Thursday, October 29, 2009

Makinda wa Arsenal waizima Liverpool

LONDON, England

CHIPUKIZI wa Arsenal jana waliifanyia kweli Liverpool baada ya kuichapa mabao 2-1 katika mechi Kombe la Ligi, matokeo ambayo yanaivusha timu hiyo hatua ya robo fainali.
Katika mechi nyingine, Manchester City waliwachapa mabingwa wa daraja la pili, Scunthorpe United mabao 5-1, na kuingia hatua ya nane bora, huku Chelsea 'wakiiadabisha' Bolton Wanderers na kipigo cha mabao 4-0 kwenye uwanja wa Stamford Bridge.
washindi hao wanaungana na mabingwa watetezi Manchester United, washindi wa pili wa mwaka jana Tottenham Hotspur, Blackburn Rovers, Portsmouth na Aston Villa katika mechi za robo fainali ambazo zitazikutanisha timu zinazocheza Ligi Kuu ya England Jumamosi wiki hii.
Kocha wa Arsenal Arsene Wenger, akiiongoza timu yake kucheza mechi ya 750, aliweka imani kubwa kwa vijana wake na walifanya vizuri kwenye mechi.
Fran Merida, 19, kiungo wa kimataifa kutoka Hispania alikuwa wa kwanza kufunga bao kwa Arsenal baada ya dakika 19 tangu kuanza kwa mchezo, kabla ya Liverpool kusawazisha kwa bao safi la Emiliano Insua, likiwa la kwanza kwake katika mechi sita.
Liverpool, nayo ilijaza vijana kwenye mechi hiyo na kuonyesha kandanda safi lakini walishindwa kupata ushindi dhidi ya Arsenal katika kipindi cha miaka tisa.
Bao lililoitosa Liverpool lilifungwa na kwa shuti kali la mguu wa kushoto katika dakika ya 50 na mchezaji Niklas Bendtner.
"Kulikuwa na tofauti ndogo sana kati ya timu hizi," alisema kocha wa Arsenal Arsene Wenger wakati akiongea na Sky Sports.
"Kikosi chetu kilikuwa hatari, na chao pia kilikuwa hivyo, lakini nadhani kuna wachezaji wazuri na wenye uwezo kushinda taji msimu huu."
Kocha wa Liverpool Rafa Benitez, aliyefanya mabadiliko tisa kutoka kwenye kikosi kilichoifunga Manchester United Jumapili iliyopita aliipongeza timu yake na kusema kipigo hicho hakiusiana na ushindi wa Jumapili dhidi ya United.
"Ndio, hatuna raha kupoteza mchezo lakini kufungwa kwetu si hakuhusiani na ushindi wa United. Timu ilikuwa nyingine kabisa kwa sababu mashindano ni ya aina nyingine pia."
Manchester City, ambao hawajawahi kushinda kombe kubwa tangu mwaka 1976, ilikuwa ya kwanza kufunga bao kupitia kwa Stephen Ireland baada ya dakika tatu tangu kuanza kwa mchezo, kabla ya Jonathan Forte kusawazisha katika dakika ya 26.
City walirejea tena mbele kwa bao la pili kupitia kwa Roque Santa Cruz, likiwa bao lake la kwanza tangu ajiunge kutoka Blackburn Rovers.Mabao mengine yalifungwa Joleon Lescott, Carlos Tevez na Michael Johnson.
Chelsea nayo iliipeleka puta Bolton kwenye uwanja wa Stamford Bridge, huku Salomon Kalou, Florent Malouda, Deco na Didier Drogba wakiwa mashujaa baada ya kila mmoja kufunga bao.

No comments:

Post a Comment