
RONNIE Whelan jana alimshukia vikali kocha wa Liverpool Rafa Benitez na kusema siku zake za kubaki kwenye klabu hiyo zinahesabika.
Whelan alimponda vibaya Benitez kufuatia maamuzi ya kocha huyo kumpumzisha Fernando Torres katika mechi ya kipigo cha mabao 1-3 kutoka kwa Fulham, akitaka kumlinda ili aweze kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Jumatano wiki hii dhidi ya Lyon.
Kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Ireland, Whelan, 48, aliyeshinda mataji 12 katika kipindi chake chote cha kucheza soka alisema: "Kuna jambo haliko sawa kwa kocha, amelenga zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa.
"Anataka kushinda Kombe Ulaya ili aweze kupata kazi Ulaya. Kwangu mimi, nasema siku zake zinahesabika Liverpool.
"Kwanini baada ya ushindi mzuri dhidi ya Manchester United, unarudi tena nyuma baada ya kufungwa na Arsenal kwenye Kombe la Ligi pia? Sioni kama kuna maana."
Whelan, alikuwa akiongea kupitia kituo cha televishen cha Ireland, aliongeza: "Anawapumzisha wachezaji ambao ni wazi wanaweza kucheza na kumpa ushindi.
"Anafanya hivyo kwa sababu ana mchezo mkononi Jumatano."Nilipoiona timu nikadhani hataki kuisumbua. Anachukua mayai yote na kuyaweka kwenye kikapu, sielewi kwanini amefanya hivyo.
Benitez alimpumzisha Torres wakati matokeo yakiwa 1-1. Liverpool ilijikuta kwenye wakati mgumu kwenye mechi hiyo baada ya wachezaji wake wawili kutolewa nje kwa kadi nyekundu--Philipp Degen na Jamie Carragher.
Ni mechi ya nane kupoteza Liverpool, na ya sita katika mechi saba walizocheza.
Wako nyuma kwa pointi tisa dhidi ya wanaoongoza ligi Chelsea, huku pia matumaini kutwaa ubingwa wa ligi kuu yakiendelea kuyumba, na huenda kipigo dhidi ya Lyon Jumatano wiki hii kitahitimisha kibarua cha Benitez.
Lyon itakwenda kwenye hiyo ikiwa na matumaini makubwa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya St Etienne.
No comments:
Post a Comment