Saturday, December 5, 2009

Ratiba Kombe la Dunia 2010

IVORY COAST KUNDI GUMU
*Wenyeji kufungu dimba na Mexico
CAPE TOWN, Afrika Kusini

WAKATI wenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Dunia, Afrika Kusini wakianza kupamba historia ya michuano hiyo kufanyika Afrika kwa mara ya kwanza kwa kufungua dimba dhidi ya Mexico, mambo ni magumu kwa wawakilishi wengine wa Afrika, Ivory Coast ambayo imejikuta kwenye kundi gumu la fainali hizo zitakazoanza katikati ya mwaka ujao.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotewa jana na Shirikisho la Kimataifa la Soka Ulimwenguni-FIFA, Afrika Kusini iko Kundi A, sambamba na waliowahi kuwa mabingwa mwaka 1998 na washindi wa pili wa fainali zilizopita, Ufaransa na Uruguay.
Lakini kimbembe kiko Kundi G, ambako wawakilishi wa Afrika wanaotegemewa kufanya vizuri, Ivory Coast imejikuta kundi moja na Brazil--mabingwa wa mara tano wa fainali hizo, Ureno na Korea Kaskazini.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa, mechi ya ufunguzi itachezwa Juni 11, mjini Johannesburg kwenye uwanja wa Soccer City, na mechi ya fainali ya michuano hiyo ya 64 katika mtiririko wa kufanyika kwake, itachezwa kwenye uwanja huo huo, Julai 11.
Mabingwa Ulaya, Hispania ambao wanaongoza kwa ubora wa viwango kwa mujibu wa FIFA, wako Kundi H, sambamba na Uswisi, Honduras na Chile.
Tayari kocha wa Hispania, Vicente Del Bosque, ameshatamba kufanya vizuri kwenye kundi lake. "Hatuwezi kulalamika. Hatuwezi kuficha ukweli, sisi ni moja ya timu zenye uwezo mkubwa," alisema wakati akiongea na Sky Italia.
Lakini inaweza kujikuta kwenye wakati mgumu na kukutana na timu za Brazil na Ureno katika hatua ya 16-bora kutoka Kundi G.
Mabingwa watetezi, Italia, waliowachapa Ufaransa kwenye mechi ya fainali za mwaka 2006 nchini Ujerumani, wako kwenye kundi jepesi wakiwa na Paraguay, New Zealand na Slovakia wanaounda Kundi F.
Ujerumani nayo iko kwenye kundi gumu, ikijumuishwa na timu za Australia, Serbia na mwakilishi mwingine wa Afrika, Ghana wakiunda Kundi D.
Kwa upande wao, England watakumbana na Marekani waliowachapa bao 1-0 katika fainali za kukumbukwa za mwaka 1950, pamoja na Algeria na Slovenia Kundi C.
Upangaji wa ratiba hiyo ulishuhudiwa na rais wa sasa wa Afrika Kusini Jacob Zuma, viongozi wa FIFA akiwemo katibu mkuu Jerome Valcke na msanii wa filamu wa Afrika Kusini Charlize Theron.
Rais Zuma akiongea katika hafla hiyo alisema, ana hakika safari hii Kombe la Dunia litabaki Afrika kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, katika historia ya mashindano hayo, hakuna timu kutoka Afrika iliyowahi kufika nusu fainali.

No comments:

Post a Comment