Tuesday, July 28, 2009

Mwalala ajuta kuitosa Yanga


Na Badru Kimwaga, Jijini

MSHAMBULIAJI nyota toka Kenya, Ben Mwalala ambaye amerejea Jijini Dar baada ya kushindwa majaribio ya kucheza soka la kulipwa huko China, anajuuta kuikosa klabu yake ya zamani Yanga katika michuano ya Ligi Kuu msimu huu.
Yanga iliamua kumtema Mwalala katika usajili wake msimu huu kwa madai anakwenda kusaka maisha klabu ya Zheijing Green Town FC, huku akiwa amemaliza mkataba wake, hivyo kukosa kucheza ligi nusu ya kwanza ya msimu, hivyo kwa sasa kuangalia ustaarabu mwingine wa kutafuta mahali pa kujihifadhi.
Akizungumza na Alasiri jana usiku, Mwalala alisema kwa sasa yupo Dar baada ya kurejea kwenye majaribio yake, bila kusema lolote kama atarejea nchini kwao Kenya kusaka timu ya kuichezea au ataenda wapi 'kutesti' zali.
"Aah nimesharudi bwana, mambo hayakuwa mazuri na kwa sasa napumzika kwanza, ila tutazungumza vema baadae," Mwalala alisema kwa ufupi alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi.
Hata hivyo kukwama kwa Mwalala kupata timu nje ya nchi imekuwa kama bahati mbaya kwake kwani klabu aliyokuwa akiichezea Yanga ilishamfungia milango katika usajili mpya kwa kumtema kufuatia kumaliza nae mkataba.
Kocha Mkuu wa Yanga, Dusan Kondic alinukuliwa kuwa, Mkenya huyo aisahau Yanga kwa sasa hadi utakapofika wakati wa usajili mdogo kuona kama wamsajili au la kulingana na kiwango atakachokuwa nacho.
Mwalala, ameachwa na Yanga akiwa na shujaa aliyeisaidia timu hiyo kufuta uteja wa miaka nane mfululizo kwa Simba kwa bao lake lililoipa ushindi wa bao 1-0 na pia kufunga bao jingine lililoipa Yanga sare ya mabao 2-2 kwa watani zao hao katika mechi ya pili ya ligi kuu msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment