Thursday, August 20, 2009

IOC, TOC kuwafunda waandishi wa michezo


Na Jacqueline Massano
KAMATI ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kwa kushirikiana na Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) zimeandaa semina ya kimataifa ya siku mbili kwa waandishi habari za michezo wanawake itakaofanyika mjini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi amesema semina hiyo inatarajia kuanza kesho na kumalizika siku inayofuata.
Bayi amesema mkutano huo una lengo la kuwaelemisha waandishi hao juu ya thamani ya Olympiki na vile vile kuwajengea uwezo ili waweze kufanya kazi zao kwa umakini zaidi.
Aidha, mkutano huo pia utawawezesha kutambua umuhimu wao wakiwa kama waandishi wa habari wanawake na wajibu wao katika kukuza michezo na wanamichezo wanawake katika nchi zao.
Amesema semina hiyo inatarajia kuhudhuriwa na waandishi wa habari 28 wanaoandika michezo kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
"Huu utakuwa ni uwanja kwa wanahabari kuweza kujadili na kubadilishana mawazo ya jinsi ya kukuza mahusiano kati yao na wanamichezo na kuboresha utendaji wa kazi zao," alisema.
Katibu huyo amesema pia waandishi hao watafahamishwa juu ya utendaji wa kazi wa Kamati ya Olympiki ya Kimataifa pamoja na idara zake ili kuweza kufikia malengo yao ya kuwawezesha wanawake.
Amezitaja mada ambazo zitajadiliwa kwenye semina hiyo ni pamoja na changamoto zinazowakabili wandishi wa habari wanawake na jinsi ya kukabiliana nazo, Michezo ya Wanawake nchini na jinsi ya kuboresha uandishi wao na kuepukana na vikwazo.
Ameongeza kuwa waandishi watajifunza mambo mbalimbali na pia watapata uzoefu kutoka kwa washiriki kutoka Uganda na Kenya.

Mrwanda kitanzini Simba

Na Jacqueline Massano, Jijini

BAADA ya mshambuliaji wa Simba, Danny Mrwanda kumjibu kwa kejeli bosi wake, Omary Gumbo, uongozi wa klabu hiyo unatarajia kukutana mara baada ya kumaliza mechi zao za Majimaji na Prisons ili kumjadili mchezaji huyo.
Akizungumza na blogu hii mapema leo, Katibu Mkuu wa Simba, Mwina Kaduguda amesema kitendo kilichofanywa na Mrwanda si cha kiungwana na ni cha udhalilishaji.
"Hawezi kumjibu bosi wake kama mtoto mwenzake, yeye alikuwa amekosea na alitakiwa kuwa mstaarabu na mwenye hekima," alisema Kaduguda.
Alisema kamati hiyo itakapokutana italijadili suala hilo na kabla ya kumchukulia hatua, itamwita ili aweze kutoa maelezo.
Kaduguda alisema mshambuliaji huyo alikuwa amekosea na wakati alipokuwa akionywa na mkuu wa msafara ambaye alikuwa Gumbo alimjibu kwa jeuri.
"Mrwanda alimjibu vibaya Gumbo, alimwambia usinibabaishe na amesahau kuwa Gumbo ni mmoja wa viongozi wa klabu ya Simba," alisema.
Hata hivyo, Kaduguda alikanusha kama Gumbo alizichapa na Mrwanda kama baadhi ya magazeti yalivyoandika.
Amesema wakati timu hiyo ilipokuwa ikisafiri wachezaji wote walivaa nguo zenye nembo ya Kilimanjaro isipokuwa Mrwanda ambaye aliambiwa na meneja wa timu hiyo, Innocent Njovu lakini alikaidi.
"Bahati nzuri wakati Njovu anazungumzia suala hilo, Gumbo alikuwa karibu ndiyo ikabidi aingilie kati na kumwambia Mrwanda kuwa anachofanya si sahihi lakini mshambuliaji huyo alimjibu vibaya Gumbo.
"Kwa kweli Gumbo hakupigana na Mrwanda, alipoona amejibiwa vibaya ilibidi anyamaze kimya," aliongeza.
Kaduguda amesema wakati wanaingia mkataba na TBL, moja ya kipengele chao cha makubaliano ni lazima wachezaji wote wavae nguo zenye nembo ya kilimanjaro wakiwa safarini na kambini na wala si vinginevyo.
"Huo ndiyo mkataba tulioingia na TBL, hatuwezi kupoteza mamilioni ya fedha kwa upuuzi unaofanywa na mchezaji mmoja wa kukataa kuvaa nguo zao," alisema.

