MIAMI, MarekaniKITENDO cha David Beckham kuichezea kwa mkopo AC Milan kina maana kuwa atakuwa mbali na familia yake kwa miezi sita na kiungo huyo wa England amesema kukaa kwake mbali 'kunamuua' yeye. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 atakuwepo Italia kuanzia Januari hadi Juni mwakani kabla ya kurejea Los Angeles Galaxy baada ya fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.
Katika mahojiano na radio moja, Beckham alisema alipoteza pesa katika kipindi alichoichezea timu hiyo kwa mkopo mapema mwaka huu lakini kuwa mbali na watoto wake ni kitu kilichokuwa kigumu sana kwake.
"Kitu kikubwa sana kwangu kwenda na kuishi mbali na familia yangu kwa miezi sita.
Na kila wiki nane walikuwa wanakuja kukaa wiki nzima na kuniangalia, "alisema.
"Mtu yeyote anayenijua ninavyojisikia kuhusu watoto wangu, kuhusu mke wangu na familia yangu kwa ujumla ninachukia kukaa mbali na familia yangu.
Kuwa mbali na familia yangu na watoto wangu ni kitu ambacho kinaniua mimi.
"Nakwenda na kuishi Italia na siwezi kwenda na familia yangu kwa sababu vijana wangu wanasoma na hatuwezi kuwasumbua watoto, "aliongeza Beckham.
Alisema nia yake ya kuichezea England katika fainali zijazo za Kombe la Dunia ndizo zilizomsukuma kuondoka Marekani na kwenda kuichezea klabu ya Serie A, na haimuhakikishii kuwemo katika kikosi cha mwisho cha Fabio Capello.
"Hiyo ndio sababu pekee iliyonifanya kukubali kuwa mbali na familia yangu kwa takribani miezi sita, "alisema.
"Kuwa katika kikosi cha Kombe la Dunia sio lazima, hata kama naenda kucheza Milan hakunihakikishii nafasi hiyo, lakini natakiwa kufanya kila linalowezekana kupata nafasi hiyo.


No comments:
Post a Comment