Wednesday, August 12, 2009

Yanga yaiwakia TFF

Na Jacqueline Massano, Jijini
WAKATI Shirikisho la Soka nchini, TFF, likitoa tamko kuhusiana na mchezaji wa Yanga, George Owino, uongozi wa klabu hiyo umeendelea kusisitiza kwamba mchezaji huyo si wao.
Kauli ya Yanga inafuatia TFF kutoa siku tano kwa mabingwa hao wa soka Bara kukata jina moja la mchezaji mmoja wa kigeni baada ya kamati ya mashindano ya shirikisho hilo kuthibitisha Owino ni mchezaji halali wa timu hiyo.
Akizungumza mapema leo mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega amesema wanachotambua wao kama viongozi wa klabu hiyo, mchezaji huyo si wao na ameuzwa kwenye nchi nyingine ingawa hakutaka kuitaja.
"Owino si wetu sasa hivi ameshauzwa zamani na wakala wake ila kwa kuwa TFF wameamua kusema hivyo tunasubiri barua ya maamuzi yao ili na sisi tukutane na kuwajibu," alisema.
Madega amesema watakapopata barua kutoka TFF watakutana na kuipitia halafu na wao watakata rufaa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho hilo kupinga maamuzi yaliyotolewa.
Amesema watapeleka vielelezo vyote vinavyoonyesha kuwa beki huyo si mchezaji wao na sasa anaitumikia nchi nyingine.
"Hizi zote ni njama za Simba wala si vinginevyo, ila na sisi tutapeleka ushahidi wetu," alisema
Yanga ambayo haikupeleka jina la Owino katika usajili wake wa msimu huu, iliwekewa pingamizi na watani zao, Simba ikipinga hatua ya kumuacha mchezaji huyo kienyeji.

No comments:

Post a Comment