Friday, October 30, 2009

Nyasi za Taifa kuwaka moto kesho

(kocha wa Simba-Patrick Phiri)
(Kocha wa Yanga-Kostadin Papic)

Na Badru Kimwaga, Jijini
VIGOGO vya soka nchini Simba na Yanga Jumamosi wanatarajiwa kuwa 'vitani' katika pambano la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2009-2010.
Hilo litakuwa pambano la 127 kati yao tangu mwaka 1953, likijumuisha ile ya ligi na mingineyo iwe ya vikombe au ya kirafiki.Katika mechi zao za awali 126, Yanga ndio wanaoongoza kwa kushinda mechi nyingi ukilinganisha na watani zao, wakiibuka kidedea mara 47 dhidi 42 za watani zao na kupata sare mechi 37.
Tangu 1965 kwa michezo ya ligi bila kujali kama ni ya Tanzania Bara au Muungano, Yanga imeshinda mechi 30 dhidi ya 25 za watani zao na sare mbalimbali ni mechi 27, huku Yanga ikifunga mabao 95 na kufungwa 82 na kujikusanyia jumla ya pointi 122 dhidi ya 101 za Simba.
Pamoja na Yanga kuongoza karibu kila mlolongo wa mechi za watani, bado imeshindwa kuvunja rekodi ya idadi kubwa ya magoli iliyowekwa na Simba Julai 19, 1977 walipolala mabao 6-0.Kipigo hicho kilichokuwa kisasi cha Simba dhidi ya Yanga iliyowalaza mabao 5-0 mnamo Juni Mosi, 1968, mpaka leo kimekuwa 'mzimu' unaoisumbua Yanga kwa miaka 32 sasa.
Katika mechi hiyo ya kihistoria mshambuliaji, Abdalla Kibaden 'King Mputa' alifunga mabao matatu peke yake, kitu kilichoshindwa kufanywa na mwingine katika historia za timu hizo katika ligi tangu 1965.
Hata hivyo wapo waliofunga mabao mawili katika mechi moja za watani hao ambapo kwa upande wa Yanga ni marehemu Maulid Dilunga, Saleh Zimbwe na Said Mwamba. Wengine ni Omar Husseni 'Keegan' na Idd Moshi.Kwa Simba wapo Jumanne Hassani 'Masimenti', Dua Said, Emmanuel Gabriel, Nico Nyagawa na Steven Mapunda 'Garincha'.
Beki Seleman Sanga wa Yanga ndiye wa kwanza kujifunga katika mechi za watani alipofanya hivyo mwaka 1977 katika kipigo cha mabao 6-0, Lilla Shomari wa Simba aliyejifunga 1983, Simba ikilala mabao 2-0 na Mustafa Hozza wa Simba alifanya hivyo 1996 Yanga na Simba zilipotoka sare ya 4-4 Omar Husseni 'Keegan' wa Yanga, nduye anayeongoza kwa kufunga magoli mengi katika mechi baina ya vigogo hivyo akiwa na goli sita akifuatiwa na marehemu Edward Chumila wa Simba mwenye mabao mabao matano.
Wachezaji Abeid Mziba 'Tekelo', Makumbi Juma 'Homa ya Jiji', Sekilojo Chambua na Idd Moshi wa Yanga na Dua Said wa Simba wanafuatia katika orodha hiyo kwa kufunga mabao manne kila mmoja.
Wapo waliofunga magoli matatu ambao ni Kibadeni, Kitwana Manara 'Popat' na Said Mwamba 'Kizota', huku kukiwa na orodha ndefu ya waliofunga mabao mawili na moja moja.
Zipo mechi zingine za vikombe kadhaa kama vile vya Tusker ama mechi za kirafiki timu hizo zimeweza kutambiana kwa zamu, lakini Simba ikiongoza kwa kushinda mechi nyingi.
Kwa mujibu wa kumbukumbu tulizonazo ni kwamba tangu mwaka 2001, Simba na Yanga zimekutana mara 17 katika ligi na Simba wakishinda mara nane huku watani wakitamba mara moja na wote wakapata sare mara nane.
Mara ya mwisho Yanga kula kichapo kwa Simba ilikuwa Oktoba 24, 2007 ilipolala bao 1-0, Morogoro kwa bao la Ulimboka Mwakingwe na kuzinduka mwaka jana walipoilaza Simba kwa bao la Mkenya Ben Mwalala.
Kwa kuangalia hali ilivyo Yanga katika mechi ijayo itakuwa na kazi kubwa ya kulinda ushindi wao wa mwaka jana na pia kuvunja rekodi ya miaka 32 ya Simba ya kipiugo cha mwaka 1977.Pia itataka kuzuia rekodi ya Simba ya kushinda mechi mfululizo bila kufungwa au kuambulia sare katika ligi ya msimu huu.
Yanga inayotetea taji la ligi hiyo, ina nyota kadhaa wa ndani na nje ya nchi ambao hata hivyo hawajaonyesha makeke kama wenzao wa Simba waliosajili 'mapro' watatu tu ambao tayari wameshaonyesha umahiri wao.
Wageni hao wa Simba ni pamoja na Joseph Owino, Hilary Ichessa na Emmanuel Okwi, ambao kila mmoja ameshafumainia nyavu, huku Yanga mgeni aliyefunga ni Mike Baraza, huku wengine wakivurunda.
Timu zote kama msimu uliopita zipo chini ya makocha wa kigeni, Simba ikiwa na Mzambia, Patric Phiri, Yanga ikinolewa na Mserbia Kostadin Papic aliyemrithi Dusan Kondic ambao wanambiana kuwa lazima timu zao zishinde.
Bila shaka pambano hilo la Jumamosi litakuwa lenye upinzani na litakaloweza kutoa picha ya nani atakayecheka msimu huu wakijiandaa kwenda mapumziko kwa ajili ya duru la pili la ligi hiyo.



No comments:

Post a Comment