Monday, August 3, 2009

Yanga, Simba kazi kubwa

Na Jacqueline Massano, Jijini

ALIYEWAHI kuwa kocha mkuu wa mabingwa wa soka nchini, Yanga ambaye sasa anafundisha St. George ya Ethiopia, Milutin 'Micho' Sredejovic amesema Ligi ya Vodacom msimu huu itakuwa na ushindani mkubwa kulinganisha na mwaka uliotangulia.
"Kama Yanga hawakupata taabu sana kutwaa ubingwa msimu uliopita, wasitegemee wanaweza kufanya hivyo tena kirahisi msimu huu," alisema Micho wakati akiongea na blog hii ya Jirushe-jiachie mapema leo.
Micho amesema usajili uliofanywa na timu za Simba, Yanga African Lyon na Azam ni mzuri hivyo anategemea timu hizo zitashindana kwa kiasi kikubwa kuwania kutwaa ubingwa.
Akiongeza alisema: "Natambua kuwa timu zingine nazo zimefanya usajili mzuri, nina hakika ligi ya msimu huu itakuwa nzuri na yenye ushindani mkubwa."
"Yanga wanaweza kuwa na nafasi zaidi kwani ina wachezaji wake wengi waliokuwepo msimu uliopita na wageni waliowasajili ni wazuri zaidi.
"Simba wamefanya usajili mzuri pia, lakini kuondoka kwa Henry na Mgosi, kwangu naona ni pengo kubwa kwa kocha Patricki Phiri."Yanga imefanya usajili mzuri wa wachezaji wapya, lakini pia haikuacha wengi wa zamani. Hii ni faida kubwa kwa kocha wao.
"Lyon na Azam nazo zimetumia pesa nyingi kufanya usajili wa wachezaji wazuri. Nina hakika nne bora itajumuisha timu za Simba, Yanga, Lyon na Azam," alifafanua zaidi kocha huyo aliyeifundisha Yanga miaka miwili
"Mtibwa na Prisons nazo zitakuwa miongoni mwa timu zitakazoleta ushindani. Sina hakika na usajili wao, lakini kwa uzoefu wangu Tanzania, hizi ni timu za kuangaliwa sana," alisema.
"Nadhani Simba kuna kitu watakosa. Mgosi ni mchezaji hatari, nimesikia nakwenda kucheza soka ya kulipwa, na Henry tayari ameshaondoka. Hili ni pengo kwa Simba."Kuhusu wachezaji wa kigeni, alisema anatarajia wataleta mabadiliko makubwa katika uchezaji na hivyo kuleta changamoto kwa wachezaji wa Tanzania.
"Ligi inapokuwa na wachezaji wengi wa kigeni, kunaongeza msisimko na ushindani, hili ndilo naloliona kwa sasa katika msimu ujao wa ligi," alisema kocha huyo.
Aliongeza: "Inawezekana utamaduni wa timu za Simba na Yanga kuonekana wababe katika kila msimu wa ligi, mwaka huu ukapungua na kushuhudia timu zingine zikitesa nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi."

No comments:

Post a Comment