Wednesday, August 19, 2009

Tuesday, August 18, 2009

Arsernal kuifuata Celtic leo

GLASGOW, Scotland
ARSENAL leo itakuwa na kibarua cha kuwanyamazisha wapenzi wa soka wa hapa wakati itakapokabiliana na Celtic katika mchezo wa kwanza wa kusaka nafasi ya kucheza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Celtic imekuwa tishio inapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Celtic Park na ina rekodi nzuri, ambapo iliilazimisha sare ya 1-1 Manchester United msimu uliopita.
"Siku zote hali ni tete Scotland," alisema kocha wa Arsenal, Arsene Wenger akizungumzia mchezo wa leo usiku."
Endapo tutacheza vizuri tunaweza kuifanya hali kuwa shwari..."
Celtic iliweka rekodi ya mahudhurio ya watazamaji kwa klabu za Ulaya wakati watazamaji 133,961 walipojitokeza kushuhudia kikosi cha Jock Stein kikiichapa Leeds katika nusu fainali ya mashindano ya Ulaya mwaka 1970 kwenye uwanja wa Hampden Park, lakini Wenger anaamini kuwa kikosi chake kitaendana na hali yoyote.
"Tumecheza Ulaya katika hali zenye ushindani mkubwa na kutokana na uzoefu wetu tunajua tufanye nini ili tuendane na hali, " aliongeza kocha huyo.

Micho amjia juu Ivo


Na Jacqueline Massano, Jijini
WAKATI aliyekuwa kipa wa St. George ya Ethiopia, Ivo Mapunda akilalamika kutemwa dakika za majeruhi na klabu yake hiyo, kocha wa timu hiyo, Milutin Sredejovic 'Micho' amesema kukosa nidhamu na kushuka kwa kiwango kwa mchezaji huyo ndiko kumesababisha atemwe.
"Ivo anatakiwa aseme ukweli na wala si kusema ameachwa dakika za majeruhi, hivi kwa nini wachezaji wa bongo huwa wakishindwa wanasingizia mambo mengi," amehoji Micho.
Ameendelea kusema, "Ivo nilikuwa nampenda sana nilijitahidi kumsaidia kila kitu, pia nilitamani aendelee mbele zaidi lakini kutokana na mambo yake sikuwa na jinsi ya kumbeba."
Micho ameiambia blogu hii mapema jana kwa njia ya mtandao kuwa mchezaji huyo hatakiwi kulalamika kwa sababu alinunuliwa na klabu hiyo na kuchukuliwa kama mfalme siku zote alizokuwa akiitumia timu hiyo.
Kocha huyo amesema katika mechi za kwanza za ligi, kipa huyo alifanya vizuri sana na kuwavutia mashabiki wa Ethiopia kutokana na udakaji wake lakini baada ya siku kwenda akaonekana anabadilika.
"Ivo alipendwa na mashabiki wa St. George na kumuona kama mfalme, lakini mwishoni mwa ligi ndipo alipoanza kuvurunda, sioni sababu ya yeye kulalamika wakati ameichezea bahati mwenyewe," alisema.
Hata hivyo, Micho alisema baada ya kugundua kuwa mashabiki wa klabu hiyo hawamtaki tena kipa huyo ndipo alipoamua kumpeleka Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye klabu inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.
"Ilifika kipindi nikimpanga Ivo uwanjani kwa ajili ya kudaka mashabiki wanaanza kumzomea wakidai kuwa hawamtaki, ni kutokana na kuanza kufungwa magoli ya kizembe.
"Lakini sikukata tamaa niliamua kumtafutia timu nje, na hii yote ni kwa ajili ya kupenda maendeleo yake lakini hata huko nako alishindwa majaribio," alisema kocha huyo ambaye amewahi kuifundisha Yanga kwa misimu miwili.

Sunday, August 16, 2009

Yanga yaamia Jangwani

Na Jacqueline Massano, Jijini

BAADA ya kuchapwa bao 2-1 na Mtibwa Sugar katika mechi ya kuwania kombe la Hisani, Wachezaji wa Yanga wameingia kambini kwao Jangwani rasmi jana usiku.
Awali Yanga ilikuwa ikifanya mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani wakati ikiendelea kusubiri vitu kadhaa viendelee kukamilishwa ndani Jengo lao lililopo mtaa wa Twiga na Jangwani.
Habari zilizopatikana mapema leo kutoka kwa mmoja wa wachezaji wa klabu hiyo, ni kwamba wameanza kuingia kambini kuanzia jana usiku mara walipomaliza kupokea kipigo kutoka kwa Mtibwa Sugar.
Alasiri ilipomuuliza mchezaji huyo kuhusiana na mazingira na kambi yao, alisema: "Kwa kweli itakuwa ngumu kuelezea sasa hivi kwa sababu ndiyo kwanza jana tumeingia tena usiku, labda kadri tutakapokuwa hapa ndiyo tutaona mapungufu.
"Ila kinachoniboa mimi ni mazingira ambayo tupo ingawa jengo letu ni zuri sana na kila chumba kina AC, kwa kweli viongozi wetu wamejiatahidi sana. Lakini mambo mengine bado sijayajua vizuri kama masuala ya msosi na mambo mengine," aliongeza mchezaji huyo
Mchezaji huyo amesema itawawia vigumu sana kupazoea mahali hapo kwa kuwa pamezungukwa na watu wengi sana na kuna kelele sana za mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wanaopenda kukaa hapo.
"Sasa hapa tutapambana na kelele za ubishi wa mashibiki na wanachama wanaopenda kukaa hapa. Kinachotakiwa ni viongozi kutuepusha na hilo kwa kuwa sisi kama wachezaji tunatakiwa kukaa sehemu isiyo na kelele wa fujo," alisema
Yanga inajiandaa na mechi yake ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya African Lyon inayotarajia kufanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Friday, August 14, 2009

ONA SASA!


MAMBO YA EXTRA BONGO HAYOOO


Cheo 'chamdatisha' Chano

Na Badru Kimwaga, Jijini
KATIKA hali inayoonekana kama kupagawa na cheo kipya, mhazini mpya wa kuajiriwa wa klabu ya Simba, Almasi Chano, amesema haamini hadi sasa kama yeye ndiye bosi mpya wa nafasi hiyo nyeti.
Aidha, Chano amewamwagia shukrani viongozi wenzake, kamati ya utendaji pamoja na wanachama kwa ujumla wa Simba kwa kumuamini na kumpa cheo hicho kipya akiahidi kukitumikia kwa uadilifu katika muda wa ajira yake.
Akizungumza na jana, Chano aliyekuwa mhazini msaidizi wa klabu hiyo, alisema haamini kama amefanikiwa kukwea nafasi hiyo ndani ya Simba kutokana na ukweli hakuwahi kuota kabisa kuipata.
"Kwa kweli siwezi kueleza furaha yangu ya kuweza kuteuliwa nafasi hii kubwa, ukweli sikuwahi kuifikiria, nawashukuru wote walioniteua," alisema Chano.
Chano aliongeza kuteuliwa kwake bila shaka ni salamu kwa wote waliokuwa wakimtilia mashaka na kumpakazia kashfa mbalimbali, akidai kama asingekuwa muadilifu asingeipata nafasi hiyo katika klabu hiyo kubwa.
"Nadhani wale waliokuwa wakinipakazia na kunizushia wamepata salamu ni kiasi gani ninavyoaminiwa ndani ya Simba," alisema Chano.
Chano alisema hawezi kuahidi chochote kwa sasa hadi kwanza apokee rasmi barua yake ya ajira, lakini aliwashukuru wale wajumbe wa kamati ya utendaji iliyomteua yeye na wenzake wawili kama waajiriwa wa kwanza wapya na pia kuwapa ahsante wanachama wote wa Simba kwa kumuamini.
Mhazini huyo, aliteuliwa pamoja na Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda na Afisa Habari, Clifford Ndimbo kushikilia nyadhifa zao za kuajiriwa kwa muda wa miezi minne katika kikao cha kamati ya utendaji cha Simba kilichofanyika juzi.

Wednesday, August 12, 2009

LEO NI LEO RWANDA

Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa 'Taifa Stars' kitakachopambana na Amavubi leo. MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI TAIFA STARS!

