Tuesday, December 29, 2009

Simba kuteta mwishoni mwa wiki

#Ni kujadili mabao mawili ya Yanga
Na Badru Kimwaga
VIONGOZI wa klabu ya Simba wanatarajia kuwekana 'kitimoto' na kujadili kipigo cha Yanga katika kikao chao cha Kamati ya Utendaji kitakachofanyika mwishoni mwa wiki.
Viongozi na wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji wameshajulishwa kikao hicho muhimu, ambacho pia kitatoa nafasi ya kujadili mambo mengine muhimu ya maendeleo ya klabu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu ya Simba, ni kwamba kikao hicho ambacho ni muendelezo ya kikao kilichofanyika awali Novemba 30 kitafanyika kwenye hoteli ya Regency.
Kubwa litakaloongelewa kwenye kikao hicho ni kipigo toka Yanga, uchaguzi mkuu na hoja ya mapato na matumizi ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu sasa.
Kamati hiyo inaundwa na Ayoub Semvua, Omar Gumbo, Mohammed Mjenga na Hassan Othman 'Hassanoo', iliyopewa kazi ya kukutana na TFF kwa lengo la kufanyia marekebisho ya katiba yao kabla ya kuitishwa kwa uchaguzi mkuu.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji, Said 'Seydou' Rubeya, alithibitisha kupata barua ya mualiko wa kikao hicho na kusisitiza anaenda kwenye kikao hicho kutaka majibu ya ombi lake juu ya mapato na matumizi ya klabu yao.

Kipigo kingine chaisubiri Simba

*Yanga yatamba
Na Jacqueline Massano

KATIKA mwendelezo wa kunogewa na furaha ya ushindi dhidi ya watani wao wa jadi Simba, mabingwa wa soka nchini, Yanga imesema ingetamani kupata nafasi nyingine ya 'kuionea' Simba wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajia kuanza baadaye mwezi ujao Visiwani, Zanzibar.
Yanga ilimaliza uchovu wa kutoondoka na furaha kila inapokutana na Simba baada ya kuwanyuka Wekundu hao wa Msimbazi mabao 2-1 katika mechi ya dakika 120--nusu fainali ya michuano ya Kombe la Tusker iliyomalizika kwa Yanga kutwaa ubingwa.
Simba, mabingwa wa soka nchini, Yanga na Mtibwa zitashiriki kutoka Bara, wakati wenyeji timu za Kisiwani Zenji ni pamoja na Malindi, Miembeni, Jamhuri, Zanzibar Ocean View na Mafunzo.
Afisa Uhusiano wa Yanga, Louis Sendeu amesema kuwa kikosi chako kwa sasa kiko imara kukabiliana na timu yoyote, na italeta furaha kama watakutana tena na Simba kwenye michuano hiyo.
Katika michuano ya Tusker, Simba ilimaliza kwa kushika nafasi ya tatu, kufuatia ushindi wa jasho jingi lililokauka baada ya dakika 120 na kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tusker ya Kenya katika mechi ya nusu fainali, huku Tusker ikikosa nafasi hiyo kiduchu baada ya kuwa mbele bao 1-0 mpaka dakika za majeruhi kabla ya Simba kusawazisha na kupelekea nyongeza ya dakika.
Alisema kuwa ushindi mafanikio mazuri waliyopatra kwenye michuano ya Tusker imefungua njia zaidi ya ushindani hasa katika michuano ya Ligi Kuu.
"Kama tutapangwa kundi moja na Simba, au ikatokea kukutana katika hatua yoyote, basi hii ndiyo furaha yetu. Kwa sasa tunaweza kuifunga Simba tunavyotaka. Ilikuwa makosa kudhani kwamba Simba haifungiki," alisema.
Wakati Yanga wakikosa mapumziko baada ya michuano ya Tusker, wapinzani wao Simba wako mapumzikoni mpaka Januari 2. Kwa mujibu wa Sendeu, timu yao inaanza mazoezi leo kwenye uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika, IST.
Hata hivyo taarifa za hofu kwamba Simba huenda isishiriki michuano hiyo, zimezimwa leo baada ya kuthibitisha ushiriki wao kupitia mtoa habari Clifford Ndimbo.
Ndimbo amesema kuwa, klabu yao itashiriki michuano hiyo kama ilivyopangwa, na kwamba wanatarajia kuanza mazoezi muda mfupi baada ya kurejea kocha Patrick Phiri aliyerudi zambia kwa mapumziko mafupi.

