Friday, July 31, 2009

Mazoezi Yanga yadoda

Na Jacqueline Massano, Coco Beach
HATIMAYE imekuwa! Zile tetesi za wachezaji wa Yanga huenda wakasusia mazoezi kutokana na kutolipwa mishahara yao ya miezi miwili, zimejidhihirisha leo baada ya wachezaji 10 tu kati ya 30 wa klabu hiyo kujitokeza kufanya mazoezi katika ufukweni wa bahari wa Coco.
Hali hiyo imeonekana mapema asubuhi wakati Alasiri ilipofika katika ufukweni huo kushuhudia mazoezi ya wachezaji hao ambao yanaendeshwa na kocha mkuu wa klabu hiyo, Dusan Kondic na wasaidizi wake.Alasiri iliwashuhudia wachezaji hao tisa wakijifua ufukweni huku watatu kati yao wakiwa wa kigeni na waliobaki ni wazawa.
Wachezaji waliojitokeza ni kipa Obren Curkovic, Nelson Kimati, Idd Mbaga, Shadrack Nsajigwa, John Njoroge, Wisdom Ndlove, Vicent Barnabas, Razack Khalfan, Bakari Mohammed na Kigi Makasi.
Hata hivyo, mwandishi wa gazeti hakuweza kuzungumza na kocha Kondic ila alifanikiwa kuzungumza na mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga, Emmanuel Mpangala ambaye alisema baadhi ya wachezaji wao ni wagonjwa.
Mpangala alisema mazoezi wanaofanya wachezaji hao ni magumu na ndiyo maana baadhi yao wakitoka mazoezini siku inayofuata wanashindwa kurudi tena mazoezini.
"Kwa kweli haya ni mazoezi magumu, ndiyo maana wengine wanashindwa kurudi kwani wakiamka kesho yake wanadai kuumwa," alisema Mpangala.
Aidha, Mpangala licha ya hao wanaosingizia kuumwa, lakini wengine ni wagonjwa wa kikweli kweli akiwemo Hamis Yusuph aliyepigwa na majambazi, Ally Msigwa (shingo), Boniface Ambani (nyonga), Athuman Idd (malaria), Shamte Ally (mguu) na Fred Mbuna (kifundo cha mguu).
Alipoulizwa kuhusiana na wachezaji wengine ambao hawajahudhiria mazoezi, bosi huyo amesema wataonekana kwenye mazoezi ya jioni yanayofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Alasiri ilipomuuliza kama ni kweli wachezaji hao wamegoma kuja uwanjani kwa sababu hawajalipwa mishahara yao, alisema: "Si kweli mbona hata jana walikuwepo."
Hivi karibuni baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo, walikaririwa wakidai kugomea mazoezi hadi hapo uongozi wao utakapowalipa mishahara yao ya miezi miwili.

No comments:

Post a Comment