Wednesday, November 25, 2009

Man United, Chelsea kibaruani leo

MILAN, Italia

TIMU mbili za Uingereza, Manchester United 'Red Devils' na Chelsea 'The Blues' ambazo tayari zimefuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, leo zina kazi nyepesi zikiwa zinaelekea ukingoni mwa mechi za hatua ya makundi pale zitakaposhuka katika viwanja tofauti.
Man United itakuwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford itakapoikaribisha Besiktas katika mechi ya kundi B ya michuano hiyo.
Wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Uingereza wakiwa uwanja wa nyumbani, washindani wao katika ligi hiyo Chelsea wakipepetana na mahasimu wao wa Ureno, Porto.
Hata hivyo, mechi nyingine kali itakuwa dhidi ya mabingwa mara saba Ulaya, AC Milan ambao kwa sasa kiungo wao Ronaldinho akiwa ameimarika itakaposaka nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano itakapoikaribisha Olympique Marseille.
Milan inayoshiriki Serie A inaongoza katika msimamo wa Kundi C, ikiwa pointi sawa na Real Madrid, lakini timu hiyo ya Ufaransa iko pointi moja nyuma ikiwa imebakiza michezo miwili kabla ya kufungwa kwa mechi hizo za makundi.
Mbali na mchezo huo, pia APOEL Nicosia leo ina kazi nyingine ya kupepetana na Atletico Madrid katika mechi ya kundi D.
VfL Wolfsburg inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi B ikiwa na pointi saba, itakuwa mgeni wa CSKA Moscow katika mchezo mwingine wa kundi hilo utakaozikutanisha timu mbili zenye uwezo wa kucheza hatua inayofuata.
Katika mechi za kundi A, Girondins Bordeaux itakuwa mwenyeji wa Juventus, Bayern Munich iliyokalia kuti kavu itaikaribisha Maccabi Haifa.

No comments:

Post a Comment