Monday, December 28, 2009

SOFAPAKA yawanyatia wawili wa Mtibwa


KLABU ya soka ya SOFAPAKA kutoka Kenya, imewazimia wachezaji wawili wa timu ya Mtibwa Sugar.
Fununu zilizoifikia blog hii ni kwamba uongozi wa klabu hiyo umeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na mabeki hao wa Mtibwa.
Wachezaji hao ambao wanaweza kulamba bingo hilo iwapo yatafikiwa makubaliano kati ya uongozi wa Mtibwa na Sofapaka ni Idrisa Rajabu na Abdulhim Amour.
Habari zilizopatikana ni kwamba endapo uongozi huo utafanikiwa kuwasajili wachezaji hao itawatumia kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

Yanga yaitisha Simba

UONGOZI wa klabu ya Simba umekiri mahasimu wao Yanga walistahili kutwaa ubingwa wa michuano ya kombe la Tusker kutokana na kujiandaa vizuri kuliko wao.
Aidha, uongozi huo umewataka wanachama wao kuacha kumsaka mchawi kwa matokeo yaliyowatokea katika michuano hiyo iliyomalizika jana, na badala yake kutakiwa kushikamana kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu nchini.
Katibu Msaidizi wa klabu hiyo, Mohammed Mjenga, alisema watani wao walionekana kubadilika kisoka kwa kucheza mpira wa pasi na kwa kiwango hicho walistahili kuwa mabingwa wa Tusker.
Mjenga alisema ni dhahiri Yanga walijiandaa vyema kwa michuano hiyo tofauti na Simba na ndio maana waliweza kuibuka washindi katika mechi yao na hawana la kusingizia zaidi ya kuridhika na matokeo.
Alisema hata hivyo pamoja na kuwapa heko watani zao, bado binafsi anawatupia lawama waamuzi kwa kuonyesha udhaifu katika michuano hiyo."Tatizo la waamuzi ni sugu na hatujui litaisha lini, ni kama hawajui wajibu wao wawapo uwanjani," alisema Mjenga.
Pia aliwataka wanachama wa Simba kuacha kumsaka mchawi kutokana na matokeo ya mechi yao na Yanga na badala yake kushikamana pamoja kwa ajili ya kujiandaa na duru la pili la ligi kuu pamoja na Kombe la Shirikisho.
Mjenga alisema, lawama kwa sasa wakati muafaka, ila umoja na mshikamano pamoja na kumsapoti kocha na wachezaji kwa michuano iliyopo mbele yao ndio kitu cha muhimu zaidi.

Simba wamgeuzia kibao Phiri

BAADA ya kuchapwa mabao 2-1na mahasimu wao Yanga katika mechi ya nusu fainali ya kombe la Tusker, Simba sasa wameamua kumgeuzia kibao kocha wao mkuu, Mzambia Patrick Phiri.
Baadhi ya mashabiki, wapenzi na manazi wa timu hiyo wamesema kocha huyo ndiyo sababu kubwa ya kufungwa na Yanga, na kisha wachezaji kucheza chini ya kiwango katika michuano hiyo iliyomalizika kwa klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani kutwaa taji.
Wakizungumza baada ya pambano lao la Alhamisi kumalizika, wapenzi hao wa Simba wakasema kitendo cha Phiri kuondoka na kwenda mapumzikoni nyumbani kwao Zambia na kuwapa mapumziko ya muda mrefu wachezaji, ndiyo sababu iliyosababisha wachezaji hao kuporomoka viwango.
"Kama kocha angekuwepo kambini na timu huko Zanzibar na kutoa mazoezi kama yale anayowapa katika Ligi Kuu Bara, basi wana imani wasingefungwa na kunyanyaswa na Yanga uwanjani na pia kuchukua ubingwa," alisema Muhidin Parojo mnazi wa Simba.
Simba timu inayochukuliwa kama ni kioo cha michuano hiyo, imecheza katika kiwango duni na kuwashangaza mashabiki waliozoea kuiona ikicheza Ligi Kuu mechi 11 bila kufungwa wala kutoka sare."
Katika mechi ua kusaka mshindi wa tatu, Simba waliishinda Tusker kwa mabao 2-1 na kushika nafasi ya tatu.Mashabiki wengi wamemtaka kocha Phiri kutowapa mapumziko tena wachezaji wake na badala yake awafanyishe mazoezi makali mara baada ya mwaka mpya kuanza.

