Thursday, October 29, 2009

Makomandoo Simba, Yanga kukipatapata

Na Jimmy Charles
SHIRIKISHO la soka nchini (TFF), limewachimba mkwara makomandoo wa timu za Yanga na Simba kuachana na mawazo ya kutaka kuingia bure kwenye mchezo wa watani hao uliopangwa kuchezwa kesho kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini jana, Afisa Habari wa TFF, Frolian Kaijage alisema kuwa TFF kwa kushirikiana na jeshi la Polisi wamejiandaa kuhakikisha hakuna mtu anayeingia bure.
Kaijage alieleza kuwa endapo mtu yeyote atakuwa na malengo hayo atakuwa amechelewa kwani hakutakuwa na nafasi ya bure kwa watu wasiokuwa na kazi maalum ndani ya uwanja huo.
"TFF imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila shabiki mwenye nia ya kutaka kushuhudia mchezo huo analipa kiingilio na kama yupo komandoo mwenye nia hiyo ni vema akafuta mawazo yake hayo,"alisema Kaijage.
Aliongeza kuwa mbali ya kutoa tahadhari kwa watu wenye kutaka kuingia bure lakini pia amewatahadharisha watu wenye nia ya kughushi tiketi ama kununua kwa wingi na kuziuza tena kuachana na mpango huo.
Kaijage alieleza kuwa TFF, kamati inayosimamia uwanja huo pamoja na jeshi la Polisi
wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanawadhibiti watu watakaokuwa na nia ya kutaka kujiingizia kipato kwa njia ya magendo.
Alitoa wito kwa mashabiki wa kweli wa timu hizo kujinunulia tiketi zao kweney maeneo yaliyopangwa ili kuepuka usumbufu.

No comments:

Post a Comment