Sunday, July 19, 2009

Dikta afichua siri ya Michael Jackson

LOS ANGELES, Marekani

DAKTARI aliyempa Michael Jackson dawa zilizobadili rangi ya ngozi yake kuwa nyeupe Dk. Arnie Klein, amesema Mfalme wa Pop huyo kamwe hakupenda kuwa mzungu bali ni dawa zilizoidhuru ngozi yake.
"Michael alikuwa mweusi," alisema Dk Klein kuiambia CNN. "Alijivunia asili yake".
Dk Klein alisema kilichompa cha nyota huyo wa pop kuwa mweupe ni 'cream' alizompa kwa ajili ya kutibu ugonjwa wake wa ngozi uitwao Vitiligo, ambao hudhoofisha ngozi na kumtoa mtu madoa-doa.
Mtabibu huyo amesema ugonjwa huo ulimuanza Michael Jackson mkononi na kusambaa kote mwilini isipokuwa usoni.Mwanamama rafiki wa Michael, muigizaji Cicely Tyson, amesema soksi ya mkononi aliyoivaa Michael kwa mara ya kwanza kwenye video ya wimbo wake wa 'Billie Jean' ambayo ikaja kuwa kama alama yake ya kumtambulisha, aliibuni kwa ajili ya kuficha ugonjwa huo wa ngozi mkononi mwake.
"Mimi na Michael tulishea mbunifu wa mitindo kwenye miaka '80, na nilikuwepo pale pamoja nao wakati wakiibuni soksi ile ya mkononi," alisema Cicely kumwambia mtangazaji wa CNN Don Lemon.
"Nililazimika kubebwa mwamvuli," alisema Lee Thomas, ambaye aliandika kitabu cha maisha yake alichokiita 'Kugeuka Mweupe' ambacho kinasimulia mateso ya kimwili na kiakili anayoyapata Mmarekani Mweusi aliyebadilika rangi ya ngozi yake na kuwa mweupe baada ya kupatwa na ugonjwa wa ngozi wa Vitiligo.
Lee, mwandishi wa habari wa televisheni na mshindi wa tuzo ya Emmy wa Detroit, Michigan, aliiambia CNN alikumbwa na hali kama ya Michael Jackson."Nilitokwa na madoa meupe kwenye mkono wangu mmoja, nikalazimika kuvaa soksi ya mkono ili kushika mic wakati nikitangaza," alisema Lee.
Utetezi huu, huenda ukapunguza makali ya habari zilizokuwa zikiandikwa kumuelezea Michael ikiwemo iliyomtaja kama "mvulana 'hendisamu' mweusi aliyegeuka mwanamke mzee aliyechoka wa Kizungu".
Makala za sasa zimemtetea Michael kama mtu ambaye dunia imekuwa "ikimuonea" kwa kumshutumu kwa miaka mingi bila ya kuzingatia historia yake ya maisha ambapo "alinyimwa" nafasi ya kuwa mtoto.
Akiwa na umri wa miaka 10 tu tayari alikuwa ana majukumu ya ki-utuzima ya kutumbuiza katika ratiba ndefu na kuwaliwaza mashabiki, kazi alizozifanya chini ya uangalizi wa karibu wa baba yake Joe Jackson aliyekuwa akimuita "pua kubwa" na hata kumchapa anapokosea katika mazoezi ya bendi.
Ndio maana akaimba katika wimbo wake aliouita 'Childhood' uliokuwemo kwenye albam yake ya 'History': "Mmewahi kuniona nikiwa mtoto? Naitafuta dunia niliyotokea... hakuna mtu anayenielewa. Wanaona kama nafanya vitu vya ajabu.
Kwasababu nafanya utani wakati wote, kama mtoto, lakini hebu niacheni... Watu wanasema siko sawa eti kwasababu napenda mambo ya kitoto.
Ni wakati wangu kufidia maisha ya utoto ambayo sikupitia."Kutokana na kutamani maisha ya utoto, ndio sababu Michael hakutaka hata watoto wake waende shule akiona ndio njia sahihi ya kuwapa muda wa kutosha wa kufurahia kuwa watoto kitu ambacho yeye hakukipata. Lakini upendo wake wa kutaka kucheza na watoto ulimzulia kesi ya kudhalilisha mtoto kimapenzi, ambayo hata hivyo aliishinda.

No comments:

Post a Comment