Thursday, November 5, 2009

Simba 'yawaingiza mjini' mashabiki

Na Badru Kimwaga, Jijini
TIMU ya soka ya Simba jana iliwaingiza 'mjini' mashabiki walioenda kwenye uwanja wa Kinesi kushuhudia mazoezi yao baada ya kushindwa kufanyika na badala yake kuanza rasmi leo asubuhi na kuendelea tena jioni ya leo.
Uongozi wa Simba ulitangaza mazoezi yangeanza jana jioni, lakini hayakufanyika kwa kile kilichoelezwa ni mabadiliko ya 'programu' za kocha wao Mzambia Patric Phiri, ambaye alikuwa uwanja wa Uhuru kuzishuhudia Villa Squad na TMK Utd zilizokuwa zikicheza mechi yao ya ligi daraja la kwanza.
Baadhi ya wapenzi na mashabiki wa timu hiyo walifurika kwenye uwanja huo wa Kinesi, bila kuwaona wachezaji wao na kulalamika, lakini Mhazini Mkuu wa klabu hiyo, Almasi Chano alisema mazoezi hayo yalianza leo na yataendelea tena jioni.
"Tunawaomba radhi mashabiki na wanachama wetu kwa usumbufu waliopata, ila tumeanza mazoezi leo asubuhi na yataendelea jioni na kesho kabla ya Jumamosi kucheza mechi ya kirafiki na Azam kwenye uwanja wa Uhuru," alisema Chano.
Chano alisema kilichofanya washindwe kuanza jana kama walivyokuwa wamepanga ni mabadiliko ya ratiba ya mwalimu.
Mhazini huyo alisema mwalimu ametaka kucheza na Azam kwa imani itawasaidia kujiweka fiti kabla ya kuivaa Mtibwa katika mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania duru la kwanza itakayofanyika jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment