Wednesday, November 25, 2009

Ambani kujaribiwa St. George

Na Jacqueline Massano

MSHAMBULIAJI Mkenya aliyetemwa Yanga katika usajili wa dirisha dogo, Boniface Ambani, ameitwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mserbia Milutin Sredejovic 'Micho' ambaye kwa sasa anaifundisha St. George ya Ethiopia kwa ajili ya kufanya majaribio.
Ambani ametemwa na klabu hiyo kwa madai ya kushuka kiwango na kushindwa kumshawishi kocha mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic.
Akizungumza na blog hii kwa njia ya mtandao, Micho alisema tayari amefanya mazungumzo na mchezaji huyo ili aweze kufanya majaribio kwenye timu yake.
"Ngoja aje nimuone maana siwezi kuzungumza na mtu bila hata kujua kiwango chake, akija hapa nitamfanyia majaribio na kuangalia kiwango chake na akinifurahisha nitamsajili kwa kipindi hiki," alisema Micho.
Micho alisema ikiwa kiwango cha mchezaji huyo hakitamridhisha basi atamuacha ili aweze kutafuta timu nyingine ya kuichezea.
"Huku St. George kwanza kabisa tunazingatia nidhamu na bidii ya mchezaji akiwa uwanjani, na kiwango chake kikiwa hakifurahishi tunaachana naye," alisema.
Hata hivyo, Alasiri ilipowasiliana na Ambani kutoka Kenya, alikiri kufanya mazungumzo na kocha huyo na kudai kwa sasa anasubiri kuitwa.
"Nilikuwa na safari ya kwenda kufanya majaribio kwenye timu nyingine, lakini mara baada ya kupokea simu ya Micho ikinihitaji kwenda Ethiopia, nimesitisha mishemishe zangu, na sasa nasubiri mipango ya kuondoka kwangu," alisema Ambani.
Ambani mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu ijayo kwa ajili ya kufuatilia malipo yake ya kuvunjiwa mkataba na klabu yake ya zamani, Yanga.

No comments:

Post a Comment