Wednesday, November 25, 2009

Liverpool 'out', Arsenal yapeta

LONDON, England
MABINGWA mara tano Liverpool jana walijikuta wakitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa kwenye hatua ya makundi pamoja na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Debrecen huku Fiorentina na Arsenal wakifuzu kuingia kwenye 16 bora.
Mabingwa watetezi Barcelona walifufua kampeni yao kwa ushindi mzuri wa mabao 2-0 dhidi ya Inter Milan kwenye mechi iliyokuwa na mvuto zaidi usiku wa jana, wakijipatia mabao yao ndani ya dakika 26 za mwanzo kupitia kwa Gerard Pique na Pedro.
Arsenal wametinga hatua ya 16 bora kwa msimu wa 10 mfululizo kufuatia ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Standard Liege.
Fiorentina walifuzu baada ya kujipatia ushindi wa bao 1-0 kwa njia ya mchomo wa adhabu uliopigwa na Mperu Juan Vargas dhidi ya Olympique Lyon, ambao tayari wameshafuzu, na kujiunga na Girondins Bordeaux, Manchester United, Chelsea, Porto na Sevilla kwenye hatua inayofuata.
Ushindi wa Waitalia hao pia ulihitimisha ndoto za Liverpool za kufuzu kutoka kwenye Kundi E.
"Tumekuwa wazuri sana (kwenye miaka ya hivi karibuni) kwenye Ligi ya Mabingwa, sasa watu wanadhani itakuwa hivyo hivyo kila mwaka," meneja Rafa Benitez wa Liverpool aliwaeleza wanahabari.
Kikosi cha Benitez kiliwasili Hungary kikijua majaliwa yao kwa kiasi kikubwa hayakuwa mikononi mwao na goli la ushindi lililofungwa katika dakika ya nne na mshambuliaji Ngog, ambalo liliwafanya Debrecen wanaocheza michuano hiyo kwa mara ya kwanza kuchapwa mechi tano mfululizo, halikuweza kusaidia chochote.
Ushindi wa Fiorentina umewafanya waongoze kundi wakiwa na pointi 12, mbili juu ya Lyon huku Liverpool wakiwa nyuma zaidi kwa pointi tatu.
Hata kama mabingwa hao wa mara tano watalingana na Lyon, kikosi hicho cha Ufaransa kitafuzu kutokana na kuwa na rekodi nzuri walipokutana baina yao. Mshambuliaji wa zamani wa Barcelona Samuel Eto'o alipewa mapokezi mazuri aliporudi Nou Camp akiwa na klabu yake mpya ya Inter lakini mambo hayakuwa mazuri kwake.
Japokuwa Barcelona walikuwa wameshashinda mechi tatu tu kati ya saba zilizopita nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa, walikuwa hawajawahi kufungwa kwenye mechi sita dhidi ya timu za Italia.
Pamoja na kutokuwa na majeruhi Lionel Messi na Zlatan Ibrahimovic, Barcelona walikuwa wazuri sana kuwalinganisha na Inter.
Pique alifunga bao la kwanza kufuatia kona ya dakika ya 10 kabla ya Pedro kumaliza kazi kwa kupachika bao la pili dakika 16 baadaye.
Ushindi huo umewafanya Barcelona kuongoza Kundi F wakiwa na pointi nane, mbili mbele ya kikosi cha Jose Mourinho na walio nafasi ya tatu mabingwa wa Russia, Rubin Kazan, ambao walilazimishwa sare ya bila kufungana nyumbani na Dynamo Kiev.
Kiev wanashikilia mkia wakiwa na pointi tano lakini bado pia wanaweza kufuzu kwenye kundi hilo.
Barcelona watakuwa wageni wa mabingwa hao wa Ukraine kwenye mechi za mzunguko wa mwisho mwezi ujao huku Inter wakiwakaribisha Rubin.
"Tumeonyesha kwamba yeyote anayeingia kwenye kikosi hiki analeta kitu kipya," alisema Daniel Alves wa Barcelona akimaanisha watu waliochukuwa nafasi za Ibrahimovic na Messi.
Arsenal hawakuwa na kazi kubwa kuendeleza rekodi yao ya kutofungwa nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu za nje kufikia mechi 29.
Vijana hao wa London walijipatia mabao kupitia kwa Samir Nasri kwenye dakika ya 35 kabla ya Mbrazil Denilson kufunga kwa shuti la kutokea umbali wa mita 30 kwenye dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza.
Ushindi huo umewahakikishia Arsenal nafasi ya kwanza kwenye Kundi H wakiongoza kwa tofauti ya pointi sita mbele ya Olympiakos waliotoka sare ya 0-0 dhidi ya AZ Alkmaar.
Unirea Urziceni walizidi kujipalilia nafasi zao kwenye Kundi G kwa kuwafunga Sevilla, ambao tayari wameshafuzu, kwa bao 1-0 baada ya Ivica Dragutinovic kujifunga mwenyewe kwa kichwa muda mfupi kabla ya mapumziko.
Mabingwa hao wa Romania wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi nane, mbili mbele ya VfB Stuttgart ambao waliwafunga Rangers mabao 2-0 kuwapa Wascotland hao kipigo chao cha tatu mfululizo kwenye kundi hilo.

No comments:

Post a Comment