Tuesday, November 24, 2009

Simba kwafukuta

Na Badru Kimwaga
WAKATI vuguvugu la uchaguzi mkuu Simba likizidi kushika kasi, limeibuka kundi la wanachama wa klabu hiyo na kutishia kuwafungia nje viongozi wao wa sasa ifikapo Desemba 4 mwaka huu.
Wanachama hao wakiongozwa na Issa Said Ruchaki 'Masharubu' mwenye kadi namba 2511, alisema wamedhamiria kufanya hivyo kutokana na ukweli mwisho wa uongozi huo unatakiwa kuhitimishwa Desemba 3.
Masharubu alisema watachukua hatua hiyo baada ya kuona viongozi hao wanataka kuwapiga 'changa la macho' juu ya uchaguzi mkuu, ambao unatarajiwa kutangazwa rasmi Jumamosi hii.
"Mkataba wetu na viongozi wa sasa wa Simba ni mwisho Desemba 3, baada ya hapo tutaifunga klabu na kuikabidhi timu kwa meneja Inoccent Njovu pamoja na manahodha Nico Nyagawa na Juma Kaseja chini ya Baraza la Udhamini la Wazee," alisema Masharubu.
Masharubu alisema anawakilisha kundi la wanachama zaidi ya 20, na kudai hawana tatizo na mtu yeyote bali wanataka klabu iwe chini ya watu hao hadi watakapopatikana viongozi wapya.
Aidha, alisema wanachama wa Simba wanawapa pongezi mwenyekiti Hassani Dalali na Mhazini Mkuu, Chano Almasi kwa kuendelea kugawa kadi za uanachama wa klabu hiyo bila ukomo kama walivyokuwa wamekubaliana.
"Hili la utoaji wa kadi hadi leo ni suala la kupongezwa kwani linafanya wawili hao wajiweke karibu na wanachama, ila msimamo wetu ni kwamba Desemba 3 ndio mwisho wa kukanyanga klabuni hadi viongozi wapya wapatikane."

No comments:

Post a Comment