Thursday, November 12, 2009

Wachezaji wamchanganya Papic

Na Jacqueline Massano
UONGOZI na kocha mkuu wa klabu ya Yanga, hadi sasa hawajui nani watamuongeza katika usajili wa dirisha dogo la Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia wachezaji wote walioanza majaribio na klabu hiyo kufanya vizuri.
Isitoshe, bado haijafahamika mchezaji gani atakayepunguzwa kwenye kikosi hicho kutokana na wachezaji wote kuwa na mkataba na klabu hiyo isipokuwa Mike Barasa ambaye mkataba wake umemalizika.
Yanga ina nafasi moja tu ya kuongeza mchezaji iwapo itashindwa kukubaliana na mshambuliaji wa kimataifa, Barasa ili aweze kuongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo.
Habari zilizopatikana mapema leo ni kwamba, hadi sasa kocha wa timu hiyo, Kostadin Papic hajajua ni mchezaji gani amsajili kwenye timu yake kwa sababu bado anamuhitaji Barasa na pia amevutiwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Salvatory Edward
.Habari zinadai kuwa baadhi ya viongozi wameonyesha nia ya kutaka kumsajili tena aliyekuwa kipa namba moja wa klabu hiyo, Ivo Mapunda ambaye alikuwa anaichezea St. George ya Ethiopia.
"Haya ni maajabu, maana hadi sasa haijajulikana nani anapunguzwa na nani anaongezwa, kwani kocha naye anamtaka Barasa aendelee kuitumikia klabu hiyo. Uongozi pia unamtaka Ivo," alisema mtoa habari ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.
Yanga iko kwenye mchakato wa usajili mdogo ingawa hadi sasa haina nafasi ya kuongeza mchezaji, vinginevyo kama watapunguza wachezaji kwenye kikosi chao.

No comments:

Post a Comment