Tuesday, November 3, 2009

Beckham kuamia Milan mwakani

Milan, Italia
David Beckham anatarajia kujiunga na AC Milan kwa mkopo wakati wa usajili wa dirisha dogo, Januari mwakani akitoka klabu ya Los Angeles Galaxy ya Marekani, taarifa ya klabu yake ilisema jana.
Kiungo huyo wa kimataifa wa England, 34, atabaki Italia kuanzia Januari mpaka Juni kabla ya kurejea tena kwenye timu hiyo ya Marekani kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Beckham, ambaye msimu uliopita aliichezea timu hiyo, anataka kupata nafasi ya kutosha kucheza ili amshawishi kocha wa England Fabio Capello kumuita kwenye kikosi cha timu ya taifa kilichofuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani zinazotarajia kuanza Juni 11.
"Nataka kupata nafasi ya kucheza ili niweze kuwemo kwenye kikosi cha England kitakachokwenda Afrika Kusini. Kucheza kwa mkopo hapa Milan, kunaweza kunisaidia," alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.
"Ukweli ni kwamba nilikuwa na wakati mzuri nilipocheza Milan, natarajia tena kuonana na wachezaji na wafanyanyazi wa Milan. Mimi ni mchezaji halali wa LA Galaxy nitaendelea kuwa nao na kucheza soka Amerika."
Nahodha huyo wa zamani wa England, mara nyingi amekuwa akiingia kama mchezaji kutoka benchi katika kikosi cha Capello.
"Tuna furaha kumuona tena David Beckham katika jezi ya rangi nyeusi baada ya kuwepo hapa kwa mafanikio msimu uliopita," alisema bosi wa Milan Adriano Galliani.
"Tuna hakika nafasi hii ya kucheza Ulaya itamuwezesha kupata nafasi ya kucheza Kombe la Dunia mwakani, kisha kurejea kuendelea kucheza soka Los Angeles Galaxy."

No comments:

Post a Comment