Wednesday, August 5, 2009

Simba yafyata kwa TFF

Na Jacqueline Massano, Jijini
HATIMAYE msimamo uliowekwa na Shirikisho la Soka nchini, TFF, kuhusu wachezaji wa Simba kujiunga na timu ya taifa, Taifa Stars, umefanya viongozi wa klabu hiyo kuwaruhusu wachezaji wake saba kujiunga na kambi ya Stars na kutoa masharti ya kuachiwa kabla ya Agosti 8 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda alipozungumza na mwandishi wa habari hizi mapema leo kwa njia ya simu.
Kaduguda amesema wamepokea barua kutoka Shirikisho la Soka nchini, TFF, ikiwataka iwaruhusu wachezaji hao saba kujiunga na kambi ya Stars inayojiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Amavubi ya Rwanda huko Kigali.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa Agosti 12 nchini Rwanda huku Stars ikitarajiwa kuondoka Jumapili.
Amesema baada ya kupokea barua hiyo waliwasiliana na kocha mkuu wa timu yao, Mzambia Patrick Phiri ambaye alikubaliana na ombi hilo kutokana na kumaliza programu zake za mazoezi.
Bosi huyo amesema kwa kuwa nao ni watanzania wazalendo, wameona bora wawaruhusu wachezaji hao wakaitumikie nchi yao.
Kiongozi huyo ameitaka TFF kuzingatia kwamba wachezaji hao wanatakiwa kuachiwa mapema ili wajiandae na mechi ya tamasha lao dhidi ya Villa ya Uganda linalotarajiwa kufanyika Jumamosi.
"Sisi tunachotaka wachezaji wetu warudi, kwani timu yetu inacheza na timu kubwa na itakuwa si jambo la busara kama tutachezesha wachezaji wengine wakati nyota wetu wote hawapo," alisema Kadu.
Wachezaji wa Simba walioitwa kujiunga na Stars ni Ally Mustapha 'Barthez', Juma Jabu, Kelvin Yondani, Danny Mrwanda, David Naftari, Mussa Hassan 'Mgosi' na Juma Nyoso.

No comments:

Post a Comment