Thursday, October 29, 2009

Banana kushiriki Wahapahapa

Na Jimmy Charles

MWANAMUZIKI wa muziki wa kizazi kipya Banana Zoro anatarajia kushiriki kwenye tamasha kubwa la uzinduzi wa albamu ya 'Wahapahap'a inayotoa elimu juu ya kuwaepusha vijana na ngono zembe litakalofanyika Novemba 6, jijini Mbeya.
Afisa kutoka wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya Habari na Ukimwi, Benard Fimbo alisema lengo la tamasha hilo ni kutoa elimu kwa vijana juu ya kujiepusha na ngono ambazo zinaweza kuwasababishia kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Fimbo alisema katika miaka ya karibuni kwa kiasi kikubwa wasanii, wanahabari na mashirika binafsi yanayojihusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi wamesaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo tofauti na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Kwa upande wake mkurugenzi wa waandaaji wa tamasha hilo Deo Mwanansabi alisema mbali ya Banana kutoa burudani kwenye tamasha hilo pia kutakuwa na wanamuziki wengine wa hapa nchini.
Aliwataja wanamuziki hao kuwa ni Enika, bendi kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park na bendi ya Wahapahapa.
Mwanansabi alieleza kuwa mara baada ya tamasha la jijini Mbeya kumalizika wasanii hao watafunga safari hadi mkoani Iringa kwa ajili ya kufanya tamasha jingine lenye malengo ya kuwaelimisha vijana juu ya gonjwa hilo, ambapo hakutakuwa na kiingilio katika matamasha yote hayo.

No comments:

Post a Comment