
London, England
LIVERPOOL leo inashuka dimbani kucheza na Olympique Lyon katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya huku ikiwa na majeruhi kibao, huku pia wakati mgumu ukimuandama kocha Rafael Benitez, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano ya tangu ajiunge na dimba la Anfield.
Benitez anatarajia kuwa na mchezaji aliyemsajili kabla ya kuanza kwa msimu huu wa ligi Alberto Aquilani lakini sehemu ya kiungo ya timu yake itakuwa bila mchezaji tegemeo ambaye ni nahodha wa timu hiyo Steven Gerrard (nyonga) na Albert Riera (misuli nyuma ya mguu) wakati mabeki Martin Kelly (kifundo cha mguu) na Martin Skrtel (misuli) nao pia hawatacheza mchezo huo.
Liverpool imepoteza mechi zake sita kati ya saba zilizopita katika mashindano yote, ikiwemo kipigo cha nyumbani cha bao 2-1 kutoka kwa Lyon wiki mbili zilizopita, na matumaini yake ya kucheza hatua ya mtoano yatakuwa matatani endapo itafungwa huko Stade Gerland.
Lyon inaongoza katika Kundi E ikiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi tatu na endapo itashinda leo itakuwa imejihakikishia nafasi ya kucheza hatua hiyo ya mtoano itakayoshirikisha jumla ya timu 16.
Fiorentina, inayoikaribisha timu iliyopo mkiani ya Debrecen, wako katika nafasi ya pili wakiwa na pointi sita, wakifuatiwa na Liverpool (3), na timu ya Hungary haina pointi hata moja.
Liverpool, bingwa wa Ulaya mara tano, ikiwa na rekodi ya misimu mitatu iliyopita kucheza robo fainali, katika msimu huu imeshindwa kuonyesha cheche zake, na imeshindwa mechi nane kati ya 16 katika mashindano yote.
Mshambuliaji wao wa kutegemewa Fernando Torres, alibadilishwa katika dakika ya 63 licha ya kufunga katika mchezo wa Ligi Kuu ya England Liverpool ilipopokea kipigo cha bao 3-1 huko Fulham alionekana akicheza huku akiwa na maumivu kufuatia kuumia mwezi uliopita alipokuwa akiichezea timu ya taifa ya Hispania.
Mechi nyingine ya Kundi E itazikutanisha Fiorentina na Debrecen wakati katika Kundi F Rubin Kazan itakwaana na Barcelona na Dynamo Kiev itaonyeshan kazi na Inter Milan, wakati katika Kundi G Unirea Urziceni itacheza na Rangers, Sevilla na VfB Stuttgart.
Katiku Kundi H, Arsenal itakuwa mwenyeji wa AZ Alkmaar na Standard Liege itapepetana na Olympiakos Piraeus.
No comments:
Post a Comment