Sunday, August 16, 2009

Yanga yaamia Jangwani

Na Jacqueline Massano, Jijini

BAADA ya kuchapwa bao 2-1 na Mtibwa Sugar katika mechi ya kuwania kombe la Hisani, Wachezaji wa Yanga wameingia kambini kwao Jangwani rasmi jana usiku.
Awali Yanga ilikuwa ikifanya mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani wakati ikiendelea kusubiri vitu kadhaa viendelee kukamilishwa ndani Jengo lao lililopo mtaa wa Twiga na Jangwani.
Habari zilizopatikana mapema leo kutoka kwa mmoja wa wachezaji wa klabu hiyo, ni kwamba wameanza kuingia kambini kuanzia jana usiku mara walipomaliza kupokea kipigo kutoka kwa Mtibwa Sugar.
Alasiri ilipomuuliza mchezaji huyo kuhusiana na mazingira na kambi yao, alisema: "Kwa kweli itakuwa ngumu kuelezea sasa hivi kwa sababu ndiyo kwanza jana tumeingia tena usiku, labda kadri tutakapokuwa hapa ndiyo tutaona mapungufu.
"Ila kinachoniboa mimi ni mazingira ambayo tupo ingawa jengo letu ni zuri sana na kila chumba kina AC, kwa kweli viongozi wetu wamejiatahidi sana. Lakini mambo mengine bado sijayajua vizuri kama masuala ya msosi na mambo mengine," aliongeza mchezaji huyo
Mchezaji huyo amesema itawawia vigumu sana kupazoea mahali hapo kwa kuwa pamezungukwa na watu wengi sana na kuna kelele sana za mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wanaopenda kukaa hapo.
"Sasa hapa tutapambana na kelele za ubishi wa mashibiki na wanachama wanaopenda kukaa hapa. Kinachotakiwa ni viongozi kutuepusha na hilo kwa kuwa sisi kama wachezaji tunatakiwa kukaa sehemu isiyo na kelele wa fujo," alisema
Yanga inajiandaa na mechi yake ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya African Lyon inayotarajia kufanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment