Thursday, August 20, 2009

IOC, TOC kuwafunda waandishi wa michezo


Na Jacqueline Massano
KAMATI ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kwa kushirikiana na Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) zimeandaa semina ya kimataifa ya siku mbili kwa waandishi habari za michezo wanawake itakaofanyika mjini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi amesema semina hiyo inatarajia kuanza kesho na kumalizika siku inayofuata.
Bayi amesema mkutano huo una lengo la kuwaelemisha waandishi hao juu ya thamani ya Olympiki na vile vile kuwajengea uwezo ili waweze kufanya kazi zao kwa umakini zaidi.
Aidha, mkutano huo pia utawawezesha kutambua umuhimu wao wakiwa kama waandishi wa habari wanawake na wajibu wao katika kukuza michezo na wanamichezo wanawake katika nchi zao.
Amesema semina hiyo inatarajia kuhudhuriwa na waandishi wa habari 28 wanaoandika michezo kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
"Huu utakuwa ni uwanja kwa wanahabari kuweza kujadili na kubadilishana mawazo ya jinsi ya kukuza mahusiano kati yao na wanamichezo na kuboresha utendaji wa kazi zao," alisema.
Katibu huyo amesema pia waandishi hao watafahamishwa juu ya utendaji wa kazi wa Kamati ya Olympiki ya Kimataifa pamoja na idara zake ili kuweza kufikia malengo yao ya kuwawezesha wanawake.
Amezitaja mada ambazo zitajadiliwa kwenye semina hiyo ni pamoja na changamoto zinazowakabili wandishi wa habari wanawake na jinsi ya kukabiliana nazo, Michezo ya Wanawake nchini na jinsi ya kuboresha uandishi wao na kuepukana na vikwazo.
Ameongeza kuwa waandishi watajifunza mambo mbalimbali na pia watapata uzoefu kutoka kwa washiriki kutoka Uganda na Kenya.

Mrwanda kitanzini Simba

Na Jacqueline Massano, Jijini

BAADA ya mshambuliaji wa Simba, Danny Mrwanda kumjibu kwa kejeli bosi wake, Omary Gumbo, uongozi wa klabu hiyo unatarajia kukutana mara baada ya kumaliza mechi zao za Majimaji na Prisons ili kumjadili mchezaji huyo.
Akizungumza na blogu hii mapema leo, Katibu Mkuu wa Simba, Mwina Kaduguda amesema kitendo kilichofanywa na Mrwanda si cha kiungwana na ni cha udhalilishaji.
"Hawezi kumjibu bosi wake kama mtoto mwenzake, yeye alikuwa amekosea na alitakiwa kuwa mstaarabu na mwenye hekima," alisema Kaduguda.
Alisema kamati hiyo itakapokutana italijadili suala hilo na kabla ya kumchukulia hatua, itamwita ili aweze kutoa maelezo.
Kaduguda alisema mshambuliaji huyo alikuwa amekosea na wakati alipokuwa akionywa na mkuu wa msafara ambaye alikuwa Gumbo alimjibu kwa jeuri.
"Mrwanda alimjibu vibaya Gumbo, alimwambia usinibabaishe na amesahau kuwa Gumbo ni mmoja wa viongozi wa klabu ya Simba," alisema.
Hata hivyo, Kaduguda alikanusha kama Gumbo alizichapa na Mrwanda kama baadhi ya magazeti yalivyoandika.
Amesema wakati timu hiyo ilipokuwa ikisafiri wachezaji wote walivaa nguo zenye nembo ya Kilimanjaro isipokuwa Mrwanda ambaye aliambiwa na meneja wa timu hiyo, Innocent Njovu lakini alikaidi.
"Bahati nzuri wakati Njovu anazungumzia suala hilo, Gumbo alikuwa karibu ndiyo ikabidi aingilie kati na kumwambia Mrwanda kuwa anachofanya si sahihi lakini mshambuliaji huyo alimjibu vibaya Gumbo.
"Kwa kweli Gumbo hakupigana na Mrwanda, alipoona amejibiwa vibaya ilibidi anyamaze kimya," aliongeza.
Kaduguda amesema wakati wanaingia mkataba na TBL, moja ya kipengele chao cha makubaliano ni lazima wachezaji wote wavae nguo zenye nembo ya kilimanjaro wakiwa safarini na kambini na wala si vinginevyo.
"Huo ndiyo mkataba tulioingia na TBL, hatuwezi kupoteza mamilioni ya fedha kwa upuuzi unaofanywa na mchezaji mmoja wa kukataa kuvaa nguo zao," alisema.

