Friday, August 14, 2009

Cheo 'chamdatisha' Chano

Na Badru Kimwaga, Jijini
KATIKA hali inayoonekana kama kupagawa na cheo kipya, mhazini mpya wa kuajiriwa wa klabu ya Simba, Almasi Chano, amesema haamini hadi sasa kama yeye ndiye bosi mpya wa nafasi hiyo nyeti.
Aidha, Chano amewamwagia shukrani viongozi wenzake, kamati ya utendaji pamoja na wanachama kwa ujumla wa Simba kwa kumuamini na kumpa cheo hicho kipya akiahidi kukitumikia kwa uadilifu katika muda wa ajira yake.
Akizungumza na jana, Chano aliyekuwa mhazini msaidizi wa klabu hiyo, alisema haamini kama amefanikiwa kukwea nafasi hiyo ndani ya Simba kutokana na ukweli hakuwahi kuota kabisa kuipata.
"Kwa kweli siwezi kueleza furaha yangu ya kuweza kuteuliwa nafasi hii kubwa, ukweli sikuwahi kuifikiria, nawashukuru wote walioniteua," alisema Chano.
Chano aliongeza kuteuliwa kwake bila shaka ni salamu kwa wote waliokuwa wakimtilia mashaka na kumpakazia kashfa mbalimbali, akidai kama asingekuwa muadilifu asingeipata nafasi hiyo katika klabu hiyo kubwa.
"Nadhani wale waliokuwa wakinipakazia na kunizushia wamepata salamu ni kiasi gani ninavyoaminiwa ndani ya Simba," alisema Chano.
Chano alisema hawezi kuahidi chochote kwa sasa hadi kwanza apokee rasmi barua yake ya ajira, lakini aliwashukuru wale wajumbe wa kamati ya utendaji iliyomteua yeye na wenzake wawili kama waajiriwa wa kwanza wapya na pia kuwapa ahsante wanachama wote wa Simba kwa kumuamini.
Mhazini huyo, aliteuliwa pamoja na Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda na Afisa Habari, Clifford Ndimbo kushikilia nyadhifa zao za kuajiriwa kwa muda wa miezi minne katika kikao cha kamati ya utendaji cha Simba kilichofanyika juzi.

No comments:

Post a Comment