapewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo ya FIFA baada ya kuibuka wa pili nyuma ya Kaka katika kinyang'anyiro cha mwaka 2007 na alikuwa nyuma ya Ronaldo mwaka 2008.
Nyota wa England Steven Gerrard, Wayne Rooney, Frank Lampard na John Terry wote wameshindwa kuwemo katika orodha hiyo baada ya kuwemo katika kinyang'anyiro cha awali cha wachezaji 23 mwezi Oktoba.
England wanajisikia faraja baada ya mchezaji wao mmoja kuwemo katika orodha ya wachezaji wakike wanaowania tuzo hiyo ya mchezaji bora, Smith akiwa miongoni mwa wachezaji watano wanaowania tuzo hiyo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, ambaye anacheza soka Marekani, alikuwemo katika kikosi cha England kilichofikia fainali ya Euro 2009.
Wachezaji wengine wanaowania tuzo hiyo ni mshindi wa mwaka jana Marta na Mbrazil mwenzake Cristiane, pamoja na Wajerumani wawili Inka Grings na Birgit Prinz.
Kura hizo hupigwa na manahodha na makocha wakuu wa timu za taifa za wanaume na wanawake.

Saturday, December 5, 2009

RATIBA YA KOMBE LA DUNIA 2010

IJUMAA, JUNI 11, 2010
KUNDI A
Afrika Kusini v Mexico, Johannesburg (Soccer City)(1600)
Uruguay v Ufaransa, Cape Town (2030)

JUMAMOSI Juni 12
KUNDI B
Kusini Korea v Ugiriki, Port Elizabeth (1330)
Argentina v Nigeria, Johannesburg (Ellis Park) (1600)

KUNDI C
England v United States, Rustenburg (2030)

JUMAPILI, JUNI 13
KUNDI C
Algeria v Slovenia, Polokwane (1330)

KUNDI D
Serbia v Ghana, Pretoria (1600)
Ujerumani v Australia, Durban (2030)

JUMATATU, JUNI 14
KUNDI E
Netherlands v Denmark, Soccer City (1330)
Japan v Cameroon, Bloemfontein (1600)

KUNDI F
Italia v Paraguay, Cape Town (2030)

JUMANNE, JUNI 15
KUNDI F
New Zealand v Slovakia, Rustenburg (1330)

KUNDI G
Ivory Coast v Portugal, Port Elizabeth (1600)
Brazil v Korea Kaskazini, Ellis Park (2030)

JUMATANO, JUNI 16
KUNDI H
Honduras v Chile, Nelspruit (1330)
Spain v Switzerland, Durban (1600)

KUNDI A
Afrika Kusini v Uruguay, Pretoria (2030)

ALHAMIS, JUNI 17
KUNDI A
Ufaransa v Mexico, Polokwane (2030)

KUNDI B
Argentina v Korea Kusini, Soccer City (1330)
Ugiriki v Nigeria, Bloemfontein (1600)

IJUMAA, JUNI 18
KUNDI D
Ujerumani v Serbia, Port Elizabeth (1330)

KUNDI C
Slovenia v United States, Ellis Park (1600)
England v Algeria, Cape Town (2030)

JUMAMOSI, JUNI 19
KUNDI D
Ghana v Australia, Rustenburg (1600)

KUNDI E
Netherlands v Japan, Durban (1330)
Cameroon v Denmark, Pretoria (2030)

JUMAPILI, JUNI 20
KUNDI F
Slovakia v Paraguay, Bloemfontein (1330)
Italia v New Zealand, Nelspruit (1600)

KUNDI G
Brazil v Ivory Coast, Soccer City (2030)

JUMATATU, JUNI 21
KUNDI G
Portugal v Korea Kaskazini, Cape Town (1330)

KUNDI H
Chile v Switzerland, Port Elizabeth(1600)
Spain v Honduras, Ellis Park (2030)

JUMANNE, JUNI 22
KUNDI A
Mexico v Uruguay, Rustenburg (1600)
Ufaransa v Afrika Kusini, Bloemfontein (1600)

KUNDI B
Nigeria v Korea Kusini, Durban (2030)
Ugiriki v Argentina, Polokwane (2030)

JUMATANO, JUNI 23
KUNDI C
Slovenia v England, Port Elizabeth(1600)
United States v Algeria, Pretoria (1600)

KUNDI D
Australia v Serbia, Nelspruit (2030)
Ghana v Ujerumani, Soccer City (2030)

ALHAMIS, JUNI 24
KUNDI F
Slovakia v Italia, Ellis Park (1600)
Paraguay v New Zealand, Polokwane (1600)

KUNDI E
Denmark v Japan, Rustenburg (2030)
Cameroon v Netherlands, Cape Town (2030)

IJUMAA, JUNI 25
KUNDI G
Portugal v Brazil, Durban (1600)
Korea Kusini v Ivory Coast, Nelspruit (1600)

KUNDI H
Chile v Spain, Pretoria (2030)
Switzerland v Honduras, Bloemfontein (2030)

Hatua ya 16 bora inachezwa Juni 26 hadi 29
Robo fainali inachezwa Julai 2 na 3
Nusu fainali ni Julai 6 na 7
Mshindi wa tatu anapatikana Julai 10
Fainali ni Julai 11

Akina Dalali wapigwa Stop Msimbazi

*Waambiwa muda wao umekwisha
Na Badru Kimwaga

UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba chini ya Mwenyekiti wake, Hassani Dalali, umepigwa marufuku kuingia mkataba wowote na mtu, kampuni au taasisi yoyote kutokana na kumaliza muda wa wa uongozi tangu juzi.
Kwa mujibu wa barua iliyonaswa na Alasiri usiku wa kuamkia leo na iliyotiwa saini na Mdhamini wa klabu hiyo anayetambuliwa na serikali, Abdulwahab Abbas, ni kwamba uongozi huo wa Simba hauruhusiwa kuingia mkataba wowote kwa sasa kutokana na muda wao wa madarakani kumalizika.
Barua hiyo ya wazi, inasema kuwa kwa vile uongozi wa Simba uliingia madarakani Desemba 3, 2006 kwa mujibu wa katiba muda wao umemalizika juzi Desemba 3, 2009.
"Kwa maana hiyo iliyokuwa Kamati ya Utendaji au mjumbe wake hana uwezo wa kisheria kuingia mkataba wowote na mtu, kampuni au taasisi yoyote na mkataba huo ukawa na nguvu kisheria," sehemu ya barua hiyo inasomeka.
Barua hiyo ikatahadharisha kuwa, kwa vile kuna fununu za uongozi huo wa Simba kutaka kuingia mkataba wa muda mrefu wa kupangisha jesho la klabu yao lililopo mtaa wa Msimbazi, ni vema umma ukawa chonjo usilizwe.
"Yeyote atakayeingia mkataba na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kamati ya utendaji au chombo chochote kinachodai kufanya kazi kwa niaba ya kamati hiyo ya uongozi itakuwa imekula hasara kwani haitatambuliwa au kuhusika na mkataba huo wala kurudishiwa fedha zitakazotolewa kutimiliza mkataba huo,"
Blog hii ilijaribu kuwasiliana na Mwenyekiti Hassani Dalali kutaka kujua kama imeshaipata barua hiyo na ana maoni gani juu ya tahadhari hiyo, lakini simu yake ya mkononi haikuwa hewani.

Ratiba Kombe la Dunia 2010

IVORY COAST KUNDI GUMU
*Wenyeji kufungu dimba na Mexico
CAPE TOWN, Afrika Kusini

WAKATI wenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Dunia, Afrika Kusini wakianza kupamba historia ya michuano hiyo kufanyika Afrika kwa mara ya kwanza kwa kufungua dimba dhidi ya Mexico, mambo ni magumu kwa wawakilishi wengine wa Afrika, Ivory Coast ambayo imejikuta kwenye kundi gumu la fainali hizo zitakazoanza katikati ya mwaka ujao.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotewa jana na Shirikisho la Kimataifa la Soka Ulimwenguni-FIFA, Afrika Kusini iko Kundi A, sambamba na waliowahi kuwa mabingwa mwaka 1998 na washindi wa pili wa fainali zilizopita, Ufaransa na Uruguay.
Lakini kimbembe kiko Kundi G, ambako wawakilishi wa Afrika wanaotegemewa kufanya vizuri, Ivory Coast imejikuta kundi moja na Brazil--mabingwa wa mara tano wa fainali hizo, Ureno na Korea Kaskazini.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa, mechi ya ufunguzi itachezwa Juni 11, mjini Johannesburg kwenye uwanja wa Soccer City, na mechi ya fainali ya michuano hiyo ya 64 katika mtiririko wa kufanyika kwake, itachezwa kwenye uwanja huo huo, Julai 11.
Mabingwa Ulaya, Hispania ambao wanaongoza kwa ubora wa viwango kwa mujibu wa FIFA, wako Kundi H, sambamba na Uswisi, Honduras na Chile.
Tayari kocha wa Hispania, Vicente Del Bosque, ameshatamba kufanya vizuri kwenye kundi lake. "Hatuwezi kulalamika. Hatuwezi kuficha ukweli, sisi ni moja ya timu zenye uwezo mkubwa," alisema wakati akiongea na Sky Italia.
Lakini inaweza kujikuta kwenye wakati mgumu na kukutana na timu za Brazil na Ureno katika hatua ya 16-bora kutoka Kundi G.
Mabingwa watetezi, Italia, waliowachapa Ufaransa kwenye mechi ya fainali za mwaka 2006 nchini Ujerumani, wako kwenye kundi jepesi wakiwa na Paraguay, New Zealand na Slovakia wanaounda Kundi F.
Ujerumani nayo iko kwenye kundi gumu, ikijumuishwa na timu za Australia, Serbia na mwakilishi mwingine wa Afrika, Ghana wakiunda Kundi D.
Kwa upande wao, England watakumbana na Marekani waliowachapa bao 1-0 katika fainali za kukumbukwa za mwaka 1950, pamoja na Algeria na Slovenia Kundi C.
Upangaji wa ratiba hiyo ulishuhudiwa na rais wa sasa wa Afrika Kusini Jacob Zuma, viongozi wa FIFA akiwemo katibu mkuu Jerome Valcke na msanii wa filamu wa Afrika Kusini Charlize Theron.
Rais Zuma akiongea katika hafla hiyo alisema, ana hakika safari hii Kombe la Dunia litabaki Afrika kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, katika historia ya mashindano hayo, hakuna timu kutoka Afrika iliyowahi kufika nusu fainali.

Friday, December 4, 2009

Ratiba Kombe la Dunia kupangwa leo

CAPE TOWN, Afrika Kusini
AFRIKA Kusini imesema vitendo vyovyote vya kihalifu havitavumilika wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini humo, na kwa sababu hiyo imejiandaa vizuri kiusalama ambapo vifaa vya kisasa vya ulinzi vitatumika.
Nchi hiyo yenye rekodi mbaya ya matukio ya kihalifu lakini ikiwa nje ya ukanda wa kivita, imesema itaongeza idadi kubwa ya polisi wakati wa fainali hizo zitakazodumu kwa muda wa mwezi mmoja.
Tangazo hilo limekuja huku maafisa na mashabiki wakionyesha mashaka kutokana na kuendelea kwa vitendo vya uhalifu.
"Kwa sasa, wakati tunasubiri kupangwa kwa ratiba ya fainali za mwaka 2010, na zikiwa zimesalia siku kama 187 kabla ya kuanza kwa michuano, timejiandaa vya kutosha kwa asilimia 100," alisema Waziri wa Polisi, Nathi Mthethwa.
Ratiba ya michuano hiyo itakayozishirikisha timu 32, inatarajia kutolewa jioni ya leo, ambapo askari 1,000 wakashiriki katika kulinda usalama.
Mwanasoka wa kimataifa wa England, David Beckham anatarajia kushiriki katika hafla hiyo.
Mthethwa alisema polisi watasambazwa kwenye hotel, huku wengine wakiwa na nguo za kiraia, huku wengine wakifanya kazi kwa siri zaidi ili kupambana na vitendo vyovyote vya kihalifu.
Afrika Kusini iko katika mkakati mkali wa kupambana na matukio ya kihalifu wakati wa fainali za mwakani, ambapo serikali ya nchi hiyo imeuhakikishia ulimwengu kuwa usalama utakuwepo kwa asilimia 100 ili wageni wapatao 450,000 wakataokuja kushuhudia michuano hiiyo hawapati usumbufu.
Septemba mwaka huu, Mthethwa alitoa taarifa inayoonyesha kupungua kwa vitendo vya kihalifu kati ya Aprili 2008 to Machi 2009.

