Friday, July 17, 2009

Mr Tabasamu anayetaka kutoka na kila mtu


Mr Tabasamu anayetaka kutoka na kila mtu
Na Amour Hassan
RAPA wa Bongofleva Mr Blue anafahamu kuwa ni yeye 'mkubwa sana' katika gemu hii ya kizazi kipya.
Anafahamu kuwa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati jina lake linazungumzika vizuri.
Lakini pia anafahamu kuwa hajafika anakoelekea."Unaweza ukajiamini kuwa ni 'mkubwa' katika gemu hapa nyumbani halafu ukasahau kuwa wewe ni mtoto mchanga kabisa barani Afrika na kiwango cha dunia ni sawa na hujazaliwa kabisa," alisema rapa huyo alipozungumza na blogu ya jirushe-jiachie.
Blue alisema anafahamu kuwa kwa ukanda huu wa Afrika Masharariki na Kati ameshakubalika vyema lakini ana changamoto kubwa ya kufungua mipaka zaidi.
"Haina maana kufanya muziki halafu ukaishia kutamba nyumbani kwako tu. Ni sawa na kuimba bafuni wakati wa kuoga, wnaokusikia ni watu wa ndani kwenu tu na ni rahisi kukusifu hata kwa uongo. Changamoto ya kweli ni kufanya kitu kizuri kitakachoweza kukubalika nje. Watu wa nje wakikwambia kuwa unaweza hapo ndipo unapoweza kuamini kuwa unaweza," alisema.
Baada ya kuumaliza mwaka 2008 kwa kishindo kupitia wimbo wake wa 'Tabasamu' unaobamba kila kona kuanzia katika vituo vya radio, televisheni na klabu za burudani, Mr Blue amesema anataka kuendelea na kasi hiyo mwaka huu.

KUTOKA NA KILA MTU
Mistari ya hatari, kiitikio cha ukweli na 'biti' la kushiba vimetoa bonge la songi linalotosha kumfanya aliyenuna atabasamu.Na bila ya shaka, video ya kupania iliyofanywa na studio ya Kallaghe Pictures, imechangia umaarufu wa wimbo huo na, infact, imeitoa vyema kampuni hiyo ya video na kuifanya izungumziwe katika matawi ya kampuni inayotawala kwa muda mrefu ya Visual Lab.
Muunganiko wa vitu vikubwa katika maandalizi ya wimbo huo, umetosha kumrejesha vyema Blue ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu, ukiacha nyimbo mbili-tatu za kushirikishwa na wasanii wenzake.
Lakini katika marejeo yake ya 2009, Blue anataka kuufuta ukimya ambao ameukiri katika mashairi ya 'Tabasamu' pale aliporap: "Mr Blue vipi, mbona sikusikii tena, mbona sikusikii ukinena, mbona sikusikii ukisema."
Rapa huyo amesema amedhamiria kufanya mambo makubwa mwaka huu baada ya kuuanza vyema kwa wimbo wake huo aliofungia mwaka.
Baada ya mashabiki wa kizazi kipya kusikia kiitikio cha ukweli kutoka kwa msanii Steve aliyemtambulisha kwenye gemu kupitia wimbo huo wa 'Tabasamu', ambao chipukizi huyo amenata na 'biti' kama 'supastaa' mzoefu, Mr Blue anasema mwaka huu anataka kutoka na kila mtu.
"Natamani kila mtu atoke. Natamani kila mtu afanikiwe katika kile anachokifanya. Natamani kila mtu awe na maisha bora, natamani kila amtu awe na raha ya maisha," alisema. "Mmemshamsikia Steve, na sasa mwaka huu kuna wakali wengine wapya kibao wanakuja. Sitaki kukutajia kwa sasa kwa sababu kuongea sio staili yetu ya maisha, sisi ni vitendo tu, tunatoa 'pini' mashabiki wenyewe wanatuletea taarifa za mitaani huko watu wanavyopagawa."
Alisema kupitia mdhamini wake mpya Tippo wa Zizzou Fashion, ambaye pia anamdhamini rapa wa East Zoo Ngwair, amesema anatarajia kuachia single nyingine mwezi Machi.
"Nazipa muda nyimbo zangu kama ambavyo nimekuwa nikitoa miaka yote. Najua kwa kipindi hiki chote hadi Machi mashabiki watakuwa wanaendelea 'kutabasamu' tu," alisema.
Alisema hataji jina na wimbo kwa sababu maalum lakini umefanywa na aliyekuwa prodyuza wake wa muda mrefu marehemu Roy Bukuku wa G2 Records kabla hajafariki.
"Ni kwa ajili ya kumbukumbu ya prodyuza wangu," alisema rapa huyo ambaye jina lake la kuzaliwa ni Herry Samir.
Nyota huyo ambaye nyimbo zake zimekuwa zikifananishwa na maisha yake, alijikuta akiitwa Mr Blue kufuatia wimbo wake wa kwanza katika gemu ulioitwa 'Mr Blue'.
Wimbo wake mwingine wa 'Mapozi' ulimfanya pia ajulikane kama 'Bwana Mapozi'.
Lakini uwezo wake mkubwa katika gemu pia ulishuhudia rapa huyo akifunika hata katika nyimbo alizoshirikishwa kama 'Mbona' wa PNC, 'Joanita' wa Pingu na Deso, 'Nilikataa' wa Top Band akiwa na TID na Q-Chillah na 'Nipe Mkono' alioshirikishwa na Mrembo wa Milenia Miss Tanzania 2000 Jacqueline Ntuyabaliwe a.k.a K-Lynn.

No comments:

Post a Comment