Tuesday, August 4, 2009

Yanga kupewa chao kesho

Na Jacqueline Massano, Jijini
BAADA ya vyombo mbalimbali vya habari kuandika taarifa zilizokuwa zikifanywa siri na uongozi wa Yanga kufuatia kuchelewa kuwalipa mishahara wachezaji, hatimaye uongozi umeingia mfukoni na kuahidi kutoa mishahara kesho, imefahamika.

"Tunawashuruku sana waandishi wa habari hasa gazeti la Alasiri kwa kuandika mara ya kwanza kuhusu kutolipwa mishahara yetu. Hivi navyokuambia kesho tunadaka chetu," alisema mchezaji huyo jina tunalo.
"Wapo kati yetu hawajalipwa pesa za usajili na wengi hatujalipwa mishahara ya miezi miwili, lakini kuna taarifa kuwa kesho tunaweza kupata pesa zetu zote," aliongeza.
"Usiwaone wachezaji wanafanya mazoezi, wengine wamekopwa kabisa na baadhi wamelipwa nusu kwa ahadi watalipwa hivi karibuni," alisema.
Amesema hali mbaya iliyopo ndani ya klabu hiyo inaonyesha dhahiri kuwa hali ni mbaya.
"Bora wangesema kuwa hali ni mbaya tuendelee kusubiri cha ajabu ni kwamba, wamekaa kimya na kutoa ahadi zisizotekelezeka. Nashangaa yaani mpaka waandishi wa habari waandike ndio uongozi ukubali kulipa wakati wanajua ni jukumu lao?"
Mwanzoni mwa wiki iliyopita Alasiri ilitembelea kambi ya mazoezi ya timu hiyo ambapo ilishuhudia wachezaji wachache tu, na ilipojaribu kuhoji kulikoni baadhi ya wachezaji walisema wenzao wamesusa kwa sababu ya kutolipwa pesa zao.
Lakini ilipomuuliza mtendaji Lucas Kisasa sababu za kutolipwa mishahara wachezaji, alikuwa mkali na kukana taarifa hizo huku akimtaka mwandishi kutaja majina ya wachezaji wanaodai mishahara.
Alisema: "Taja jina la mchezaji anayedai hajalipwa mshahara, nyie kazi yenu ni kuandika mambo ya kuchonganisha. Yanga kwa sasa tumetulia, andikeni habari za kukamilika kwa ukarabati wa jengo letu, habari za mishahara achana nazo.
"Hata hivyo, baada ya vyombo zaidi vya habari kuandika sakata hilo la mishahara, hatimaye uongozi ulikiri kutowalipa kwa miezi miwili na kutoa ufafanuzi wa sababu za kuchelewa kulipwa kwa mishahara hiyo.

No comments:

Post a Comment