Bingwa 'World Cup' kulamba bil. 30

Afrika Kusini
BINGWA wa fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, atajinyakulia donge nono--dola mil. 30 (zaidi ya bil. 30), taarifa ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA lilisema jana kufuatia mkutano wake uliofanyika kwenye kisiwa cha Robin.
Aidha, mshindi wa pili atajinyakulia dola mil. 24 (sawa na bil. 24), huku kila timu itakayoshiriki ikipata bilioni 1 kama gharama ya maandalizi kwa ajili ya fainali hizo, taarifa zaidi ilisema.
Maamuzi hayo yalifikiwa jana katika kikao cha Kamati ya Utendaji cha FIFA kilichofanyika kwenye kisiwa cha Robben, nchini Afrika Kusini ambapo Nelson Mandela alishikiliwa kwa muda wa miaka 18 na utawala wa wazungu wakati huo.
Rais wa FIFA, Sepp Blatter na katibu mkuu wa Shirikisho hilo, Jerome Valcke walikuwa wakiongea na waandishi wa habari 250 waliosafiri na boti kutoka mji wa Cape Town kwenda kisiwa cha Robben.
Valcke alisema kuwa jumla ya zawadi zote kwa timu 32 ni shilingi bilioni 420, ikiwa ni ongezeko la asilimia 61 kutoka shilingi bilioni 261.4 kwenye fainali zilizofanyika nchini Ujerumani mwaka 2006.
Watakaofikia hatua ya nusu fainali watapata shilingi bilioni 20, wakati timu zitakazogusa hatua ya robo fainali zitanyakua bilioni 18, huku timu zitakazofikia raundi ya pili zitaondoka na bilioni 9, na zile zitakazotolewa kwenye hatua ya makundi kila mmoja ataondoka na bilioni 8.
Vile vile, Valcke alisema kuwa FIFA itatoa kiasi cha shilingi bilioni 40 kwa timu ambazo wachezaji wake watashiriki kwenye michuano hiyo.
"Kila klabu ambayo itakuwa na mchezaji kwenye fainali hizo, itapata kiasi cha milioni 1.8 kwa siku," alisema Valcke. "Pesa hizo zitalipwa siku 15 kabla ya kuanza kwa michuano, na siku moja baada ya wachezaji kuanza kucheza kwenye fainali hizo.
"Pesa ambazo zitalipwa klabu zitapitia kwenye vyama vya soka, huku pia vilabu vikikubali kutochukua hatua yoyote ya kudai fidia kupitia mahakama za madai, lakini kama ipo sababu, basi vitafanya hivyo kupitia FIFA, au CAS--mahakama ya kimataifa ya Michezo.

Wambura aishukia Simba

Na Daniel Mkate

HUKU akiendelea kupigwa 'danadana' kuhusu kadi mpya ya uanachama wa klabu ya Simba, Michael Wambura, ameutaka uongozi wa klabu hiyo umuuleze tatizo alilonalo kiasi cha kutopewa kadi yake.
Wambura alisema hajafahamu kosa alilofanya hata kusababisha kuzungushwa kukabidhiwa kadi yake.
"Sielewi huu uongozi unanigwaya nini, sijatangaza kuwania uongozi, ninachotaka ni kadi yangu tu ambayo ni mali yangu halali...sidaiwi, nimelipia ada zote za uanachama," alisema Wambura.
Alisema mpaka sasa anazungushwa kama 'daladala', kwani akienda kwa mhasibu wa klabu hiyo, Chano Almasi, anaambiwa aende kwa mwenyekiti Hassan Dalali ambaye 'humkimbia'.
"Dalali nikimpigia simu anakata na kisha kuzima kabisa, sasa sielewi nina tatizo gani kwa uongozi huo kwani kadi ni mali yangu wala haitakiwi kukalishwa vikao ili nipewe," alisema.
Aidha, Wambura alisema kadi hiyo yenye namba 2704, inaonekana anafanyiwa 'kauzibe' asipewe kwa lengo la kuwafurahisha watu fulani.
Wambura alisema iwapo viongozi hao wanadhani kukabidhiwa kadi hiyo kutamfanya awanie moja ya nafasi katika klabu hiyo, basi anawaomba wasiwe waoga wa uchaguzi.

Thursday, December 3, 2009

Nyoso, Makasi kuikosa Burundi


WACHEZAJI wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Kigi Makasi na Juma Nyoso kesho hawatakuwepo kwenye kikosi cha timu yao kutokana na kupewa kadi nyekundu katika mechi tofauti ya michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea mjini Nairobi, Kenya.
Stars inatarajia kushuka dimbani kesho kumenyana na Burundi ili iweze kupata tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo.
Nyoso alikuwa wa kwanza kulimwa kadi nyekundu wakati timu hiyo ilipokuwa inamenyana na Uganda na Stars kuchapwa bao 1-0, huku Makasi alilimwa kadi nyekundu wakati Stars ilipokuwa inacheza na Zanzibar Herous na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Papic akagua Kaunda