Ancelotti ashindwa kumnasa De Rossi



LONDON, England
CARLO Ancelotti ameshindwa kumfanya mchezaji aliyekuwemo katika kikosi cha Italia kilichotwaa Kombe la Dunia, Daniele De Rossi kuwa mchezaji wa kwanza mwenye jina kubwa kumsajili katika klabu ya Chelsea.
Kocha huyo mpya wa Blues aliwasilisha dau la paundi milioni 22 kwa ajili ya kutaka kumsajili kiungo huyo wa Roma.
Lakini ofa yake ilitupiliwa mbali na klabu ya Roma inayoshiriki Serie A ambayo ilisisitiza De Rossi, 26, hauzwi kwa bei yoyote.
Mkurugenzi wa Roma, Bruno Conti alisema: "Pamoja na kiasi kilichotolewa kuwa kikubwa lakini kilikataliwa. Kwa Roma mchezaji huyu haguswi."Naye rais wa timu hiyo, Rosella Sensi aliongeza: "De Rossi hauzwi..."
Ancelotti kwa sasa ameandaa ofa ya paundi milioni 2.5 kwa ajili ya kiungo wa Norway, Erik Huseklepp, 24.
Nyota huyo amefunga mabao matano katika mechi zake sita za mwisho alizocheza na leo usiku anatarajia kuwemo katika kikosi cha timu ya taifa ya Norway itakapocheza na Scotland.Aston Villa na Newcastle nao pia wanamsaka mchezaji huyo.

Dida amgalagaza Kaseja mazoezini


Na Adam Fungamwango, Ubungo
TIMU ya Simba imeanza tena mazoezi yake kujiandaa na ligi kuu Tanzania Bara baada ya kumalizika kwa tamasha lao la Simba Day lililofanyika Agosti 8 na kufana.
Katika mazoezi hayo, Kocha Patrick Phiri alionekana kuwafua wachezaji wake katika eneo la kutafuta pumzi, baada ya kuwakimbiza kwa karibuni robo tatu ya mazoezi hayo.
Wachezaji wote wa Simba walikuwepo, lakini waliocheza mazoezi walikuwa 12 tu, huku wegine wakiwa pembeni kwa sababu mbalimbali.
Hata hivyo wachezaji ambao wanadaiwa kuwa ni majeruhi waliongozwa na Haruna Moshi, Jabir Aziz na Adam Kingwande hawakuwepo mazoezini hapo.
Wengine ambao hawakuwepo ni wale waliokwenda kwenye timu ya Taifa, Taifa Stars.
Katika mazoezi hayo, wachezaji waliotia fora katima kumkimbia ni Uhuru Selemani ambaye ndiye anayeonekena ana mbio kuliko mchezaji yoyote ndani ya Simba akimzidi hata Mussa Hassan Mgosi.
Kivutio kikubwa kilikuwa ni baina ya makipa wawili wa timu hiyo, Deogratius Munishi Dida na Juma Kaseja ambao katika pambano lao la mbio, Dida alimgaragaza Kaseja mara zote walizokuwa wakikimbia.
Dida alionekana ni mtaalam wa kukimbia kuliko Kaseja, ingawa naye mara kadhaa alikuwa akijitahidi kwa kila hali kumpita mwenzake, lakini ilikuwa ikishindikana na kuwa burudani ya aina yake kwenye uwanja wa Kinesi Bull, ambako timu hiyo inafanya mazoezi.
Wachezaji alioonekana jana ni Mgosi, Dida, Kaseja, Emmanuel Okwi, Joseph Owino, Hiraly Echessa, Amri Kihemba, Mohamed Kijuso, Mohamed Banka, Salum Kanoni, na Uhuru.

