Thursday, August 20, 2009

Mrwanda kitanzini Simba

Na Jacqueline Massano, Jijini

BAADA ya mshambuliaji wa Simba, Danny Mrwanda kumjibu kwa kejeli bosi wake, Omary Gumbo, uongozi wa klabu hiyo unatarajia kukutana mara baada ya kumaliza mechi zao za Majimaji na Prisons ili kumjadili mchezaji huyo.
Akizungumza na blogu hii mapema leo, Katibu Mkuu wa Simba, Mwina Kaduguda amesema kitendo kilichofanywa na Mrwanda si cha kiungwana na ni cha udhalilishaji.
"Hawezi kumjibu bosi wake kama mtoto mwenzake, yeye alikuwa amekosea na alitakiwa kuwa mstaarabu na mwenye hekima," alisema Kaduguda.
Alisema kamati hiyo itakapokutana italijadili suala hilo na kabla ya kumchukulia hatua, itamwita ili aweze kutoa maelezo.
Kaduguda alisema mshambuliaji huyo alikuwa amekosea na wakati alipokuwa akionywa na mkuu wa msafara ambaye alikuwa Gumbo alimjibu kwa jeuri.
"Mrwanda alimjibu vibaya Gumbo, alimwambia usinibabaishe na amesahau kuwa Gumbo ni mmoja wa viongozi wa klabu ya Simba," alisema.
Hata hivyo, Kaduguda alikanusha kama Gumbo alizichapa na Mrwanda kama baadhi ya magazeti yalivyoandika.
Amesema wakati timu hiyo ilipokuwa ikisafiri wachezaji wote walivaa nguo zenye nembo ya Kilimanjaro isipokuwa Mrwanda ambaye aliambiwa na meneja wa timu hiyo, Innocent Njovu lakini alikaidi.
"Bahati nzuri wakati Njovu anazungumzia suala hilo, Gumbo alikuwa karibu ndiyo ikabidi aingilie kati na kumwambia Mrwanda kuwa anachofanya si sahihi lakini mshambuliaji huyo alimjibu vibaya Gumbo.
"Kwa kweli Gumbo hakupigana na Mrwanda, alipoona amejibiwa vibaya ilibidi anyamaze kimya," aliongeza.
Kaduguda amesema wakati wanaingia mkataba na TBL, moja ya kipengele chao cha makubaliano ni lazima wachezaji wote wavae nguo zenye nembo ya kilimanjaro wakiwa safarini na kambini na wala si vinginevyo.
"Huo ndiyo mkataba tulioingia na TBL, hatuwezi kupoteza mamilioni ya fedha kwa upuuzi unaofanywa na mchezaji mmoja wa kukataa kuvaa nguo zao," alisema.

No comments:

Post a Comment