Na Jacqeline Massano
KOCHA mkuu wa mabingwa wa soka nchini, Yanga, Kostadin Kondic jana aliukagua Uwanja wa timu hiyo wa Kaunda uliopo makao makuu ya klabu hiyo ambao kwa sasa unaendelea na unaendelea na ularabati.
Afisa Habari wa mabingwa hao wa Jangwani, Loius Sendeu alisema Papic anataka uwanja huo ukarabatiwe haraka ili uweze kutumika kwa ajili ya mazoezi ya timu hiyo.
Anasema wakati wa kuukagua amegundua kuwa bado kuna mambo kadhaa hayajamaliziwa hivyo waliwataka wajenzi wa uwanja huo waharakishe ili umalizike kwa wakati.
"Kuna mambo madogo ambayo hayajamalizika, ila ukimalizika tu, timu itakuwa inautumia kwa ajili ya kufanya mazoezi ikiwa ni pamoja na kucheza mechi ndogondogo za kirafiki. Lakini wale wajenzi wamemuahidi kuwa utamalizika mapema," alisema
Wakati huo huo, Yanga imethibitisha kushiriki kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayotarajia kuanza kufanyika Jumamosi mjini Zanzibar.
Mashindano hayo ambayo fainali zake zinatarajia kufanyika Januari 12 mwakani, yanatarajia kuzishirikisha timu za Mtibwa Sugar, Yanga, Simba, Miembeni, Mafunzo, Malindi na Zanzibar Ocean View.

Arsenal, Chelsea nje Kombe la Ligi

Man U, Man City nusu fainali
London, England

MAJIRANI Manchester City na Manchester United, watakumbana katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Ligi, huku Blackburn Rovers wakikutana na Aston Villa katika hatua hiyo hiyo.
Blackburn Rovers ilipata ushindi jana baada ya kuwaangusha vinara wa Ligi Kuu England, Chelsea iliyokuwa na wachezaji 10 dimbani kwa penati 4-3 baada ya kumaliza dakika 120 kwa sare ya mabao 3-3 kwenye uwanja wa Ewood Park.
Chelsea walijikuta wakiwa nyuma mara mbili kabla ya kusawazisha bao katika dakika ya 122 na kupelekea mchezo kuamuliwa kwa njia ya mikwaju ya penati.
Matajiri wa Manchester, Manchester City 'waliwaonea' chipukizi wa Arsenal kwa kuwatandika mabao 3-0 katika mechi nyingine ya robo, matokeo ambayo sasa yatawakutanisha na majirani zao Manchester United katika hatua ya nusu fainali.
Ikicheza bila kocha wao, Sam Allardyce ambaye amefanyiwa upasuaji wa moyo, Blackburn ilikuwa ya kwanza kutikisa nyavu za Chelsea kupitia kwa mshambuliaji wa Croatia, Nikola Kalinic dakika tisa tangu kuanza kwa mchezo.
Kocha wa Chelsea, Carlo Ancelotti alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu kwa wakati mmoja, na dakika tatu baadaye mshambuliaji Didier Drogba aitumbukiza mpira wavuni, na kisha Salomon Kalou kufunga bao lingine na kuifanya Chelsea kuwa mbele kwa mabao 2-1, lakini Blackburn walisawazisha baada ya kipa Hilario kushindwa kucheza mpira wa krosi uliopigwa na Brett Emerton.
Kalou aliumia katika dakika ya 73 na kulazimika kutoka nje na hivyo Chelsea kubaki na wachezaji 10 uwanjani.
Blackburn walikwenda mbele na kufunga bao ndani ya muda wa nyongeza kupitia kwa mshambuliaji Benni McCarthy, lakini bao la Paulo Ferreira wa Chelsea lilifanya matokeo ya mwisho kuwa 3-3.
Kalinic na Michael Ballack wa Chelsea walikosa penati, kabla ya Robinson kuokoa mpira wa penati dhaifu ya Kakuta.

Wednesday, December 2, 2009

Yanga bado yamng'ang'ania Ambani

Jacqueline Massano, Jijini
PAMOJA na mshambuliaji Mkenya wa Yanga, Boniface Ambani kusisitiza hana mpango na timu hiyo, lakini uongozi wa klabu hiyo umezidi kudai kuwa ni mchezaji wao halali kutokana na kutompatia barua yoyote ya kusitisha mkataba wake.
Kauli ya Yanga, imekuja baada ya mshambuliaji huyo mrefu wa Kenya kusisitiza kutotambua kurejeshwa kwake kundini baada ya awali kuonekana 'kudhalilishwa' kwenye vyombo vya habari kwamba ametemwa kwa kushuka kwa kiwango chake cha uchezaji.
"Ni kweli awali tulikuwa na mpango wa kumuacha, na tulipanga kumpa barua ya kusitisha mkataba wake atakaporudi kutoka Kenya, lakini tumesitisha uamuzi wetu baada ya kuona hajapata timu ya kuchezea hadi sasa.
"Na sheria za Shirikisho la Soka nchini,TFF, ni kwamba kama klabu inataka kumuacha mchezaji mwenye mkataba ni lazima awe amepata timu kwanza," alisema Afisa Habari wa Yanga Luis Sendeu alipokuwa akizungumza na blog hii asubuhi ya leo
Sendeu alisema kinachotakiwa ni mchezaji huyo kuja nchini kwa ajili ya kujiunga na wenzake ambao wanaendelea na mazoezi na wala si kusikiliza maneno ya vyombo vya habari.
"Kama Ambani atakuwa anafanyakazi na vyombo vya habari atakuwa anafanya makosa, anachotakiwa ni kuwasikiliza viongozi wake, kwani sisi hatujampa barua ya kukatisha mkataba wake," alisema.
Alisema ikiwa mchezaji huyo ataamua kukatisha mkataba yeye mwenyewe atatakiwa kuilipa Yanga na wala si vinginevyo.
Sakata la Yanga na mchezaji huyo kwa sasa limeingiliwa na TFF, ambayo imethibitisha kuwa Ambani ni mchezaji halali wa Yanga kwa kuwa bado ana mkataba nayo.
PAMOJA na mshambuliaji Mkenya wa Yanga, Boniface Ambani kusisitiza hana mpango na timu hiyo, lakini uongozi wa klabu hiyo umezidi kudai kuwa ni mchezaji wao halali kutokana na kutompatia barua yoyote ya kusitisha mkataba wake.Kauli ya Yanga, imekuja baada ya mshambuliaji huyo mrefu wa Kenya kusisitiza kutotambua kurejeshwa kwake kundini baada ya awali kuonekana 'kudhalilishwa' kwenye vyombo vya habari kwamba ametemwa kwa kushuka kwa kiwango chake cha uchezaji."Ni kweli awali tulikuwa na mpango wa kumuacha, na tulipanga kumpa barua ya kusitisha mkataba wake kutoka Kenya, lakini tumesitisha uamuzi wetu baada ya kuona hajapata timu ya kuchezea hadi sasa."Na sheria za Shirikisho la Soka nchini,TFF, ni kwamba kama klabu inataka kumuacha mchezaji mwenye mkataba ni lazima awe amepata timu kwanza," alisema Afisa Habari wa Yanga Luis Sendeu alipokuwa anazungumza na Alasiri mapema leo.Sendeu alisema kinachotakiwa ni mchezaji huyo kuja nchini kwa ajili ya kujiunga na wenzake ambao wanaendelea na mazoezi na wala si kusikiliza maneno ya vyombo vya habari."Kama Ambani atakuwa anafanyakazi na vyombo vya habari atakuwa anafanya makosa, anachotakiwa ni kuwasikiliza viongozi wake, kwani sisi hatujampa barua ya kukatisha mkataba wake," alisema.Alisema ikiwa mchezaji huyo ataamua kukatisha mkataba yeye mwenyewe atatakiwa kuilipa Yanga na wala si vinginevyo.Sakata la Yanga na mchezaji huyo kwa sasa limeingiliwa na TFF, ambayo imethibitisha kuwa Ambani ni mchezaji halali wa Yanga kwa kuwa bado ana mkataba nayo.

Man Utd yaiadhibu Spurs

LONDON, England
Mchezaji Darron Gibson jana aliwawezesha mabingwa Manchester United kucheza hatua ya nne-bora ya Kombe Ligi kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tottenham Hotspur, matokeo ambayo yamezima ndoto za wapinzani wao kucheza hatua ya fainali ya michuano hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo.
United, waliowachapa kwa mikwaju ya penati Spurs msimu uliokwisha kwenye uwanja wa Wembley, watakumbana na Aston Villa katika mchezo wa nusu fainali baada ya wao nao kupata ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Portsmouth 4-2 kwenye uwanja wa Fratton Park.
'Matajiri' Manchester City watakutana na Arsenal, huku vinara wa Ligi Kuu ya England Chelsea ikisafiri kuifuata Blackburn Rovers katika mechi za robo fainali zitakazochezwa leo.
Kiungo wa kimataifa wa Ireland, Gibson alikuwa wa kwanza kupachika bao wavuni katika dakika ya 16, kabla ya kuongeza bao lingine katika dakika ya 22 kwa shuti kali la umbali wa mita 18. Kikosi cha vijana wa United kilicheza vizuri, lakini walikuwa Tottenham waliong'ara zaidi hasa kipindi cha kwanza wakisaka ushindi wa kwanza kwenye uwanja wa Old Trafford katika kipindi cha miaka 20.
Jermain Defoe kidogo afunge bao baada ya kumjaribu kipa wa United, Tomasz Kuszczak kwa shuti katika dakika ya saba tu, na alikuwa na nafasi nyingine nzuri ya kusawazisha makosa ya awali katika dakika ya 21 lakini jitihada zaje zilizuiwa na beki Nemanja Vidic

