Thursday, November 26, 2009

Wagombea Simba wapigwa mkwara

Na Badru Kimwaga
BAADHI ya wanachama wa klabu ya soka ya Simba wamewataka viongozi wa sasa wa klabu hiyo wenye dhamira ya kurejea tena madarakani wajitokeze kugombea, lakini wawe na majibu ya ahadi zao walizoshindwa kuzitekeleza.
Wanachama hao walisema kuwa kabla viongozi hao hawajawaomba kura siku ya uchaguzi huo ni lazima waambie zile ahadi zao walizotoa mwaka 2006 ziliishia wapi na kuwaridhisha ili wawapigie tena kura kurejea uongozini.
Mmoja wa wanachama waliotoa 'mkwara' huo ni Zubeir Mpacha mwenye kadi namba 297, aliyesema viongozi wao wa sasa walitoa ahadi kemkem ambazo hakuna iliyotekelezwa na hivyo wanataka kwanza majibu yake.
Mpacha alisema viongozi hao waliahidi kujenga kisima, kuifanya Simba kama Zamalek, kulikarabati jengo na nyingine ambazo hakuna hata moja iliyotekelezwa, hivyo watakaowania tena uongozi wawaje majibu wawape kura.
"Tumesikia wakitangaza kuja kuwania tena uongozi, tunawakaribisha, lakini tunataka kabla ya kutuomba kura watueleze ahadi zao ziliishia wapi kama hawana majibu ni bora watulie makwao," alisema Mpacha.
Mwanachama mwingine, Issa Said Ruchaki 'Masharubu' (2511) alisema kwa vile katiba inawaruhusu viongozi hao kuomba tena, wajitokeze ila wafanye kazi ya ziada kuwashawishi wanachama kupata kura zao uchaguzi huo ujao.
Pia aliutaka uongozi huo kabla ya kuitisha uchaguzi huo uitishe mkutano wa wanachama ili ijulikane watafanya uchaguzi huo kwa katiba ipi kwa kuhofi kuna uwezekano Simba ikaingia kwenye mgogoro wa kikatiba baadae.
Viongozi wa sasa walitangaza dhamira ya kuwania uongozi katika uchaguzi huo ujao ni Mwenyekiti Hassan Dalali na Makamu wake, Omar Gumbo, huku wanachama wengine Ismail Aden Rage na Bossy Matola nao 'wamejitosa' pia.
Uchaguzi huo wa Simba unatarajiwa kutangazwa rasmi Jumamosi ijayo baada ya kufanyika kwa kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo, ambacho hata hivyo zipo habari kuwa kimeahirishwa.

No comments:

Post a Comment