Tuesday, August 18, 2009

Micho amjia juu Ivo


Na Jacqueline Massano, Jijini
WAKATI aliyekuwa kipa wa St. George ya Ethiopia, Ivo Mapunda akilalamika kutemwa dakika za majeruhi na klabu yake hiyo, kocha wa timu hiyo, Milutin Sredejovic 'Micho' amesema kukosa nidhamu na kushuka kwa kiwango kwa mchezaji huyo ndiko kumesababisha atemwe.
"Ivo anatakiwa aseme ukweli na wala si kusema ameachwa dakika za majeruhi, hivi kwa nini wachezaji wa bongo huwa wakishindwa wanasingizia mambo mengi," amehoji Micho.
Ameendelea kusema, "Ivo nilikuwa nampenda sana nilijitahidi kumsaidia kila kitu, pia nilitamani aendelee mbele zaidi lakini kutokana na mambo yake sikuwa na jinsi ya kumbeba."
Micho ameiambia blogu hii mapema jana kwa njia ya mtandao kuwa mchezaji huyo hatakiwi kulalamika kwa sababu alinunuliwa na klabu hiyo na kuchukuliwa kama mfalme siku zote alizokuwa akiitumia timu hiyo.
Kocha huyo amesema katika mechi za kwanza za ligi, kipa huyo alifanya vizuri sana na kuwavutia mashabiki wa Ethiopia kutokana na udakaji wake lakini baada ya siku kwenda akaonekana anabadilika.
"Ivo alipendwa na mashabiki wa St. George na kumuona kama mfalme, lakini mwishoni mwa ligi ndipo alipoanza kuvurunda, sioni sababu ya yeye kulalamika wakati ameichezea bahati mwenyewe," alisema.
Hata hivyo, Micho alisema baada ya kugundua kuwa mashabiki wa klabu hiyo hawamtaki tena kipa huyo ndipo alipoamua kumpeleka Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye klabu inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.
"Ilifika kipindi nikimpanga Ivo uwanjani kwa ajili ya kudaka mashabiki wanaanza kumzomea wakidai kuwa hawamtaki, ni kutokana na kuanza kufungwa magoli ya kizembe.
"Lakini sikukata tamaa niliamua kumtafutia timu nje, na hii yote ni kwa ajili ya kupenda maendeleo yake lakini hata huko nako alishindwa majaribio," alisema kocha huyo ambaye amewahi kuifundisha Yanga kwa misimu miwili.

No comments:

Post a Comment