Wednesday, November 11, 2009

Kipa Ujerumani agongwa na treni

BERLIN, Ujerumani
KIPA wa timu ya taifa ya Ujerumani na Hanover 96, Robert Enke, amefariki papo hapo baada ya kugongwa na treni iendayo kwa kasi, tukio linaloonekana kama la kupanga kujiua mwenyewe, taarifa ya polisi ilisema jana usiku.
"Ushahidi wa awali unaonyesha alipanga kujiua, "afisa habari mdogo wa polisi, Lower Saxony alisema wakati akiongea na Reuters, kabla ya kuongeza kwa kusema mwili wa kipa huyo ulikutwa karibu na makutano ya reli katika mji wa Neustadt, Hanover.
"Majira ya jioni, aligongwa na treni ya kasi inayosafiri kati ya mji wa Hamburg na Bremen," msemaji mwingine wa polisi, Stefan Wittke alisema.
"Treni ilikuwa kwenye kasi ya kilomita 160-kwa saa." Wachezaji na marafiki zake, na mshauri Joerg Neblung waliwaambia waandishi wa habari "Nawedha kuthibitisha tukio hili ni la kujiua mwenyewe.
Aliamua kujiua mwenyewe kwa kujiingiza kwenye njia ya treni muda mfupi kabla ya saa 12:00 jioni (muda wa ujerumani).Utafanyika mkutano na waandishi wa habari kesho (leo) ili kutoa taarifa zaidi."
Enke, 32, amecheza mechi za kimataifa nane akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani, na alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao wangeitwa kwenye kikosi cha Ujerumani kwa ajili ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Afrika Kusini.
Taarifa za kifo chake zimelishitua Shirikisho la Soka Ujerumani (DFB).
"Timu ya Ujerumani imeshitushwa na msiba huu mzito," ilisema taarifa ya DFB.
"Kocha wa timu ya taifa, Joachim Loew na Oliver Bierhoff, wote wameshtushwa na kifo hiki," ilisema zaidi taarifa hiyo.
Enke, aliwahi kucheza soka katika nchi za Hispania, Ureno na Uturuki kabla ya kusaini ligi ya Ujerumani 'Bundesliga' akiwa na timu ya Hanover mwaka 2004.

No comments:

Post a Comment