
MWIMBAJI maarufu wa nyimbo za Injili, Rose Muhando, amepata ajali mbaya usiku wa kuamkia leo baada ya gari lake aina ya Toyota Prado kupinduka mara tatu na kuharibika kiasi cha kutotamanika.
Habari zilizopatika mapema leo asubuhi, zinasema kuwa Rose amepata ajali hiyo Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Alipata ajali hiyo wakati yeye na wanakwaya wenzie wakielekea mkoani humo baada ya kutoka kwenye mkutano mmoja wa injili uliokuwa ukifanyika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoelezwa na na mmoja wa ndugu wa karibu wa Rose ni kwamba ajali hiyo mbaya imetokea jana usiku, mishale ya saa 5:30.
Hata hivyo, taarifa ya ndugu huyo wa Rose imeeleza kuwa mwimbaji huyo na wenzie walinusurika baada ya wote kutoka salama, ingawa gari lilikuwa limepondeka vibaya.
Ameeleza zaidi kuwa Rose alipata majeraha madogo mguuni na mkononi na kwamba baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa hakuumia kwa ndani, aliruhusiwa kurudi nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, dereva wa Rose na wanakwaya wengine saba waliokuwa kwenye gari hilo hawakupata majeraha ya kutisha na hivyo wote waliruhusiwa toka katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa dereva wa gari hilo aliona kitu kikubwa mbele yake na wakati alipojaribu kukikwepa, ndipo alipojikuta akiingia porini na gari hilo kupinduka mara tatu.
Hata hivyo, mwandishi alipojaribu kumsaka kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen ili azungumzie tukio hilo, hakuweza kumpata.
No comments:
Post a Comment