Friday, November 6, 2009

Siwezi kucheza Simba-Barasa

Na Jacqueline Massano

MSHAMBULIAJI wa mabingwa wa soka nchini, Yanga, Mike Barasa amekanusha kujipeleka mwenyewe kwa watani zao wa Jadi, Simba kutaka kusajiliwa nao kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayotarajia kuanza tena mwakani.
Kauli hiyo ya Barasa imekuja baada ya viongozi wa Simba kukaririwa wakidai kuwa wanampango wa kumsajili mshambuliaji huyo kwa kuwa alijipeleka mwenyewe akitaka kusajiliwa na klabu hiyo.
Akizungumza na Alasiri mapema leo, Barasa alisema hana mpango wa kuichezea klabu hiyo kwa sababu bado ana hasira nayo.
"Mimi sijajipeleka Simba, yaani kwenda huko kunatafsiriwa kwamba kiwango changu kimeshuka, haiwezekani mtu ambaye anajiamini ajipeleke sehemu mwenyewe bila ya kuitwa, "alisema nakuongeza:"Kwanza siwezi kuichezea Simba, bado nina hasira nayo, labda hadi hapo nitakapoifunga, ndiyo naweza kuichezea. Kama walikuwa na mahesabu ya kunichukua naona wamekosea."
Barasa amesema leo anatarajia kuonana na viongozi wa Yanga ili kuona kama kuna uwezekano wa kuongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo na kwamba ikishindikana atarudi kwao Kenya.
"Kuna vitu ambavyo nataka kuzungumza na mabosi wangu, na kama tukikubaliana nitaongeza mkataba na ikishindikana nitarudi zangu Kenya na wala siwezi kujiunga na Simba," alisema
Kwa sasa timu zinazoshiriki Ligi Kuu zipo kwenye mchakato wa kupunguza na kuongeza wachezaji kwenye usajili wa dirisha dogo linalotarajia kufikia tamati Novemba 20 mwaka huu.
Hatahivyo, kocha wa Yanga, Kostadin Papic katika program yake alidai kupunguza wachezaji watano wa kigeni ili aweze kuongeza wengine kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake.

No comments:

Post a Comment