Wednesday, October 28, 2009

Vodacom yamwaga tiketi kwa mashabiki

Na Jimmy Charles

KAMPUNI ya simu za mikononi ya Vodacom imetoa tiketi 20 za viti maalum kwa mashabiki 10 wa timu za Simba na Yanga kwa ajili ya kushuhudia mchezo utakaowakutanisha watani hao wa jadi keshokutwa.
Washindi hao kila mmoja atapatiwa tiketi mbili pamoja na kulipiwa gharama za usafiri kutoka maeneo wanayoishi pamoja na kulipiwa gharama za malazi na chakula kwa muda wa siku mbili.
Akiwatangaza washindi hao meneja matukio na promosheni wa Vodacom, Rukia Mtinwa alisema kuwa washindi hao kila mmoja anatakiwa kuja na jamaa yake mmoja, ambapo wote watalipiwa gharama zote muhimu.
Mtingwa aliwataja washindi hao kuwa ni Mary Kaduguda, Thabit Kaizer, Adam Chonya, Jingu Mseya na Rajabu Mhamila wote wakiwa ni mashabiki wa Simba.
Mashabiki wa Yanga walioshinda tiketi hizo pamoja na jezi za timu yao hiyo ni Muhidi Sufian, Issa K, Fulgence Ramadhani, Idrisa Mohamed na Maimbo Mkeia.
Wakati huo huo benki ya Stanbic imemchagua mshindi wa mwezi wa droo yake ya kwenda nchini Angola kushuhudia fainali za mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini humo, ambapo Meriso Suzan mkazi wa Arusha ameibuka kidedea.

No comments:

Post a Comment