Thursday, October 29, 2009

Simba yaipa Yanga maneno makali

Na Jacqueline Massano

WAKATI jobo la Yanga likitua Zanzibar jana na kutangaza kutembelea mazoezi ya watani zao wa Jadi, Simba, uongozi wa wekundu hao wa Msimbazi umeng'aka na kuwataka wana-yanga hao kutothubutu kufanya hivyo.
Baadhi ya wanachama hao wa Yanga wakiandamana na mwenyekiti wao, waliwasili Zanzibar jana kwa lengo la kwenda kufuata baraka kutoka kwa wazee na wanachama wengine waliopo huko.
Akizungumza mapema leo, meneja wa Simba, Innocent Njovu amesema kama Yanga wameenda Zanzibar kwa mambo yao na hawatajihusisha kwa namna yoyote na ziara yao.
Kauli hiyo, imekuja baada ya Yanga kudai kuwa leo inatarajia kutembelea mazoezi ya Simba yanayofanyika Mbweni, Zanzibar.
"Kama Yanga inakuja kwa ajili ya mambo yao, hatuna shida nao lakini kama safari yao inalenga kuvuruga kambi yetu, naomba niseme wazi kuha hatutakuwa tayari," alisema.
"Viongozi na wanachama wengine wa Yanga watakaokuja kwenye kambi yetu, wajiandae kujuta. Hatujahusika kwa namna yoyote na maandalizi yao, lakini wao wanaona kwetu ndio sehemu ya kufanya mchezo," alisema zaidi.
"Tunajua hata Yanga huku Zanzibar ina mashabiki wengi lakini inatakiwa kuzungumza na mashabiki wao, na wala si kutuingilia sisi," aliongeza.
Homa ya pambano hilo, limezidi kupata kila dakika kutokana na timu hizo mbili kuanza kuhisi kuhujimiwa.

No comments:

Post a Comment