Tuesday, October 27, 2009

Maximo atangaza kikosi cha Stars

Na Mwandishi Wetu, Jijini

KOCHA Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo amewajumuisha kwa mara ya kwanza kwenye kikosi chake kinachotarajia kumenyana na timu ya taifa ya Misri Novemba 5 wachezaji watatu, ambapo mmoja kati yao anacheza soka la kulipwa nchini Msumbiji.
Mbali ya kuwaongeza wachezaji hao lakini pia Maximo amewarejesha kundini wachezaji sita ambao hawakuwepo kwenye kikosi chake kilichomenyana na timu ya taifa ya Rwanda mapema mwaka huu.
Maximo pia ameendelea kuwaita wachezaji wake wa kimataifa wanaocheza soka la kulipwa nchini Ulaya Henry Joseph, Nizar Khalfan na Nadir Haroub kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake.
Wachezaji wapya walioitwa na Maximo ni kipa Mohamed Mwalami anayecheza soka la kulipwa nchini Msumbiji kwenye klabu ya Ferroviaro,Agrey Morris wa Azam Fc na Said Ahmed wa Moro United.
Wachezaji waliorejeshwa kwenye kikosi hicho ni Ally Mustapha, David Naftari, Stephen Mwasika, Ibrahim Mwaipopo, Shabani Nditi na Abdullahim Amour.
Akitangaza kikosi hicho kwa niaba ya Maximo kocha mkuu wa timu za taifa za vijana, Rodrigo Stocler alisema kuwa uteuzi wa wachezaji hao umezingatia nidhamu, uwezo, umri na ushirikiano wao kwa wenzao.
Stocler alisema kikosi cha Stars kitakuwa na jumla ya wachezaji 36, ambapo kati yao wachezaji watano watatoka kweney timu za taifa za vijana.
Kikosi kamili cha Stars kinaundwa na makipa, Ally Mustapha,Shaban Dihile, Shabani Kado na Mohamed Mwalami,walinzi ni Agrey Morris, Shadrack Nsajigwa, Erasto Nyoni, Davis Naftari, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Salum Swedi, Juma Jabu na Stephen Mwasika.
Viungo ni Nurdin Bakari, Ibrahim Mwaipopo, Juma Nyoso, Shaban Nditi, Abdulahim Amour, Henry Joseph, Rashid Gumbo, Mwinyi Kazimoto,Kigi Makasi, Nizar Khalfan na Said Ahmed,washambuliaji ni Mrisho Ngassa, Mwana Sammata, Musa Mgosi, Danny Mrwanda,John Boko, Jerry Tegete na Zahoro Pazi.
Wachezaji kutoka timu za vijana ni Amani Kiata,Yusuph Soka, Himid Mao, Thomas Emmanuel wote kutoka timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 na Thabit kutoka timu ya vijana wenye umri wa miaka 17.

No comments:

Post a Comment