Tuesday, October 27, 2009

Micho aitabiria ushindi Yanga

Na Renatha Msungu

ALIYEKUWA kocha mkuu wa klabu ya Yanga, Milutin Sredejovic 'Micho' ameitabiria timu yake hiyo ya zamani kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani zao wa Jadi, Simba.
Yanga na Simba inatarajia kumenyana Jumamosi ya wiki hii jijini Dar es Salaam, kwenye mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Akitoa maoni yake kwa njia ya mtandao jana, kocha huyo ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya St. George ya Ethiopia, alisema Yanga ina asilimia kubwa ya kushinda mechi hiyo kwa sababu itakuwa imejiandaa kiakili tofauti na Simba.
Micho alisema mechi hiyo ambayo Simba imejiwekea matumaini ya kushinda itakuwa ni ngumu kwa sababu hata Yanga nayo imepania kuibuka na ushindi huo ili iliweze kutetea taji lake.
"Simba imeshajiwekea kushinda mechi hiyo kwa kuwa imeanza vizuri katika ligi hiyo na ndiyo maana hata mechi yake dhidi ya Yanga inaiona ni nyepesi tu," alisema Micho
Alifafanua zaidi kuwa Simba inaweza kupoteza mchezo huo kwa sababu itaingia uwanjani kwa kujiamini na pia tayari imeishaidharau Yanga kuwa haiwezi kushinda mechi hiyo.
Aidha, kocha huyo alisema aliwahi kushuhudia timu ikiingia uwanjani kwa kujiamini lakini hatimaye ilifungwa na timu ambayo haikuwa dalili ya kufanya vizuri kwenye mechi hiyo. "Simba inajiamini sana, lakini mimi nikiwa kama kocha mwenye uzoefu ikifanya mchezo inaweza kufungwa na Yanga tena bao 1-0 na wala si zaidi ya hapo, na ikijitahidi sana inaweza kutoka sare ya bao 1-1," alisema kocha huyo

No comments:

Post a Comment