Hali ilivyokuwa fainali Kombe la Tusker

Athuman Idd 'Chuji' akimzuia mchezaji wa Sofapaka wakati wa fainali za Kombe la Tusker zilizofanyika jana. Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kuchukua kombe hilo.
Kipa wa timu ya Sofapaka, Wilson Obungu akiwapigia kelele wachezaji wenzake wakati wa mechi ya fainali hizo.


Mshambuliaji wa pembeni wa Yanga, Mrisho Ngassa akiwatoka wachezaji wa Sofapaka.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga, wakiwa wamembeba kocha wao, Kostadin Papic mara baada ya kuchukua ubingwa jana.
Mshambuliaji wa Yanga, Jerry Tegete akionyesha kikombe juu baada ya kuzawadia alipoibuka kuwa mfungaji bora kwenye michuano hiyo. Pia mchezaji huyo alipewa dola 2,000.

Katibu mkuu wa Simba, Mwina Kaduguda akipokea mfano hundi ya sh. milioni 10 baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa tatu wa michuano hiyo.

Baadhi ya wachezaji wa Yanga, wakiwa na mwenyekiti wao Iman Madega wakishangilia baada ya kupewa kombe la Tusker.

Nahodha wa Yanga, Abdi Kassim 'Babi' na kocha mkuu wa timu hiyo, Papic akionyesha juu mfano wa hundi ya sh. milioni 40 baada ya kuibuka mabingwa wa michuano hiyo.

Wednesday, December 23, 2009

Simba yatamba kuitafuna Yanga

BAADA ya kuanza vizuri kwenye michuano ya Tusker, Simbari, imesema imejiwekea malengo ya kushinda mchezo wa kesho dhidi ya Yanga wa nusu fainali ya Kombe la Tusker ili kudumisha rekodi yake iliyoianza katika Ligi Kuu Bara.
Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na uhakika na imesema dhamira ya kushinda mchezo wa kesho inatokana na ubora wa wachezaji wake akiwemo mkongwe Mike Barasa katika safu ya ushambuliaji.
Kocha msaidizi wa Simba, Amri Said 'Jaap Stam' ameiambia Alasiri jana kuwa vijana wake wapo katika hali nzuri kwa silimia 99 na kwamba kuifunga Yanga pekee haitoshi bali inataka kuvikwa taji.
"Pamoja na kwamba Simba inaongoza kwa kulitwaa kombe hilo, lakini kitendo cha kukutana na Yanga katika hatua yoyote ni changamoto ya kipekee inayoisukuma Simba kushinda," alisema.
Alisema kuifunga Yanga katika mchezo wa leo kuna maana kubwa mbili, kwanza kutaiwezesha Simba kutinga fainali na pili kutaifanya imalize mwaka vizuri.
Amri alisema katika soka la Tanzania na nchi nyingine zenye mvuto wa mchezo huo, timu pinzani zinapokutana ni lazima ratiba za wapenzi zinavurugika kila mmoja akitaka kuiona.
"Sisi tunatambua hilo na ndiyo maana tumejiwekea malengo ya kushinda na baadaye kulitwaa kombe lenyewe," alisema.