Wednesday, August 19, 2009

Tuesday, August 18, 2009

Arsernal kuifuata Celtic leo

GLASGOW, Scotland
ARSENAL leo itakuwa na kibarua cha kuwanyamazisha wapenzi wa soka wa hapa wakati itakapokabiliana na Celtic katika mchezo wa kwanza wa kusaka nafasi ya kucheza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Celtic imekuwa tishio inapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Celtic Park na ina rekodi nzuri, ambapo iliilazimisha sare ya 1-1 Manchester United msimu uliopita.
"Siku zote hali ni tete Scotland," alisema kocha wa Arsenal, Arsene Wenger akizungumzia mchezo wa leo usiku."
Endapo tutacheza vizuri tunaweza kuifanya hali kuwa shwari..."
Celtic iliweka rekodi ya mahudhurio ya watazamaji kwa klabu za Ulaya wakati watazamaji 133,961 walipojitokeza kushuhudia kikosi cha Jock Stein kikiichapa Leeds katika nusu fainali ya mashindano ya Ulaya mwaka 1970 kwenye uwanja wa Hampden Park, lakini Wenger anaamini kuwa kikosi chake kitaendana na hali yoyote.
"Tumecheza Ulaya katika hali zenye ushindani mkubwa na kutokana na uzoefu wetu tunajua tufanye nini ili tuendane na hali, " aliongeza kocha huyo.

Micho amjia juu Ivo


Na Jacqueline Massano, Jijini
WAKATI aliyekuwa kipa wa St. George ya Ethiopia, Ivo Mapunda akilalamika kutemwa dakika za majeruhi na klabu yake hiyo, kocha wa timu hiyo, Milutin Sredejovic 'Micho' amesema kukosa nidhamu na kushuka kwa kiwango kwa mchezaji huyo ndiko kumesababisha atemwe.
"Ivo anatakiwa aseme ukweli na wala si kusema ameachwa dakika za majeruhi, hivi kwa nini wachezaji wa bongo huwa wakishindwa wanasingizia mambo mengi," amehoji Micho.
Ameendelea kusema, "Ivo nilikuwa nampenda sana nilijitahidi kumsaidia kila kitu, pia nilitamani aendelee mbele zaidi lakini kutokana na mambo yake sikuwa na jinsi ya kumbeba."
Micho ameiambia blogu hii mapema jana kwa njia ya mtandao kuwa mchezaji huyo hatakiwi kulalamika kwa sababu alinunuliwa na klabu hiyo na kuchukuliwa kama mfalme siku zote alizokuwa akiitumia timu hiyo.
Kocha huyo amesema katika mechi za kwanza za ligi, kipa huyo alifanya vizuri sana na kuwavutia mashabiki wa Ethiopia kutokana na udakaji wake lakini baada ya siku kwenda akaonekana anabadilika.
"Ivo alipendwa na mashabiki wa St. George na kumuona kama mfalme, lakini mwishoni mwa ligi ndipo alipoanza kuvurunda, sioni sababu ya yeye kulalamika wakati ameichezea bahati mwenyewe," alisema.
Hata hivyo, Micho alisema baada ya kugundua kuwa mashabiki wa klabu hiyo hawamtaki tena kipa huyo ndipo alipoamua kumpeleka Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye klabu inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.
"Ilifika kipindi nikimpanga Ivo uwanjani kwa ajili ya kudaka mashabiki wanaanza kumzomea wakidai kuwa hawamtaki, ni kutokana na kuanza kufungwa magoli ya kizembe.
"Lakini sikukata tamaa niliamua kumtafutia timu nje, na hii yote ni kwa ajili ya kupenda maendeleo yake lakini hata huko nako alishindwa majaribio," alisema kocha huyo ambaye amewahi kuifundisha Yanga kwa misimu miwili.

Sunday, August 16, 2009

Yanga yaamia Jangwani

Na Jacqueline Massano, Jijini

BAADA ya kuchapwa bao 2-1 na Mtibwa Sugar katika mechi ya kuwania kombe la Hisani, Wachezaji wa Yanga wameingia kambini kwao Jangwani rasmi jana usiku.
Awali Yanga ilikuwa ikifanya mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani wakati ikiendelea kusubiri vitu kadhaa viendelee kukamilishwa ndani Jengo lao lililopo mtaa wa Twiga na Jangwani.
Habari zilizopatikana mapema leo kutoka kwa mmoja wa wachezaji wa klabu hiyo, ni kwamba wameanza kuingia kambini kuanzia jana usiku mara walipomaliza kupokea kipigo kutoka kwa Mtibwa Sugar.
Alasiri ilipomuuliza mchezaji huyo kuhusiana na mazingira na kambi yao, alisema: "Kwa kweli itakuwa ngumu kuelezea sasa hivi kwa sababu ndiyo kwanza jana tumeingia tena usiku, labda kadri tutakapokuwa hapa ndiyo tutaona mapungufu.
"Ila kinachoniboa mimi ni mazingira ambayo tupo ingawa jengo letu ni zuri sana na kila chumba kina AC, kwa kweli viongozi wetu wamejiatahidi sana. Lakini mambo mengine bado sijayajua vizuri kama masuala ya msosi na mambo mengine," aliongeza mchezaji huyo
Mchezaji huyo amesema itawawia vigumu sana kupazoea mahali hapo kwa kuwa pamezungukwa na watu wengi sana na kuna kelele sana za mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wanaopenda kukaa hapo.
"Sasa hapa tutapambana na kelele za ubishi wa mashibiki na wanachama wanaopenda kukaa hapa. Kinachotakiwa ni viongozi kutuepusha na hilo kwa kuwa sisi kama wachezaji tunatakiwa kukaa sehemu isiyo na kelele wa fujo," alisema
Yanga inajiandaa na mechi yake ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya African Lyon inayotarajia kufanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Friday, August 14, 2009