Thursday, August 20, 2009

IOC, TOC kuwafunda waandishi wa michezo


Na Jacqueline Massano
KAMATI ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kwa kushirikiana na Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) zimeandaa semina ya kimataifa ya siku mbili kwa waandishi habari za michezo wanawake itakaofanyika mjini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi amesema semina hiyo inatarajia kuanza kesho na kumalizika siku inayofuata.
Bayi amesema mkutano huo una lengo la kuwaelemisha waandishi hao juu ya thamani ya Olympiki na vile vile kuwajengea uwezo ili waweze kufanya kazi zao kwa umakini zaidi.
Aidha, mkutano huo pia utawawezesha kutambua umuhimu wao wakiwa kama waandishi wa habari wanawake na wajibu wao katika kukuza michezo na wanamichezo wanawake katika nchi zao.
Amesema semina hiyo inatarajia kuhudhuriwa na waandishi wa habari 28 wanaoandika michezo kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
"Huu utakuwa ni uwanja kwa wanahabari kuweza kujadili na kubadilishana mawazo ya jinsi ya kukuza mahusiano kati yao na wanamichezo na kuboresha utendaji wa kazi zao," alisema.
Katibu huyo amesema pia waandishi hao watafahamishwa juu ya utendaji wa kazi wa Kamati ya Olympiki ya Kimataifa pamoja na idara zake ili kuweza kufikia malengo yao ya kuwawezesha wanawake.
Amezitaja mada ambazo zitajadiliwa kwenye semina hiyo ni pamoja na changamoto zinazowakabili wandishi wa habari wanawake na jinsi ya kukabiliana nazo, Michezo ya Wanawake nchini na jinsi ya kuboresha uandishi wao na kuepukana na vikwazo.
Ameongeza kuwa waandishi watajifunza mambo mbalimbali na pia watapata uzoefu kutoka kwa washiriki kutoka Uganda na Kenya.

No comments:

Post a Comment