Yanga yaiwakia TFF

Na Jacqueline Massano, Jijini
WAKATI Shirikisho la Soka nchini, TFF, likitoa tamko kuhusiana na mchezaji wa Yanga, George Owino, uongozi wa klabu hiyo umeendelea kusisitiza kwamba mchezaji huyo si wao.
Kauli ya Yanga inafuatia TFF kutoa siku tano kwa mabingwa hao wa soka Bara kukata jina moja la mchezaji mmoja wa kigeni baada ya kamati ya mashindano ya shirikisho hilo kuthibitisha Owino ni mchezaji halali wa timu hiyo.
Akizungumza mapema leo mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega amesema wanachotambua wao kama viongozi wa klabu hiyo, mchezaji huyo si wao na ameuzwa kwenye nchi nyingine ingawa hakutaka kuitaja.
"Owino si wetu sasa hivi ameshauzwa zamani na wakala wake ila kwa kuwa TFF wameamua kusema hivyo tunasubiri barua ya maamuzi yao ili na sisi tukutane na kuwajibu," alisema.
Madega amesema watakapopata barua kutoka TFF watakutana na kuipitia halafu na wao watakata rufaa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho hilo kupinga maamuzi yaliyotolewa.
Amesema watapeleka vielelezo vyote vinavyoonyesha kuwa beki huyo si mchezaji wao na sasa anaitumikia nchi nyingine.
"Hizi zote ni njama za Simba wala si vinginevyo, ila na sisi tutapeleka ushahidi wetu," alisema
Yanga ambayo haikupeleka jina la Owino katika usajili wake wa msimu huu, iliwekewa pingamizi na watani zao, Simba ikipinga hatua ya kumuacha mchezaji huyo kienyeji.

Monday, August 10, 2009

Chelsea yampandia dau Ribery


LONDON, England
ROMAN Abramovich anatarajiwa kwenda Ujerumani kuwasilisha ombi la paundi milioni 40 kwa ajili ya kumsajili winga wa Bayern Munich, Franck Ribery.
Bilionea huyo mmiliki wa Chelsea ametaka kukutana na meneja mkuu wa Bayern Munich, Uli Hoeness.
Aliweka wazi nia yake ya kutaka kumsajili nyota huyo wa Ufaransa na yuko tayari kutoa kiasi kikubwa kabisa cha pesa ambacho hakuna klabu yoyote ya Uingereza iliyowahi kuahidi ili kumpata mchezaji huyo.
Chanzo kutoka ndani ya klabu ya Bayern kilisema: "Uli alishtushwa na simu aliyopigiwa na bwana Abramovich."
Bado tumedhamiria kumbakisha Ribery lakini Hoeness alikubali kukutana na Abramovich huko Ujerumani kuzungumzia ofa hiyo."
Mwezi uliopita, Manchester United na Chelsea zote zilionyesha nia ya kutaka kumsajili Ribery katika kipindi hiki cha majira ya joto.
Hatahivyo, Man United bado haijawasilisha ofa, na Abramovich anaonekana kutaka kuizidi kete kwa kuharakisha kuwasilisha ofa hiyo.
Kocha mpya wa Blues, Carlo Ancelotti aliahidiwa na bilionea huyo wa Russia kusaini majina makubwa lakini hadi sasa maombi yake ya kutaka kumsajili Kaka na Alexandre Pato yameshindwa kufanikiwa.
Naye Ribery tayari alishaweka wazi kuwa anataka kujiunga na Real Madrid.Munich inahofu huenda Ribery akawa amesaini mkataba awali kama ule wa Cristiano Ronaldo ambao utamwezesha mchezaji huyo kuondoka katika timu hiyo na kutua Real Madrid majira yajayo ya joto.
Hasira za Munich dhidi ya jeuri ya Real Madrid, klabu hiyo ya Ujerumani huenda ikaamua kumuuza mchezaji huyo kwa Chelsea.

Majambazi yapora gari la mchezaji


LILLE, Ufaransa
MAJAMBAZI waliojifanya polisi walimfungia kwa muda katika buti la gari lake aina ya Mercedes Benzi mshambuliaji wa klabu ya Lille, Pierre-Alain Frau mapema jana, kabla ya kumuacha sehemu nyingine ya mji na kuchukua gari hilo.
Polisi walisema, wakati Frau akiingia katika gari lake, alikaribiwa na watu waliojitambulisha ni askari.
Mchezaji huyo alikuwa akirejea nyumbani baada ya kupata chakula cha jioni kufuatia Lille kupokea kipigo cha bao 2-1 na Lorient Jumapili.
Wavamizi hao walimlazimisha mchezaji huyo wa Ligue 1 kuingia ndani ya buti ya gari lake, na baadae waliliendesha gari hilo kutatisha mji.
Baadae majambazi hayo yalimtelekeza mchezaji huyo barabarani karibu na maeneo ya makazi ya watu kabla hawajaondoka na gari hilo la kifahari, kadi ya benki, simu ya mkononi na mamia ya pesa za euro.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi 10 kwa Frau kuporwa na majambazi.
Gari lake jingine liliporwa Oktoba mwaka jana.Klabu yake ilisema katika taarifa yake kuwa katika tukio hilo mchezaji huyo hakujeruhiwa na alifanya mazoezi pamoja na wenzake jana asubuhi.

Wednesday, August 5, 2009

Mlinzi wa Taasisi ya Elimu akiwa anasaidiwa baada ya kufungwa kamba na majambazi usiku wa kuamkia leo.

Simba yafyata kwa TFF

Na Jacqueline Massano, Jijini
HATIMAYE msimamo uliowekwa na Shirikisho la Soka nchini, TFF, kuhusu wachezaji wa Simba kujiunga na timu ya taifa, Taifa Stars, umefanya viongozi wa klabu hiyo kuwaruhusu wachezaji wake saba kujiunga na kambi ya Stars na kutoa masharti ya kuachiwa kabla ya Agosti 8 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda alipozungumza na mwandishi wa habari hizi mapema leo kwa njia ya simu.
Kaduguda amesema wamepokea barua kutoka Shirikisho la Soka nchini, TFF, ikiwataka iwaruhusu wachezaji hao saba kujiunga na kambi ya Stars inayojiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Amavubi ya Rwanda huko Kigali.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa Agosti 12 nchini Rwanda huku Stars ikitarajiwa kuondoka Jumapili.
Amesema baada ya kupokea barua hiyo waliwasiliana na kocha mkuu wa timu yao, Mzambia Patrick Phiri ambaye alikubaliana na ombi hilo kutokana na kumaliza programu zake za mazoezi.
Bosi huyo amesema kwa kuwa nao ni watanzania wazalendo, wameona bora wawaruhusu wachezaji hao wakaitumikie nchi yao.
Kiongozi huyo ameitaka TFF kuzingatia kwamba wachezaji hao wanatakiwa kuachiwa mapema ili wajiandae na mechi ya tamasha lao dhidi ya Villa ya Uganda linalotarajiwa kufanyika Jumamosi.
"Sisi tunachotaka wachezaji wetu warudi, kwani timu yetu inacheza na timu kubwa na itakuwa si jambo la busara kama tutachezesha wachezaji wengine wakati nyota wetu wote hawapo," alisema Kadu.
Wachezaji wa Simba walioitwa kujiunga na Stars ni Ally Mustapha 'Barthez', Juma Jabu, Kelvin Yondani, Danny Mrwanda, David Naftari, Mussa Hassan 'Mgosi' na Juma Nyoso.

Tuesday, August 4, 2009

Na mimi nimo

Yanga kupewa chao kesho

Na Jacqueline Massano, Jijini
BAADA ya vyombo mbalimbali vya habari kuandika taarifa zilizokuwa zikifanywa siri na uongozi wa Yanga kufuatia kuchelewa kuwalipa mishahara wachezaji, hatimaye uongozi umeingia mfukoni na kuahidi kutoa mishahara kesho, imefahamika.

"Tunawashuruku sana waandishi wa habari hasa gazeti la Alasiri kwa kuandika mara ya kwanza kuhusu kutolipwa mishahara yetu. Hivi navyokuambia kesho tunadaka chetu," alisema mchezaji huyo jina tunalo.
"Wapo kati yetu hawajalipwa pesa za usajili na wengi hatujalipwa mishahara ya miezi miwili, lakini kuna taarifa kuwa kesho tunaweza kupata pesa zetu zote," aliongeza.
"Usiwaone wachezaji wanafanya mazoezi, wengine wamekopwa kabisa na baadhi wamelipwa nusu kwa ahadi watalipwa hivi karibuni," alisema.
Amesema hali mbaya iliyopo ndani ya klabu hiyo inaonyesha dhahiri kuwa hali ni mbaya.
"Bora wangesema kuwa hali ni mbaya tuendelee kusubiri cha ajabu ni kwamba, wamekaa kimya na kutoa ahadi zisizotekelezeka. Nashangaa yaani mpaka waandishi wa habari waandike ndio uongozi ukubali kulipa wakati wanajua ni jukumu lao?"
Mwanzoni mwa wiki iliyopita Alasiri ilitembelea kambi ya mazoezi ya timu hiyo ambapo ilishuhudia wachezaji wachache tu, na ilipojaribu kuhoji kulikoni baadhi ya wachezaji walisema wenzao wamesusa kwa sababu ya kutolipwa pesa zao.
Lakini ilipomuuliza mtendaji Lucas Kisasa sababu za kutolipwa mishahara wachezaji, alikuwa mkali na kukana taarifa hizo huku akimtaka mwandishi kutaja majina ya wachezaji wanaodai mishahara.
Alisema: "Taja jina la mchezaji anayedai hajalipwa mshahara, nyie kazi yenu ni kuandika mambo ya kuchonganisha. Yanga kwa sasa tumetulia, andikeni habari za kukamilika kwa ukarabati wa jengo letu, habari za mishahara achana nazo.
"Hata hivyo, baada ya vyombo zaidi vya habari kuandika sakata hilo la mishahara, hatimaye uongozi ulikiri kutowalipa kwa miezi miwili na kutoa ufafanuzi wa sababu za kuchelewa kulipwa kwa mishahara hiyo.

