Monday, November 30, 2009

KIPA MPYA YANGA KUJARIBIWA LEO

WAKATI ikiendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kipa mpya wa Yanga kutoka Ghana, Yaw Berka anatarajiwa kufanyiwa majaribio leo uwanjani hapo.
Berka ambaye aliwahi kuichezea timu ya tifa ya vijana ya Ghana, atafanyiwa majaribio akiwa chini ya kocha mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic.
Yanga kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kusajili wachezaji katika dirisha dogo la usajili ambalo linafikia tamati leo.

PICHA YA WIKI


UCHAGUZI SIMBA MWAKANI

WAKATI wanachama wa klabu ya Simba wakilicharukia Shirikisho la Soka nchini, TFF, kuwa limekwamisha kufanyika kwa uchaguzi mkuu, uongozi wa klabu hiyo umetangaza uchaguzi huo sasa utafanyika Januari 17, mwakani.
Kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo iliyokutana usiku wa kuamkia leo, umeamua kwa kauli moja kuwa uchaguzi huo utafanyika Januari mwakani na wala si Desemba mwaka huu kama ilivyokuwa ikitarajiwa na wengi.
Kwa mujibu wa taarifa toka kwa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ni kwamba kikao hicho kimeamua uchaguzi huo kufanyika tarehe hiyo ili kupisha zoezi la ugawaji wa kadi, kikao cha mapato na matumuzi na mkutano mkuu.

Sunday, November 29, 2009

Ibrahimovic aipa ushindi Barca

ZLATAN Ibrahimovic aliingia uwanjani akitokea katika benchi la wachezaji wa akiba na kuipatia Barcelona ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao wakubwa Real Madrid na kuirejesha timu hiyo kileleni mwa msimamo wa La Liga.
Mshambuliaji wa Sweden Zlatan Ibrahimovic alifunga bao pekee lililoitoa Barcelona kifua mbele baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Real Madrid nyumbani na kurejea kileleni mwa msimamo wa Primera Liga.\Mchezaji huyo alifunga bao hilo katika dakika ya 56 na Barca ilijikuta ikipata pigo baada ya mchezaji wake Sergio Busquets kutolewa nje kwa kadi nyekundu muda mfupi baada ya bao hilo, lililoiwezesha timu hiyo kuwa pointi mbili zaidi kileleni dhidi ya wapinzani wake hao wakubwa ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza mechi 12.

CHELSEA YAICHAMBUA ARSENAL

LONDON, England
Chelsea bado imeendelea kuongoza kwa pointi tano kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England na kupunguza makali ya baadhi ya timu zinazoifukuza katika kinyang'anyiro hicho baada ya kuibuka na ushindi wa bao 3-0 ugenini kwenye uwanja wa Emirates na kuiacha Arsenal ikiwa nyuma kwa pointi 11.

Friday, November 27, 2009

Yanga yaongoza kwa kesi TFF

Na Jacqueline Massano, Jijini
MSHAMBULIAJI wa kimataifa, Boniface Ambani amesema ataichongea klabu Yanga ya jijini Dar es Salaam iliyotangaza kumwaga mwanzoni mwa wiki hii, Shirikisho la Soka nchini TFF iwapo klabu hiyo itashindwa kumlipa madai yake kwa wakati.
Ambani raia wa Kenya ambaye amecheza Yanga misimu miwili, anaidai klabu hiyo kufuatia kuvunjwa kwa mkataba wake miezi sita kabla.
Akiongea na blog hii mapema leo, Ambani alisema anatarajia kuwasili nchini, Jumatatu kwa ajili ya kufatilia madai yake kabla ya kwenda Ethiopia alipoitwa na kocha wa zamani wa klabu hiyo, Milutin Sredejovic 'Micho'.
"Safari yangu ya kuja Dar ni pamoja na kufuatilia pesa zangu Yanga baada ya kuvunjwa kwa mkataba. Ni vyema Yanga wakaharakisha kunilipa madai yangu," alisema.
Iwapo Ambani atakwenda kuishitaki Yanga TFF, atakuwa mchezaji wa pili katika kipindi kifupi baada ya mchezaji mwingine aliyetemwa katikati ya msimu, beki Hamis Yusuf kwenda kuishitaki klabu hiyo kwa kile kinachodaiwa kuvunjwa kwa mkataba wake.
Msimu iliopita, Yanga ilikutana tena na mashitaka TFF baada ya mchezaji wake raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Aime Lukunku kuishitaka baada ya kutelekezwa kwa muda mrefu bila kulipwa madai yake.
Mbali na wachezaji hao, pia kocha aliyemaliza mkataba wake, Dusan Kondic aliwahi kuishitaki klabu hiyo TFF baada ya kuchelewa kumlipa mshahara wake wa miezi minne zaidi ya shilingi milioni 30.
Kocha mwingine anayeidai klabu hiyo na ambaye anaweza kupiga hodi TFF kushinikiza kulipwa madai yake ni aliyekuwa msaidizi wa Kondic, Spaso Solokovisk ambaye anaidai klabu zaidi ya shilingi miluioni 21.

Uchaguzi wawagawa mabosi Simba

Na Badru Kimwaga
WAKATI Mhazini Mkuu wa Simba akitangaza dhamira yake ya kujitosa kwenye uchaguzi mkuu wa klabu hiyo, kuna habari kwamba uchaguzi huo huenda usifanyike mwezi ujao kama ilivyotarajiwa na wengi.
Habari za kuaminika zinasema kuwa pamoja na kikao cha Kamati ya Utendaji kukutana Jumapili wiki hii, huenda ikaamuliwa uchaguzi huo kufanyika Januari mwakani.
Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa kumekuwa na mvutano mkubwa juu ya uchaguzi huo ufanyike lini, kundi moja likitaka ufanyike mwezi ujao na jingine kutaka lifanyike mwakani.
"Huwezi kuamini, lakini ukweli ni kuwa viongozi Simba wamegawanyika juu ya lini uchaguzi huo ufanyike, wapo wanaotaka uitishwe mapema na wengine wanapinga wakitoa visingizio muhimu kwa sasa ni ligi kuu," chanzo kilisema.
Habari hizo zinasema kuwa hata kikao cha Jumapili kinaweza kisimalizike vema kama vikao vingine viwili vya klabu hiyo kipindi cha kusaka viongozi wa kuajiriwa kutokana na mgawanyiko huo wa viongozi kuhusu uchaguzi huo.
Hata hivyo Mhazini Mkuu wa Simba, Almas Chano alisema uchaguzi mkuu wao utafahamika rasmi Jumapili baada ya kikao chao cha kamati ya utendaji na kwamba yeye tayari amejipanga kuwania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
"Lini uchaguzi wetu ufanyike, hilo litafahamika baada ya kikao cha Jumapili na sioni watu waanze kuhoji sasa kabla ya kikao hicho," alisema Chano.
Aliongeza kuwa tarehe yoyote utakaofanyika uchaguzi huo, yeye yu tayari kuwania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji na kwamba muda si mrefu ataweka bayana safu yake watakaojipanga kuingia madarakani kuiongoza Simba.
Viongozi wa sasa Simba waliingia madarakani Desemba 3, 2006, nao ni Hassani Dalali, Omar Gumbo, Mwina Kaduguda, Mohammed Mjenga, Idd Senkondo, Almas Chano na Said 'Seydou' Rubeya.