Thursday, July 30, 2009

Man City yamnasa Kolo

London, England

Manchester City imerejea tena nyumbani kwa Arsenal na kumsajili beki mahiri wa Ivory Coast, Kolo Toure.
Kabla ya Toure, 28, Man City pia ilimsajilia mshambuliaji wa 'The Gunners', Emmanuel Adebayor mwanzoni mwa mwezi huu.
Beki huyo amesaini mkataba wa miaka minne, taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa na kocha Mark Hughes na kutumwa kwenye tovuti ya klabu hiyo ilisema jana.
Hakuna maelezo juu ya ada ya uhamisho iliyowekwa wazi mpaka sasa, lakini udadisi wa vyombo vya habari vya England, unaonyesha kuwa City imetumia paundi milioni 16 kukamilisha usajili.
City sasa iko kwenye mipango ya kujenga safu ya ulinzi baada ya kukamilisha safu ya ushambuliaji msimu huu."Sio siri kwamba kwa kipindi hiki tunajaribu kujenga safu ya ulinzi, na tunadhani kuja kwa Kolo ni kufanikiwa kwa zoezi letu la kujenga timu," alisema Mark Hughes.
Waliwahi kutaka kumsajili beki wa Everton, Joleon Lescott na Chelsea-John Terry, lakini ofa zao zilipigwa chini. Man City ambayo inaonekana pesa si tatizo kwa upande wao, tayari wameshamsajili Roque Santa Cruz wa Paraguay kutoka Blackburn Rovers, Carlos Tevez wa Argentina na Adebayor wa Togo.
Pia kiungo wa England, Gareth Barry naye amejiunga na City akitoka Aston Villa, na kufanya gharama yote ya kuwaleta wanasoka hao kufikia paundi milioni 90.
Kabla ya kujiunga na City, Toure alijiunga na Arsenal akitoka klabu ya Ivory Coast ya Asec Mimosas Februari 2002, na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa FA mwishoni mwa msimu wake wa kwanza mwaka 2003.
Beki huyo alikuwa tegemeo kubwa kwa Arsenal kiasi cha kuonekana chaguo namba moja la kocha Wenger sambamba na Sol Campbell msimu wa 2004, ambapo Arsenal ilicheza mechi nyingi bila kupoteza.

No comments:

Post a Comment