Thursday, July 30, 2009

Wachezaji Yanga walia njaa

Na Mwandishi Wetu, Jijini
WAKATI Ligi Kuu ya Bara ikikaribia kuanza, baadhi ya wachezaji wa klabu ya Yanga, wamesema mpaka sasa hakieleweki kimaisha kutokana na uongozi kutowalipa mshahara yao ya miezi miwili ikiwa ni pamoja na wengine kutomaliziwa fedha zao za usajili.
Akizungumza na Alasiri kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wachezaji wa klabu hiyo (jina tunalo), amesema uongozi kwa sasa unawachukulia 'poa' na kuwaona kama watoto ndiyo maana wanashindwa kuwalipa mishahara yao.
"Siyo mishahara tu, wengine hawajamaliziwa fedha zao za usajili na hadi sasa hatujapewa mgawo wetu wa ubingwa. Lakini sisi ndiyo tunaolalamika ila wenzetu kutoka nchi jirani wako kimya kwa kuwa maisha yao yapo juu," alisema.
Mchezaji huyo amesema wachezaji wanapodai fedha zao uongozi unakuja juu na kuwatishia kuwasimamisha au kuwafukuza kwenye kambi.
"Hivi mtu unawezaje kufanyakazi bila kulipwa mshahara, wenyewe wanafurahia ushindi na wala si kingine. Timu ikivurunda wanakuja juu, lakini sisi tukidai chetu wanakuwa wakali, hivi tutaishi hivi hadi lini," alisema.
Amesema ingekuwa ni wachezaji wa kimataifa ndiyo wanadai fedha zao uongozi ungekwenda kukopa popote pale ili uweze kuwalipa lakini kwa kuwa ni wao wanawapuuza.
Akiongea zaidi kwa niaba ya wenzake, amesema kutokana na hali hiyo ya ukata, mazoezi ya timu hiyo yamedorora kufuatia baadhi ya wachezaji kususia.
"Wengine hawahudhurii hata kwenye mazoezi. Mazoezi bila pesa mkononi? nadhani haiwezekani."
Lakini wakati wachezaji hao wakilalamikia hayo, katibu mkuu wa Yanga, Lucas Kisasa, amegeuka Mbogo alipoulizwa madai hayo ya wachezaji.
Alisema kwa kufoka: "Mtaje mchezaji anayedai pesa Yanga.""Hivi nyie huko ofisini kwenu mmeshalipwa mishahara? Au, mkicheleweshewa mshahara mnajiandika kwenye magazeti? Alihoji na kuongeza: "Mnataka kuleta mgogoro klabuni wakati tumetulia kwa sasa...andikeni habari za jengo letu kukamilika, achana na stori kama hizo za mambo ya mishahara."

No comments:

Post a Comment