Tuesday, July 14, 2009

Man City yamtega Adebayor

London, England
MANCHESTER City imesema imeamua kuzama mfukoni kupanga kutoa kiasi cha paundi milioni 25 kumsajili mshambuliaji Emmanuel Adebayor kutoka Arsenal.Kama 'dili' hilo litakamilika, basi nyota huyo kutoka taifa dogo Afrika--Togo, ataingia mkataba wa miaka mitano, na kumwezesha kulamba mshahara wa paundi za Kiingereza 130, 000 kwa wiki (zaidi ya shilingi milioni 260).Uamuzi wa kumnyemelea nyota huyo anayedaiwa 'kuchuja' kiwango Arsenal, umefikiwa baada ya kushindwa kumchomoa Samuel Eto'o kutoka Barcelona.Kocha Mark Hughes anatambua kwanini ni muhimu Adebayor kuziba nafasi ya Eto'o, hivyo anafanya juu chini kuhakikisha anamtwaa.Adebayor alikuwa akitarajia kwenda kujiunga na AC Milan ya Italia, ingawa tayari ana mkataba mrefu wa kucheza Emirates kwa mshahara wa paundi 80,000 kwa wiki.Bosi wa Washika Bunduki wa London, Arsene Wenger huenda akatumia pesa za mauzo ya Adebayor kumleta mshambuliaji wa Morocco Marouane Chamakh anayecheza Bordeaux.Kuondoka kwa Adebayor kunaweza kuwa furaha kwa baadhi ya mashabiki wa Arsenal ambao walikuwa wakimtazama kwa jicho la 'kutofaa' kubaki.Lakini City wanadhani kuwa nyota huyo anaweza kurejesha makali yake kama ilivyokuwa msimu wa mwaka 2007-08, alipoibuka kinara kwa kupachika wavuni mabao 30 akiwa na Gunners.
By Alasiri

No comments:

Post a Comment