Tuesday, October 27, 2009

Yanga Chini ya Ulinzi

Na Jacqueline Massano, Jijini

ZIKIWA zimebaki siku mbili na masaa kadhaa, jiji la Dar es Salaam kutekwa na shamrashamra za mechi ya miamba ya soka nchini, uongozi wa klabu ya Yanga umewaweka wachezaji wake kwenye ulinzi mkali.
Yanga ambayo inajiandaa na mechi dhidi ya Simba itakayofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, imeweka kambi Jangwani makao makuu ya klabu yao iliopo mtaa wa Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Habari zilizoifikia Alasiri mapema leo na kuthibitishwa na mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, ni kwamba wachezaji hao hawaruhusiwi kukutana na mtu wa aina yeyote anayekwenda kambini hapo kwa lengo la kuwasalimia.
Mchezaji huyo amesema kutokana na mechi hiyo kwa sasa wachezaji hawaruhusiwi kutoka nje ya jengo hilo kutokana na ulinzi ambao umewekwa na wanachama wa klabu hiyo.
Amesema kutoka kwao nje ni kwenda kufanya mazoezi ambapo wanafanyia kwenye uwanja wao na kuingia ndani kwa ajili ya kupumzika.
"Ukionekana tu na hao wanachama unatoka nje au mtu akija hapa kambini ni balaa, yaani unazua balaa, si unajua wanachama wa Yanga walivyo? Hapa walipo wamelizunguka jengo letu."
"Si unajua tena maandalizi ndiyo yameanza, na sisi hatuendi kuweka kambi popote ni hapa hapa Jangwani, na ndiyo maana wanachama wamejaa, wengine wanalala hapa hapa nje. Hivyo sisi huwa tunakaa juu ghorofani tunawaangalia tu," alisema mchezaji huyo
Alipoulizwa kuhusu simu zao za mkononi alisema hajui kama wataendelea kuwa nazo au watanyang'anywa kama wanavyofanyiwa kwenye mechi za miaka mingine wanapokutana na watani zao hao wa Jadi.
"Kwa kweli simu sijui, maana hawa hawatabiriki, wanaweza kutunyang'anya au kutuachia," alisema

No comments:

Post a Comment