Baadhi ya wachezaji waliosajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara

Nadir Haroub 'Canavaro' mchezaji ambaye alikuwa anachezea White Caps Vancouver ya Canada lakini kwa sasa amesajiliwa tena kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga aliyokuwa anaichezea kabla ya kwenda Canada.
Baada ya kuichezea Yanga na kutemwa, akaenda Kagera Sugar na hatimaye sasa hivi ameangukia mikononi mwa maafande wa Prisons ya Mbeya.



Tuesday, December 1, 2009

Wasomi kuchuana Tanga

Na Renatha Msungu
SHIRIKISHO la michezo ya vyuo vikuu Tanzania (TUSA) limeandaa mashindano ya michezo ya Vyuo Vikuu yaliyopangwa kufanyika kesho hadi Desemba 11 katika viwanja vya Mkwakwani vilivyopo jijini Tanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Syllersaid Mziray alisema mechi ya ufunguzi katika mashindano hayo ambayo mgeni rasmi atakuwa mkuu wa mkoa wa Tanga Said Kalembo itakuwa kati ya timu ya UDSM, na ST Stephano.
Mziray ameitaja michezo itayochezwa kwenye mashindano hayo kuwa ni soka, netiboli, mpira wa kikapu, Wavu, Meza, Riadha na mchezo wa kuvuta kamba.Amesema jumla ya wanafunzi 700 wanatarajia kushiriki katika mashindano hayo ambayo yatashirikisha timu za wanawake na wanaume kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.
Mziray amesema mabingwa watetezi kwa upande wa soka ni ni timu ya UDSM, wakati kwa upande mpira wa Wavu ni Chuo cha Ardhi, huku mpira wa Kikapu ni timu ya TUDARCO, na netiboli ni chuo cha Makumira na kwa upande wa Riadha ni UDSM.
Amevitaja vyuo ambavyo vimethibitisha kushiriki katika mashindano hayo kuwa ni Chuo cha Ardhi, Chuo Kikuu Huria, UDSM, SUZA, Chuo cha Zanzibar, Chuo Kikuu cha Tumaini cha Dar es Salaam, Tumaini Iringa, MUCOPS na DUCE.
Vyuo vingine Chuo cha Mount Meru, Makumira, MUCE, KCMC, Kairuki, Mzumbe, SUA, UDOM na ST John.Wakati huo huo, TUSA imevitaka vyuo ambavyo bado havijathibitisha ushiriki wao kuthibitisha kabla ya tarehe ya kuanza kwa mashindano hayo.

Ngassa aifutia aibu Stars

Winga mshambuliaji Mrisho Ngassa aliitoa aibu timu ya taifa 'Taifa Stars' baada ya kuifungia bao tamu katika dakika ya 18 dhidi ya Zanzibar Herous katika mechi ya michuano ya kombe la Chalenji inayoendelea mjini Nairobi, Kenya.

Messi ashinda tuzo za Ballon D'or

PARIS, Ufaransa
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Barcelona na Argentina, Lionel Messi, ameshinda tuzo ya mwanasoka bora 2009 (Ballon D'Or), inayotolewana kila mwaka na jarida la michezo la Ufaransa, taarifa ya jarida hilo kupitia tovuti yake liliandika jana mjini Paris, nchini Ufaransa.
Messi, 22, anakuwa mchezaji wa kwanza wa Argentina kushindi tuzo hiyo, ambapo msimu iliopita alimaliza akiwa wa pili nyuma ya aliyekuwa mshindi Cristiano Ronaldo.
Taarifa za jarida hilo, zimesema kuwa Messi ameibuka mshindi wa tuzo hiyo baada ya kumshinda Cristiano Ronaldo aliyeshika nafasi ya pili kwa pointi 473 dhidi ya 233.
Messi, aliiwezesha mabingwa wa Hispania--Barcelona kutwaa taji la vilabu barani Ulaya msimu uliomalizika.
Mbali na kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa, pia aliweka rekodi nzuri ya kufunga mabao kwenye michuano hiyo baada ya kufanga mara tisa.
Moja ya bao hilo ni lile la mechi ya fainali dhidi ya Manchester United mjini Rome, Italia. Aliyeshika nafasi ya tatu na nne, ni wachezaji wenzake kwenye kikosi cha Barcelona, viungo Xavi (pointi 170) na Iniesta (pointi 149).
Mshambuliaji Samuel Eto'o, aliyeondoka Barcelona na kwenda kujiunga na Inter Milan msimu huu, alishika nafasi ya tano.
Mchezaji aliyeshika nafasi ya juu kwenye kinyang'anyoro hichi kutoka England ni Wayne Rooney aliyekuwa wa tisa.

Madega aifagilia Yanga

Na Daniel Mkate
HUKU ikiwa imefanya usajili wa wachezaji wawili tu katika dirisha dogo, mwenyekiti anayemaliza muda wake katika klabu ya Yanga , Iman Madega, amesema atahakikisha anapoondoka madarakani anaiacha klabu hiyo kwenye mstari mzuri.
Awali Yanga ilipanga kufanya uchaguzi wake mkuu Januari 3 mwakani, lakini kutokana na Shirikisho la Soka nchini kusitisha zoezi hilo kwa klabu hadi Jan.15, huenda sasa ukafanya katikati ya mwezi huo.
Madega alisema baada ya timu yake kuwasajili wachezaji wawili wa kimataifa kutoka Kenya na Ghana, anaamini itafanya vyema katika mzunguko wa pili wa ligi kuu huku ikiwa inashika nafasi ya tatu katika msimamo mzima wa ligi hiyo.
"Tumefanya usajili mzuri ingawa ni wa wachezaji wawili tu, kipa Yaw Berko kutoka Liberty Professionals FC ya Ghana na John Njoroge kutoka Kenya...tumejipanga vyema zaidi mzunguko wa pili," alisema Madega.
Madega alisema pamoja na kuwa hatowania tena uongozi Yanga, lakini atahakikisha anaiacha klabu hiyo katika hali nzuri kutokana na uongozi uliojengeka wa viongozi wenzake.
"Viongozi watakaochukua klabu watakuta timu ipo katika hali nzuri, itafanya mazuri katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo inayotarajiwa kuanza katika ya Januari mwakani," alisema.
Katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Yanga imekuwa ikienda mwendo wa kuasuasua tofauti na mahasimu wao Simba wanaoongoza ligi kwa pointi 33 baada ya kushinda mechi zote 11 walizocheza huku Yanga wakiwa na pointi 21 tu.

Chokolaa atimuliwa Twanga Pepeta

Na Abdul Mitumba
UONGOZI wa African Stars Entertainment Tanzania 'ASET', umemtimua kazi mwimbaji wake, Khalidi Chokolaa aliyekuwa katika bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Mkurugenzi mtendaji wa ASET, Asha Baraka amesema wameamua kumtimua Chokolaa baada ya kubaini kutaka kuigawa bendi hiyo baada ya kuanzisha bendi nyingine kivyake.
"Tumebaini njama alizokuwa akizifanya kwa muda mrefu, awali tulidhani lengo lake la kuanzisha kundi akiwa ndani ya Twanga lililenga kujiongezea kipato, lakini baadaye tukabaini lengo ni kutaka kuisambatarisha bendi yetu," amesema.
Hata hivyo, Asha amesema hatua zilizochukuliwa na ASET dhidi ya Chokolaa ni ya muda na kwamba endapo ataachana na kundi lake, wapo tayari kumrejesha kundini kwa sababu ASET bado inamhitaji.
Uamuzi wa ASET kumtimua Chokolaa umefuatia akiwa na wenzake watatu wa Twanga kuiasi bendi na kuanzisha kundi jipya la Mapacha Wanne wakimshirikisha msanii mmoja wa bendi ya FM Academia.
Awali meneja wa ASET, Abuu Semhando alisema mbali na Chokolaa waimbaji wengine ni Kalala Junior na Charlz Baba wakati yule wa FM Academia akiwa ni Jose Mara.
"Huu ni sawa na uasi, kama wataendelea kung'ang'ania kundi lao hilo ni bora waachane na Twanga ili nafasi zao zichukuliwe na wanamuziki wengine haraka kadri itakavyowezekana," amesema Semhando.
Hata hivyo, hadi jana ni Chokolaa pekee ndiye hakuwepo Twanga huku wengine wote wakishiriki maonyesho yote likiwemo bonanza la kila Jumapili pale Leaders Club, Kinondoni.