MAMBO HAYOOOOOOOOO

MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Franco Di Santo jana amejiunga na klabu nyingine ya Ligi Kuu ya England ya Blackburn Rovers kwa mkopo ambapo ataichezea hadi Januari mwakani, imefahamika.

Monday, August 3, 2009

Yanga, Simba kazi kubwa

Na Jacqueline Massano, Jijini

ALIYEWAHI kuwa kocha mkuu wa mabingwa wa soka nchini, Yanga ambaye sasa anafundisha St. George ya Ethiopia, Milutin 'Micho' Sredejovic amesema Ligi ya Vodacom msimu huu itakuwa na ushindani mkubwa kulinganisha na mwaka uliotangulia.
"Kama Yanga hawakupata taabu sana kutwaa ubingwa msimu uliopita, wasitegemee wanaweza kufanya hivyo tena kirahisi msimu huu," alisema Micho wakati akiongea na blog hii ya Jirushe-jiachie mapema leo.
Micho amesema usajili uliofanywa na timu za Simba, Yanga African Lyon na Azam ni mzuri hivyo anategemea timu hizo zitashindana kwa kiasi kikubwa kuwania kutwaa ubingwa.
Akiongeza alisema: "Natambua kuwa timu zingine nazo zimefanya usajili mzuri, nina hakika ligi ya msimu huu itakuwa nzuri na yenye ushindani mkubwa."
"Yanga wanaweza kuwa na nafasi zaidi kwani ina wachezaji wake wengi waliokuwepo msimu uliopita na wageni waliowasajili ni wazuri zaidi.
"Simba wamefanya usajili mzuri pia, lakini kuondoka kwa Henry na Mgosi, kwangu naona ni pengo kubwa kwa kocha Patricki Phiri."Yanga imefanya usajili mzuri wa wachezaji wapya, lakini pia haikuacha wengi wa zamani. Hii ni faida kubwa kwa kocha wao.
"Lyon na Azam nazo zimetumia pesa nyingi kufanya usajili wa wachezaji wazuri. Nina hakika nne bora itajumuisha timu za Simba, Yanga, Lyon na Azam," alifafanua zaidi kocha huyo aliyeifundisha Yanga miaka miwili
"Mtibwa na Prisons nazo zitakuwa miongoni mwa timu zitakazoleta ushindani. Sina hakika na usajili wao, lakini kwa uzoefu wangu Tanzania, hizi ni timu za kuangaliwa sana," alisema.
"Nadhani Simba kuna kitu watakosa. Mgosi ni mchezaji hatari, nimesikia nakwenda kucheza soka ya kulipwa, na Henry tayari ameshaondoka. Hili ni pengo kwa Simba."Kuhusu wachezaji wa kigeni, alisema anatarajia wataleta mabadiliko makubwa katika uchezaji na hivyo kuleta changamoto kwa wachezaji wa Tanzania.
"Ligi inapokuwa na wachezaji wengi wa kigeni, kunaongeza msisimko na ushindani, hili ndilo naloliona kwa sasa katika msimu ujao wa ligi," alisema kocha huyo.
Aliongeza: "Inawezekana utamaduni wa timu za Simba na Yanga kuonekana wababe katika kila msimu wa ligi, mwaka huu ukapungua na kushuhudia timu zingine zikitesa nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi."