*Waambiwa muda wao umekwisha
Na Badru Kimwaga
UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba chini ya Mwenyekiti wake, Hassani Dalali, umepigwa marufuku kuingia mkataba wowote na mtu, kampuni au taasisi yoyote kutokana na kumaliza muda wa wa uongozi tangu juzi.
Kwa mujibu wa barua iliyonaswa na Alasiri usiku wa kuamkia leo na iliyotiwa saini na Mdhamini wa klabu hiyo anayetambuliwa na serikali, Abdulwahab Abbas, ni kwamba uongozi huo wa Simba hauruhusiwa kuingia mkataba wowote kwa sasa kutokana na muda wao wa madarakani kumalizika.
Barua hiyo ya wazi, inasema kuwa kwa vile uongozi wa Simba uliingia madarakani Desemba 3, 2006 kwa mujibu wa katiba muda wao umemalizika juzi Desemba 3, 2009.
"Kwa maana hiyo iliyokuwa Kamati ya Utendaji au mjumbe wake hana uwezo wa kisheria kuingia mkataba wowote na mtu, kampuni au taasisi yoyote na mkataba huo ukawa na nguvu kisheria," sehemu ya barua hiyo inasomeka.
Barua hiyo ikatahadharisha kuwa, kwa vile kuna fununu za uongozi huo wa Simba kutaka kuingia mkataba wa muda mrefu wa kupangisha jesho la klabu yao lililopo mtaa wa Msimbazi, ni vema umma ukawa chonjo usilizwe.
"Yeyote atakayeingia mkataba na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kamati ya utendaji au chombo chochote kinachodai kufanya kazi kwa niaba ya kamati hiyo ya uongozi itakuwa imekula hasara kwani haitatambuliwa au kuhusika na mkataba huo wala kurudishiwa fedha zitakazotolewa kutimiliza mkataba huo,"
Blog hii ilijaribu kuwasiliana na Mwenyekiti Hassani Dalali kutaka kujua kama imeshaipata barua hiyo na ana maoni gani juu ya tahadhari hiyo, lakini simu yake ya mkononi haikuwa hewani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment