Wednesday, October 28, 2009

Simba TMK kuikalia Yanga

Na Badru Kimwaga, Temeke

KATIKA kuhakikisha timu yao inaendelea na wimbi la ushindi kwa asilimia 100, wanachama wa klabu ya Simba wilaya ya Temeke, wanakutana jioni hii kupanga namna ya 'kuiua' Yanga wanayotarajia kukutana nayo katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Jumamosi wiki hii.
Wanakutana kuanzia saa 10 jioni pale kwenye makao yao makuu, Temeke Mwisho jijini Dar es Salaam siku mbili kwenye uwanja mkuu wa Taifa.
Akizungumza na Alasiri jana, Katibu wa matawi ya Simba-Temeke, Husseni Simba, alisema wamelazimika kukutana leo, ili kupanga mikakati na kusoma dua ya maangamizi ya kuiua Yanga siku ya Jumamosi.
Simba, alisema pamoja na kukiamini kikosi chao, lakini wameona ni bora kukutana kuisaidia kwa namna moja au nyingine timu yao kwa vile wanajua mechi za Simba na Yanga huwa zina mambo yake.
"Tunakutana kesho (leo) saa 10 jioni kwa ajili ya kupanga mikakati maalum na 'kuangusha' dua kuiombea mema timu yetu," alisema Simba.
Katibu huyo alisema kikao hicho kitawahusisha viongozi na wanachama wa klabu hiyo matawi ya Temeke na kuwahimiza wenzake kujitokeza mapema kabla ya saa 10 kitakapoanza kikosi hicho ambacho alisema kitajadili mambo mengine kadhaa yanayohusiana na klabu yao na matawi hayo ya Temeke.
Upande wa Yanga wamekuwa wapole katika majigambo tofauti na misimu miwili iliyopita ambapo timu hizo zilipokutana zilitoka sare mara mbili na mechi mbili kila upande ulishinda mechi moja moja.

No comments:

Post a Comment