
KOCHA wa mabingwa wa soka nchini, Yanga ya Jijini Dar es Salaam, Kostadin Papic amesema kipigo cha bao 1-0 walichopata toka Simba mwishoni mwa wiki, kilichangiwa kwa kiasi kikubwa na ubinafsi wa wachezaji na kukosekana kwa ushirikiano dimbani.
Papic alikuwa wazi kusema hayo muda mfupi baada ya mechi kumalizika na kisha kukutana katika kikao kifupi na wachezaji wake makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Jangwani.
Mmoja wa kati ya wachezaji aliyekuwepo kwenye kikao hicho, ameitonya Alasiri mapema leo kuwa, kocha alikasirika kuona wachezaji wake wakicheza mechi hiyo kama vile hakukuwa na maelekezo ya pamoja waliyopewa kabla ya mechi.
"Hakufurahishwa kwa jinsi tulivyocheza," alisema mchezaji huyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini wakati akimnukuu kocha Papic.
Aliongeza kwa kusema: "Kama kuna jambo limemsikitisha kocha ni wachezaji kushindwa kutumia mwanya wa Simba kucheza pungufu kupata si goli la kusawazisha bali hata ushindi."
Pamoja na Simba kucheza pungufu karibu kipindi chote cha pili baada ya mashambuliaji wake Danny Mrwanda kuonyeshwa kadi ya pili ya njano, bado Yanga haikuonekana kucheza kwa ushirikiano na hivyo kupoteza nafasi hata ya kuambulia sare.
"Kocha alitegemea Simba baada ya kupungua mchezaji mmoja ndani, Yanga wangetumia nafasi hiyo kushambulia sana, lakini kinyume chake ni Simba ambao bado walionyesha kucheza kwa kuelewana na kupeleka mashambulizi," alisema zaidi akimnukuu Papic.
Mtoa habari huyo alisema zaidi kuwa, kocha Papic hakufurahishwa kwa jinsi wachezaji walivyokuwa wakicheza uwanjani, kwani ilionekana kama vile kila mmoja alikuwa akicheza kwa kiwango cha kipaji chake na si kwa ushirikiano.
"Kwa sasa amepania kufanya mabadiliko makubwa na ameagiza kila mchezaji kuhakikisha anacheza kwa nguvu na kujituma, vinginevyo ajiandae kuondoka klabuni," aliongeza zaidi mchezaji huyo.
"Amelalamika pia uchoyo wa pasi. Hapendi mchezaji kukaa na mpira muda mrefu, lakini hili aliliona kwa Yanga na Simba hawakutaka kuiga mchezo wa kukaa na mpira muda mrefu kama tulivyofanya sisi ndio maana waliweza kujipanga vizuri hata baada ya kubaki wachezaji wachache uwanjani."
"Kuanzia sasa na kuendelea kila mchezaji ajione ana wajibu wa kufanya vizuri, lakini kwa yule ambaye hatakuwa tayari kufanya vizuri, hii itakuwa ni juu yake. "
Alisema zaidi kuwa, Papic si kocha wa utani na hapendi kuona wachezaji wakifanya mchezo wakati akifundisha na ndio maana aliwahi kumtimua mchezaji mmoja kwenye mazoezi baada ya kufanya mambo ya utani.
No comments:
Post a Comment